Mauaji yalivyotokea, nani kahusika -2

Muktasari:

Katika toleo la jana tuliona jinsi mtoto George Stinney (14) alivyohukumiwa kifo na akanyongwa kwenye kiti cha umeme. Hiyo ilifuatia kutiwa hatiani kwa mauaji ya watoto wawili wa kizungu yaliyotokea Machi 24, 1944. Hata hivyo, baada ya kifo chake imekuja kubainika kuwa hakuhusika kwenye mauaji hayo. Lakini kama hakuwaua, nini hasa kilitokea siku hiyo?

Katika toleo la jana tuliona jinsi mtoto George Stinney (14) alivyohukumiwa kifo na akanyongwa kwenye kiti cha umeme. Hiyo ilifuatia kutiwa hatiani kwa mauaji ya watoto wawili wa kizungu yaliyotokea Machi 24, 1944. Hata hivyo, baada ya kifo chake imekuja kubainika kuwa hakuhusika kwenye mauaji hayo. Lakini kama hakuwaua, nini hasa kilitokea siku hiyo?

Kulingana na simulizi kadhaa, Ijumaa hiyo kulipambazuka kukiwa na mawingu. Ilikuwa ni majira ya baridi na mvua katika eneo la Kaunti ya Clarendon, South Carolina.

Betty June Binnicker (11) aliporudi kutoka shuleni, kwa kuwa mama yake alikuwa kazini, alimwomba dada yake akaendeshe baiskeli pamoja na mtoto jirani yao, Mary Emma Thames (7). Alikubaliwa kwa kuwa hali ya usalama iliruhusu watoto huko Alcolu kuwa peke yao mbali na nyumbani.

Muda wa alasiri watoto hao wawili walianza safari kwa baiskeli. Walibeba pia mkasi wa kukatia maua aina ya ‘maypop’.

Baada ya muda mfupi walifika kwenye maeneo ambayo yalikuwa maarufu kwa makazi ya Wamarekani weusi. Hapo ndipo walipokutana na George akiwa na Amie Ruffner. Watoto hao wawili walikuwa wakichunga ng’ombe wa familia hiyo aliyeitwa ‘Lizzie’.

Wakiwa wamekaa kwenye nyasi wakitazama ng’ombe wao akila majani, George na Amie waliwaona wasichana wadogo weupe wakiendesha baiskeli. Wasichana hao walisimama kuwauliza George na Amie kama wanajua mahali ambapo wangepata maua ya ‘maypop’. Walijibiwa kwamba yangeweza kupatikana eneo la karibu na njia ya reli, jirani na nyumbani kwa akina Stinney.

Wasichana hao wawili waliendelea na safari yao ya kutafuta maua huku George na Amie wakiendelea kumchunga ng’ombe wao. Baadaye George akajaza maji kwenye ndoo kumnywesha kisha kumrudisha kwenye zizi lake.

George na Amie walibaki nyumbani wakimngojea mama yao na kaka yao Charles warudi kutoka dukani. Mama yao hakuwaruhusu kamwe watoto wake wawe mbali peke yao, hivyo George alikuwa nyumbani mara baada ya kumrudisha ng’ombe.

Baadaye, familia ya Stinney ilikwenda kwenye karamu iliyofanyika jirani na kwao, na wakiwa katika sherehe hiyo hawakujua kwamba, wasichana wawili wa kizungu walikuwa wamepotea nyumbani kwao na wanatafutwa.

Kwa familia ya Stinney, hiyo ilikuwa siku ya kawaida tu. Lakini, katika sehemu ya Alcolu ambako wasichana hao wawili waliishi, haikuwa ya kawaida. Hata ilipofika jioni ya siku hiyo, Betty June na Mary Emma hawakurudi nyumbani.

Mama yake Betty alirejea nyumbani karibu saa 10:30 jioni na mara moja akahisi kuna kitu kibaya kimetokea. Haikuwa kawaida kwa binti yake kuondoka nyumbani na asirudi ndani ya nusu saa.

Binnicker na binti yake mkubwa walianza kumtafuta Betty, na walipomkosa, mama alijawa na hofu na akakimbia kuripoti polisi huko Manning. Usiku ulipoingia, habari kwamba watoto hao wawili wamepotea zilizidi kusambaa eneo lote la Alcolu. Zaidi ya wakazi 100 wa eneo hilo, weusi na weupe, walijiunga na kikundi cha kuwatafuta kilichoongozwa na mtu aliyeitwa Ben Alderman.

Wakiwa kwenye karamu kwa jirani yao, familia ya Stinney ilipata habari za kupotea kwa wasichana hao, hivyo George na baba yake walijiunga kwenye kikosi cha kuwatafuta.

Baada ya kupokea simu saa nne usiku, Naibu Mkuu wa Polisi wa Kaunti ya Clarendon huko Manning, Henry Newman alifika kusaidia. Kwa wengi huo ulikuwa ni mkesha wa kutisha siku hiyo. Kadiri muda ulivyozidi kusogea, hakukuwa na dalili ya kuonekana kwa Betty June au Mary Emma.

Francis Batson, mwenye umri wa miaka 16 alijiunga na kikundi cha kuwatafuta wasichana hao. Saa tisa usiku watu wazima walimwambia arudi nyumbani kulala. Francis alitii lakini alipofika nyumbani hakuweza kupata usingizi.

Alitoka nyumbani na kuungana na watu wengine kuendelea kutafuta. Hatimaye yeye alikuwa ndiye mtu wa kwanza kuiona baiskeli ya wale wasichana ikiwa kwenye shimo lililojaa maji.

Alipochungulia kwenye shimo aliiona miili ya wasichana hao. Baiskeli ilikuwa imevunjwa sehemu na gurudumu la mbele liliondolewa. Ilionekana kuwa muuaji alikuwa na uwezo wa kutenda kwa utulivu, kwa makusudi, na akiwa ametulia.

Sidney Pratt, ofisa katika kikosi cha Serikali, alifika eneo la tukio. Katika upelelezi wake, alipata habari kuwa jana yake George alionekana akizungumza na wasichana hao, na kwa sababu hiyo kuna uwezekano mkubwa anahusika. Wapelelezi walikwenda hadi nyumbani kwa Stinney. Huko Pratt na mwenzake Henry Newman waliivamia nyumba hiyo na kumkamata George na kaka yake John (19). Wakawaweka kizuizini na kuwasafirisha hadi Kaunti ya Clarendon kwa mahojiano, na George akasisitiza kuwa hana hatia.

Baadaye, kwa njia za kuteswa na kudanganywa, Pratt na Newman walimshawishi aungame ili aachiwe, jambo ambalo George alilifanya.

George alikuwa peke yake katika jela bila msaada wowote. Alitengwa kabisa na ulimwengu kiasi kwamba hata wazazi wake hawakuruhusiwa kumwona. Alikuwa bado mtoto akihojiwa na watu wazima waliomlazimisha kukiri kosa. Wao walikuwa weupe na yeye alikuwa mweusi, tena kipindi ambacho ubaguzi wa rangi uliota mizizi na kushamiri.

Wapelelezi wawili waliouliza maswali walikuwa wanasheria wenye uzoefu mkubwa huku George akiwa peke yake bila mwakilishi wa kisheria.

Walimdanganya kuwa iwapo angeungama, basi angerudi tena kwenye familia yake na kuendelea na maisha kama kawaida. Lakini, haikuwa hivyo.

Baadaye Pratt aliandika taarifa ya uchunguzi akasema George alimbaka mmoja wa wasichana hao, na kwamba “wanaume weusi walitamani kumiliki miili ya wanawake weupe” na kwa sababu hiyo mvulana mweusi aliwafanyia ukatili wasichana weupe.

Hii peke yake ilimfanya George asionewe huruma, na raia wengi wa eneo hilo na walikuwa tayari kumuua iwapo wangeweza kumpata.

Habari za kukamatwa zilienea haraka, na Pratt alikuwa akiuliza maswali katika mitaa ya Manning kuhusu uvumi wa ubakaji. Hii iliwakasirisha wazungu wengi na baadhi yao wakawa tayari kwenda kuvunja jela ili wamuue George.

Kwa kuhofia uwezekano wa shambulio dhidi ya jela, polisi walimhamisha George na kumpeleka maili 15 kutoka eneo hadi Kaunti ya Sumter. Hapa alibaki akiwa amehifadhiwa kwa siri hadi kesi yake ilipotajwa mwezi mmoja baadaye.

Kwa jinsi hali ilivyokuwa mbaya, familia nzima ya Stinney ililazimika kuhama makazi. Familia hiyo ilichukua tahadhari ya kuondoka nyumbani kwao mmoja baada ya mwingine kwa ajili ya usalama.

Jukumu moja muhimu la kisheria lilibaki kwa mamlaka. Kabla ya kufanyika mazishi ya wasichana waliouawa, miili ilifanyiwa uchunguzi na madaktari. Ripoti ilieleza kwa kina majeraha ya kikatili kichwani na usoni yaliyosababishwa na kitu kilichodhaniwa ni nyundo. Hakukuwa na michubuko mingine mahali pengine katika miili yao.

Ripoti iliwasilishwa kwa baraza la mahakama la watu sita; nao wangetuma matokeo na mapendekezo kwa mwendesha mashtaka wa kaunti.

Tofauti na wapelelezi Pratt na Newman, madaktari hawakupata ushahidi wowote wa kubakwa. Katika ripoti hiyo, madaktari waliandika: “...sehemu za siri zilikuwa shwari.” Lakini bado wapelelezi Pratt na Newman walisisitiza wasichana hao walibakwa.

Nini zaidi kiliendelea baada ya tukio hili? Fuatilia zaidi kesho.