George Stinney Siri ya kunyongwa bila hatia-1

Muktasari:

Ijumaa ya Juni 16, 1944 ilikuwa ni moja ya siku za huzuni na zilizoacha kumbukumbu zisizofutika kwa ndugu na jamaa. Kwa nini? Ndiyo ilikuwa siku maalumu ya kunyongwa kwa watu waliotiwa hatiani na kuhukumiwa kifo katika Jimbo la South Carolina.

Ijumaa ya Juni 16, 1944 ilikuwa ni moja ya siku za huzuni na zilizoacha kumbukumbu zisizofutika kwa ndugu na jamaa. Kwa nini? Ndiyo ilikuwa siku maalumu ya kunyongwa kwa watu waliotiwa hatiani na kuhukumiwa kifo katika Jimbo la South Carolina.

Mtoto mdogo mwenye sura ya upole, George Junius Stinney (14) alikuwa miongoni mwa waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa. Alikuwa mwenye umri mdogo zaidi mwenye asili ya Afrika, kunyongwa nchini Marekani katika karne ya 20.

Hukumu hiyo ilitolewa baada ya kupatikana na hatia ya kuwaua wasichana wawili. George alinyongwa kwenye kiti cha umeme katika tukio ambalo lilikuwa na huzuni kubwa. Lakini baadaye ilikuja kubainika kuwa mtoto huyo hakuhusika na mauaji ya watoto wenzake hao na hakukuwa na ushahidi usio na shaka, bali wa mazingira.

Nini kilitokea?

Miezi mitatu kabla ya hukumu hiyo, Machi 24, 1944 yalifanyika mauaji ya watu wawili katika Kaunti ya Clarendon, takriban maili 50 Kusini Mashariki mwa mji wa Columbia. Wasichana wawili wa kizungu -- Betty June Binnicker (11) na Mary Emma Thames (7) walikutwa wameuawa kwa na kipigo. Stinney, Mmarekani mweusi alikamatwa haraka akituhumiwa kumuua mmojawapo.

Ghadhabu ilitanda katika kaunti hiyo saa chache baada ya kukamatwa. Raia walitaka kumuua Stinney haraka bila kupoteza muda kwa kusubiri kesi mahakamani.

Madaktari wawili walizifanyia uchunguzi maiti za wasichana hao na kuwasilisha matokeo yao mahakamani. Ripoti ilionyesha kuwa wasichana hao waliuawa.

Kwa sababu mahakama ya jinai kwenye kaunti hiyo haikuratibiwa kukutana kwa miezi mingine mitatu, muhula maalumu uliitishwa mwishoni mwa Aprili 1944 na mahakama hiyo iliketi Aprili 24, 1944. Baraza la majaji liliziondoa kesi saba ndogo za jinai ambazo zilipaswa kuendelea kusikilizwa kisha katika kilele cha kikao maalumu, ikageukia kesi ya Stinney.

Baraza hilo lilijadili shauri hilo chini ya dakika kumi, kisha likaamua kuwa Stinney alikuwa na hatia kwenye kesi hiyo. Jaji mfawidhi alitangaza hukumu hiyo ya kifo na akaweka na mkazo kuwa itekelezwe ifikapo Juni 16, 1944.

Stinney alisafirishwa hadi kwenye gereza la Serikali huko Columbia na kuwekwa sehemu iliyotengwa na salama zaidi ndani ya gereza hilo iitwayo ‘Tier F’ ambayo ni daraja lililohifadhi wanaume wengine watano. Mmoja wao alinyongwa kwenye kiti cha umeme siku moja na Stinney.

Siku chache kabla ya kunyongwa, wafungwa wa ‘Tier F’ walisemekana kutumia muda wao mwingi kusoma biblia na kuimba nyimbo. Mmoja kati ya wafungwa watano ambaye umri wake ulikuwa umesogea kidogo alimpa Stinney biblia, ambayo inasemekana aliisoma sana wakati huo.

Picha mbili za Stinney zilizopigwa na mpiga picha wa idara ya usimamizi wa gereza zinamwonyesha mtoto huyo amevalia mavazi ya jela akiwa na uwezekano kwamba alikuwa hajabalehe. Kufuatia itifaki ya Serikali kunyonga wahalifu, asubuhi ya Juni 7, wakuu wa gereza walimwondoa Stinney na mfungwa wa pili kutoka ‘Tier F’ na kuwahamishia kwenye ‘nyumba ya kifo’. Hili lilikuwa eneo la mauaji tangu 1912.

Siku nne baada ya kuhamishwa, ndugu kadhaa wa Stinney walimtembelea katika seli yake ya kifo. Hii inaweza kuwa tukio pekee tangu kukamatwa kwake mwishoni mwa Machi, ambapo alionana na watu wa familia yake. Mara kwa mara kasisi mweupe Mmarekani wa gereza hilo na kasisi mweusi walimtembelea yeye na mwenzake.

Angalau katika tukio moja, kasisi mweupe aliripoti kuwakuta vijana hao wawili wakisoma biblia na kuimba nyimbo. Wote walimhakikishia kwamba “kiroho” walikuwa tayari kufa.

Maombi ya kuokoa maisha ya Stinney yalikuwa yakitumwa katika ofisi ya gavana kutoka maeneo mengi ya South Carolina na pia kutoka majimbo mengine, lakini barua na telegramu hazikubadili chochote kuhusu hukumu ya mahakama.

Siku moja kabla ya kuuawa kwa Stinney, wale makasisi wawili walimtembelea tena. Kulingana na habari za magazeti, Stinney alilala fofofo usiku wa mwisho wa maisha yake. Vilevile asubuhi ile ya kuuawa kwake, makasisi hao walimtembelea kwa mara ya mwisho, na baadaye wakaripoti kuwa alikuwa ‘ametulia’ kabisa.

Saa 1:00 asubuhi, ikiwa ni nusu saa kabla ya muda wa kuwekwa kwenye kiti cha umeme na kumuua kwa shoti, Mkuu wa Kaunti ya Clarendon aliingia katika seli na kufanya naye mahojiano ya mwisho:

Sheriff: George, unajua kwamba una muda mfupi tu wa kuishi, sivyo?

Stinney: Ndiyo bwana.

Sheriff: Je! kulikuwa na mtu mwingine yeyote uliyeunganishwa naye au anayejua chochote kuhusu mauaji haya?

Stinney: Hapana, bwana.

Sheriff: Naam, kwaheri George.

Stinney: Kwaheri Sheriff.

Msafara wa wanyongaji na walinzi wanne walimchukua Stinney kwenda kumnyonga. Akiwa amevaa soksi bila viatu, Stinney alitembea ameshika biblia mkononi. Kwa kuwa alikuwa mdogo, hakutosha kwenye kiti maalumu cha umeme, hivyo alikalishwa juu ya ile biblia kwenye kiti ili kichwa chake kifikie eneo la kufunika kichwa.

Stinney aliketi kwenye kiti cha kukatisha uhai wake na walinzi wakimfunga kamba, lakini udogo wake ulifanya kazi hiyo kuwa ngumu, hasa wakati wa kubandika vishikizo vya kiti cha umeme kwenye miguu yake.

Walipofanikiwa hatimaye, msimamizi wa gereza alimuuliza Stinney ikiwa angetaka kusema lolote. “Hapana bwana,” Stinney alijibu.

Kasisi mmoja naye alimuuliza, “Hutaki kusema lolote kuhusu ulilofanya?” Stinney akajibu, “Hapana bwana.”

Ndipo ofisa wa gereza aliwasha umeme, ambao ulipeleka volti 2,400 kwenye mwili wa Stinney.

Kinyago kilichofunika uso wake kilikuwa kikubwa mno kiasi kwamba kilidondoka, lakini kikarejeshwa kichwani na umeme ukawashwa tena. Dakika tatu na sekunde arobaini na tano baadaye daktari wa gereza alitamka kuwa George Junius Stinney amefariki.

Mwili mdogo wa George Stinney ulifunguliwa kamba, ukainuliwa kutoka kwenye kiti cha umeme, na kuondolewa kwenye chumba cha kifo. Miaka 39 baadaye, ofisa wa gereza, James Gamble, alikuja kueleza jinsi moyo wake ulivyomuuma na akakiri kwamba “alitaka kutoka kwenye chumba cha mauaji.”

Miaka 60 baadaye, mwaka 2004, dada yake mkubwa alikumbuka alichosema katika mahojiano ya redio, “Nakumbuka nilikwenda kwenye mazishi. Sikuamini walichokuwa wamemfanyia huyu mtoto. Sitasahau kamwe jinsi alivyoonekana.”

Miaka kumi baada ya hapo, mwaka 2014, dada yake mwingine alieleza kwamba “mwili ulikuwa umeunguzwa, umechomwa moto; ngozi yake ilikuwa imegeuka rangi ya bluu.”

Siku ile ya hukumu, Wamarekani weupe walipanga kumkamata na kumuua Stinney ikiwa baraza la majaji halingemtia hatiani.

Licha ya kifo hicho, maswali yasiyo na majibu yalisalia: Kwa nini mtoto wa miaka 14 alishtakiwa katika mahakama ya uhalifu ya watu wazima? Je, kulikuwa na ushahidi kwamba ndiye aliyeua?

Je, alipimwa afya ya akili? Je, NAACP, shirika ambalo lilifanikiwa kushinda rufaa baada ya kesi zisizo za haki za kimahakama dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika, hadi kufikia Mahakama ya Juu ya Marekani, lilichukua hatua gani katika tukio hili? Kwa nini halikushiriki katika kesi hii?

Je, kesi hiyo iliathiriwa kwa kiasi gani na hali ya ubaguzi wa rangi nchini humo? Zaidi ya yote, je, Stinney Junius Stinney alikuwa na hatia ya uhalifu alioshtakiwa na hata kuhukumiwa kifo?

Je, ilikuwaje akashtakiwa kwa kumuua msichana mmoja badala ya wawili wakati wote wawili walikutwa mahali pamoja wakiwa wameuawa na mauaji hayo yalifanyika wakati mmoja na sehemu moja? Nini hasa kilitokia ile Ijumaa ya Machi 24, 1944?

Fuatilia mfululizo wa mkasa huu ambao kwa sasa dunia inaitazama hukumu ya mtoto huyo na tukio zima kwa sura tofauti, kesho.