Mauaji ya Mchina yatikisa ajira za wafanyakazi 200
Baadhi ya waombolezaji wakiwa wamefika kwenye msiba wa mmiliki wa kiwanda cha XIL LI, Bhaozang Ge uliopo Mabibo Sokoni ndani ya kiwanda hicho
Muktasari:
- Wafanyakazi wa kiwanda hicho wameathirika baada ya kuuawa kwa mmiliki wake, shughuli zimesimama kutokana na msiba kuwepo ndani ya kiwanda, familia inasubiriwa kuamua hatma ya kampuni na ajira za wafanyakazi.
Dar es Salaam. Wafanyakazi zaidi ya 200 wa kiwanda cha XIL LI kilichopo Mabibo Sokoni, jijini Dar es Salaam wameingia katika sintofahamu kufuatia kusimama kwa shughuli zote za uzalishaji baada ya kuuawa kwa mmiliki wa kiwanda hicho, Bhaozang Ge (50), raia wa China.
Bhaozang Ge ambaye alikuwa akiishi ndani ya kiwanda hicho, anadaiwa kuuawa usiku wa kuamkia Mei 16, 2026 baada ya kushambuliwa na walinzi binafsi wa kiwanda chake na mwili wake kutupwa ndani ya mtaro uliopo kiwandani humo.
Msiba unaendelea katika eneo la kiwanda hicho.
Pia, walinzi hao walionekana wameondoka na begi la pesa ambalo linasadikiwa kuwa na Sh10 milioni kwa ajili ya kuwalipa wafanyakazi pamoja na wauzaji makopo wanaopeleka bidhaa hiyo katika kiwanda hicho.
Kifo hicho kilithibitishwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum Mei 19, 2026 ambapo upelelezi wa tukio hilo unaendelea.
Hadi sasa shughuli zote ndani ya kiwanda hicho zimesimama huku mamia ya wafanyakazi wakisubiri hatma ya ajira zao na mwendelezo wa uzalishaji katika kiwanda hicho kinachotegemewa na familia nyingi kwa maisha yao ya kila siku.
Akizungumza na Mwananchi leo Mei 21, 2026 mhasibu wa kiwanda hicho, Evershophy Michael amesema tangu kutokea kwa tukio hilo shughuli zote zimesimama jambo lililosababisha hasara kubwa kwa kampuni pamoja na wafanyakazi waliokuwa wakitegemea kipato chao cha kila siku kiwandani hapo.
“Ajira zimesimama kwa muda hata sisi hatujui tutapangaje maisha kwa sasa, hapa tulikuwa tunasafirisha mizigo mingi kwenda nje ya nchi, lakini kila kitu kimesimama,” amesema Eversophy.
Baadhi ya waombolezaji wakiwa wamefika kwenye msiba wa mmiliki wa kiwanda cha XIL LI, Bhaozang Ge uliopo Mabibo Sokoni ndani ya kiwanda hicho
Eversophy amefafanua kuwa kusimama uzalishaji hata kwa siku hizo chache kumesababisha hasara kutokana na oda zilizokuwa zimepokelewa kutoka kwa wateja mbalimbali.
Amesema wapo ambao walilipa pesa zao zote kwa ajili ya kupelekewa bidhaa walizohitaji na wengine walitoa nusu.
“Kwa siku hizi chache kiwanda kusimama tayari ni hasara kubwa, hatujui mpaka sasa shughuli zitaanza lini tena maana hadi ndugu wakae wajadiliane na kuamua hatua watakazochukua,” amesema.
Amesema kwa sasa wafanyakazi na viongozi zaidi ya 200 wa kampuni wanasubiri kuwasili kwa familia ya marehemu kutoka China akiwemo mke wake ambaye ameanza safari leo Mei 21 na anatarajiwa kuwasili kesho Mei 22, 2026 kwa ajili ya kuendelea na taratibu za msiba pamoja na maamuzi yatakayohusu mwenendo wa kampuni hiyo.
Msimamizi wa wanawake kiwandani hapo, Jasmin Ally amesema wameathirika pakubwa kwani kila Jumamosi huwa vibarua wanalipwa na wengine wanalipwa mwisho wa mwezi.
"Hatuelewi itakuwaje na hatuna uhakika nani ataendelea na kazi baada ya mazishi, maana wenyewe wamesema wakifika watakaa na kisha watatupa majibu juu ya uamuzi wao,"amesema Jasmin.