Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matumizi matairi chakavu tishio nchini

Muktasari:

  • Licha ya umuhimu wa tairi katika magari, kumekuwa na uuzaji na matumizi holela ya bidhaa hiyo, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa ajali nyingi nchini.


Dar es Salaam. Licha ya umuhimu wa tairi katika magari, kumekuwa na uuzaji na matumizi holela ya bidhaa hiyo, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa ajali nyingi nchini.

Kumekuwa na ajali nyingi zinazotokana na tairi kupasuka aidha kwa uchakavu wake au kwisha kwa muda wake wa matumizi huku kukiwa hakuna udhibiti wa kutosha kwenye biashara hiyo.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kuanzia Agosti 30, mwaka huu umebaini kuwepo kwa biashara holela ya matairi ambayo muda wake wa matumizi umekwisha, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa watumiaji wa vyombo vya moto.

Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2020, jumla ya ajali za barabarani zilizotokea nchini zilikuwa 1,933, kati ya hizo zilizosababisha vifo ni 1,031 ambapo watu 1,384 walipoteza maisha na wengine walijeruhiwa.

Licha ya takwimu za Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani kuonyesha kuwa kwa miaka mitano ajali zimekuwa zikipungua, tatizo la kukosa umakini kwa madereva kulichangia sehemu kubwa ya ajali sawa na 1,160, ikifuatiwa na kukosa umakini kwa watembea kwa miguu (379), mwendokasi (288), kukosa umakini wa waendesha baiskeli (162), ubovu wa magari 105 na sababu nyingine.

Athari za matairi chakavu

Ingawa takwimu za Jeshi la Polisi hazitaji moja kwa moja kupasuka kwa matairi kama moja ya vyanzo vya ajali, uchunguzi wa Mwananchi umebaini hilo na kubainisha namna ambavyo umakini katika matumizi ya matairi unaweza kusaidia kupungua kwa ajili.

Hata hivyo, vyanzo vikuu vya ajali vimewekwa katika makundi matatu kwa mujibu wa Jeshi la Polisi –makosa ya kibinadamu, mazingira na ubovu wa gari na katika yote hayo, matairi huchangia kwa kuwa ndiyo mawasiliano kati ya gari na barabara.

Mkuu wa Usalama Barabarani katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi Luis Dar es Salaam, ASP Ibrahim Samwix anasema tairi ndiyo kitu cha kwanza katika usalama wa gari, licha ya kwamba mifumo yote inapaswa kufanya kazi.

“Tairi la gari ni muhimu katika kuzuia ajali, hii ni kwa sababu ndilo linahusika moja kwa moja kwenye makosa ya kibinadamu. Mwendo kasi wa gari unaweza kusababisha tairi kupata moto na kupelekea kupasuka, lakini pia mazingira ya barabara kama uwepo wa mawe au mashimo yanaweza kusababisha ajali,” anasema Samwix.

Anaongeza kuwa mashimo au kuendeshea gari kwenye kingo za barabara kunaweza kusababisha tairi kuchanika, hali ambayo pia inaweza kuwa chanzo cha ajali sanjari na ubovu wa gari au tairi lililoisha kiasi cha kushindwa kuhimili vishindo barabarani.

Hali ilivyo

Licha ya umuhimu wa tairi bora kufahamika na madhara ya bidhaa hizo zisizo na vigezo, imekuwa si rahisi ubora kuzingatiwa na kutumika ndani ya muda unaotakiwa.

Katika uchunguzi wake jijini Dar es Salaam, gazeti hili limebaini maduka kadhaa yenye matairi yaliyoisha muda wake na mengine yaliyotumika.

Mbali na hilo, kuna utaratibu wa watu kununua magari kutoka nje ya nchi na kuyatumia bila kubadilisha matairi, licha ya kuwa yameisha muda wake.

Katika baadhi ya maduka yaliyopo Kariakoo na Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, baadhi ya wauzaji wanasema mbali na ubora wa tairi, kinachoamua bei ya tairi ni muda wake wa matumizi kukaribia kwisha.

Wauzaji hao ambao baadhi waliomba majina yao yasitajwe gazetini, wanakiri kuwaambia ukweli baadhi ya wateja na kukubaliana bei huku kukiwa na wengine wasio waelewa ambao, hulaghaiwa na kuuziwa tairi ama zilizoisha muda au ambazo zinakaribia muda huo.

“Kuna tairi linaweza kuonekana jipya kabisa, lakini lina miaka miwili au mmoja kabla ya kwisha muda wake, usipokuwa mwangalifu unapigwa,” anaonya.

Muuzaji mwingine anasema wapo wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakiwalangua wateja wasio na ufahamu juu ya matairi wanayotaka, ingawa pia wapo wateja ambao shida yao ni zile za gharama nafuu.

Rahisi kuagiza

Kwa mujibu wa Ali Juma, muuzaji wa tairi Kariakoo: “tairi zilizoisha muda hazisumbui kuziingiza, unaweza kuziagiza mwaka mmoja kabla ya muda wake wa matumizi kuisha na ukauza mzigo usiishe, unarudisha stoo unasubiri wateja wanaohitaji mzigo wa namna hiyo.

“Wengi wanazikimbilia kwa kuwa zinakuwa za bei nafuu ikilinganishwa na ambazo zipo ndani ya muda,” anasema.

Anaongeza kuwa hakuna usumbufu wowote wanaupata kutoka serikalini, lakini wateja wengi huelezwa taarifa za tairi kabla ya kuuziwa na huridhia.

“Wengi wao ni wanaokwenda kuuza mkoani,” anaongeza.

Fundi wa kuziba pancha eneo la Kunduchi wilayani Kinondoni aliyejitambulisha kwa jina moja la Nditi, pia huuza tairi zilizotumika ambazo wateja wanakuwa wameziacha wanapokwenda kubadilisha tairi.

“Kuna mabosi wanakuja kuvua tairi hapa wakinunua magari mapya, mengine unakuta bado (matairi) mazima kabisa ila wao wanabadilisha yote, wakiniachia hapa mimi nauza. Unakuta kuna mtu anakuja hapa na tairi yake inamsumbua namuuzia hizo za kusukumia siku. Hata kama muda wake umeisha, kuna wakati zinadumu kuliko hata mpya,” anasema Nditi.

Hata hivyo, uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya tairi hizo chakavu kusafishwa kwa ili kuzifanya zionekane mpya na zingine zikichongwa kuweka kashata kujaribu kumhadaa mteja kwamba, ni tairi ambazo zinaweza kuhimili mikikimikiki ya barabarani.

Nyongeza na Tuzo Mapunda na Imani Makongoro.