Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matarajio ya Watanzania bajeti ya afya ikisomwa bungeni

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu  akizungumza wakati akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/25 ya Sh1.31 trilioni jana Mei 13, 2024 bungeni jijini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu kesho Jumatatu, anawasilisha Bajeti ya Wizara yake kwa mwaka 2024/25 huku baadhi ya wadau wakibainisha matarajio yao.

Dodoma. Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2024/25 leo inawasilishwa bungeni, huku macho ya Watanzania yakisubiri kuona Serikali inamalizaje mvutano uliopo kati ya watoa huduma binafsi na utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya iliyosainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Desemba 2023.

Hoja zinazosubiriwa na Watanzania ni utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, upungufu wa watumishi katika sekta ya afya, matumizi ya vifaa visivyo sahihi kwenye huduma za afya, ufinyu wa bajeti na suluhu ya malalamiko ya Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF).

Bajeti ya wizara hiyo, imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. 2022/23, wizara hiyo iliidhinishiwa Sh1.109 trilioni huku mwaka 2023/24 ikiidhinishiwa Sh1.235 trilioni sawa na ongezeko la zaidi ya Sh1.26 bilioni.

Hata hivyo, licha ya bajeti hiyo kuongezeka kila mwaka, utolewaji wa bajeti usioendana na wakati umekuwa bado ni changamoto inayoikabili wizara hiyo inayoongozwa na Waziri Ummy Mwalimu inayoathiri miradi ya maendeleo.

Februari mwaka huu, Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi ikiwasilisha taarifa yake ya shughuli za mwaka 2023, ilisema fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka 2023/2024, zimetolewa kwa kiwango kidogo.

Kamati hiyo ilisema katika uchambuzi wake hadi Disemba 2023, ni asilimia 26 tu ya bajeti ya mwaka 2023/24, ilikuwa imetolewa kwenye wizara hiyo.

Licha ya hoja hiyo, upungufu wa upatikanaji wa dawa na vitendanishi katika hospitali za umma nchini, nao unaathiri ubora wa huduma zinazopatikana kwenye hospitali za umma.

Kamati hiyo ilisema hali hiyo inasababishwa na utengwaji wa fedha ndogo kwa ajili ya dawa na kupendekeza Bohari ya Dawa (MSD) kupewa mtaji wa Sh592.92 bilioni ili iweze kununua mahitaji yote ya bidhaa za afya.

Katika miaka mitatu mfululizo, bajeti ya ununuzi ya dawa nchini ilikuwa ni Sh218.1 bilioni kwa mwaka 2021/22, mwaka 2022/23 ilitenga Sh200 bilioni na mwaka 2023/24 ziliombwa Sh205 bilioni.

Hoja ya upungufu wa ajira pia nayo itahanikiza mjadala mkubwa wa bajeti hiyo iliyopangiwa siku moja kuwasilishwa, kujadiliwa na kupitishwa na Bunge.

Takwimu zilizopatikana bungeni mwaka huu, zinaonyesha sekta hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa kiwango cha asilimia 64.

Tamko la Sera ya Afya ya Mwaka 2007, linataka uwepo kwa watumishi wa kutosha wenye ujuzi katika taaluma mbalimbali katika ngazi zote za kutolea huduma nchini.


Malalamiko ya NHIF

Bado kuna malalamiko ya huduma zinazotolewa na mfuko wa NHIF ikiwemo mfumo wa utendaji na upangaji wa gharama za matibabu kutokuwa wazi, michango inayotolewa na huduma anayopokea mwanachama kutoendana, baadhi ya watumishi wa umma kuchangiwa asilimia moja na Serikali.

Malalamiko mengine ni NHIF kutoruhusu mnufaika kuweka wategemezi nje ya wazazi, mwenza na watoto, kutokuwa na usawa katika kupata huduma kwa wanufaika pamoja na mfumo wa upangaji wa gharama za matibabu kutojulikana.

Sambamba na changamoto hizo na nyingine, pia kumekuwa na mvutano unaokabili uendeshaji wa mfuko huo na sekta binafsi ya afya,  jambo lililosababisha Waziri Ummy kuunda kamati kwa ajili ya kuchunguza na kuja na mapendekezo yatakayosaidia kuondoa mvutano uliopo.

Aidha, hoja nyingine ambayo wadau wanatarajia kupata majibu kwenye bajeti hiyo, ni kubainika katika maeneo mawili tofauti ya Mkoa wa Shinyanga na Tanga, kuwepo majokofu ya nyumbani yakitumika kuhifadhiwa damu.

Kwa upande wa afya ya akili, katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2022/23, alibaini upungufu kwenye maeneo 12 ya utoaji huduma kwa jamii ikiwamo ongezeko la idadi ya wagonjwa na vifo vinavyotokana na matatizo ya afya ya akili.


Wadau wa afya wanena

Mbunge wa Ndanda (CCM), Cecil Mwambe, amesema wanasubiri kauli ya Serikali kuhusu kuanza utekelezaji wa bima ya afya kwa wote, kwa sababu gharama za matibabu zimekuwa kubwa.

"Kwanza tutataka kusikia kuhusu bima ya afya kwa wote, ambayo imekuwa na utata kwa sababu watu wengi hawajaelewa somo la vitita vilivyopo katika bima hiyo. Gharama za matibabu zimekuwa kubwa jambo ambalo ni changamoto kwa Watanzania walio wengi," amesema.

Amesema pia wanasubiri kuona Serikali imejipangaje kuleta muswada wa marekebisho ya Sheria ya Mfuko wa Bima ya Afya, ili kuondoa malalamiko ya baadhi ya wadau wa mfuko huo ikiwemo sekta binafsi.

Mwambe ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, amesema wanaisubiri Serikali ieleze walipofikia kuhusu utatuzi wa mvutano wao na sekta binafsi.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Elimu ya Juu (THTU), Dk Paul Loisulie amesema wameona upungufu ya NHIF, kupitia tathimini iliyofanywa na kamati ndogo ya chama hicho ambayo yakirekebishwa mfuko huo utakwenda sawa.

Alisema upungufu mwingine unasababishwa na sheria, kanuni na miongozo ambayo kama walivyoshauri Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi inapaswa kuangalia upya sheria iliyoanzishwa mfuko huo.

Amesema kumekuwa na changamoto ya kutokuwa na usawa katika kupata huduma kwa wanufaika wa huduma za mfuko huo, na kutoa mfano kwa wabunge na watumishi wa umma.

“Miongoni mwa madhara ni kukosekana kwa usawa katika upatikanaji wa huduma ya afya na kuufanya mfuko wa bima kuonekana kama unafanya biashara,” amesema.

Amesema ili kutoka hapo kunahitaji majadiliano ya kina, ili kuondoa tofauti hiyo ya usawa kwa wanufaika.



Wataalamu wa afya

Naye Rais Mteule wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema wanashukuru mwaka wa bajeti unakaribia kuisha ambao Bunge liliidhinisha bajeti ya Sh1.2 trilioni kwa Wizara ya Afya.

Alisema wizara hiyo iliainisha kutekeleza vipaumbele 14 na hivyo ni wakati sasa wa kusikia utekelezaji wake umefikia wapi na kilichokwamisha.

"Tunatarajia bajeti hiyo itaongezeka mwaka huu kutoka asilimia tano ya bajeti nzima ya Serikali, hadi kufikia kati ya asilimia 10 hadi 15 ili wizara iweze kutekeleza vibaumbele vyote ilivyopanga," amesema.

Pia amesema wanatamani kusikia katika mwaka wa fedha 2024/25 utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote utakuaje, watu wangapi wanaingizwa na ni huduma gani zitakazokuwepo katika mpango huo.

Amesema pia wanatarajia Serikali itaeleza hatua gani wamefikia, kuhusu kupunguza upungufu wa watu wa afya ambao takwimu zinaonyesha ni zaidi ya asilimia 60.

Dk Nkoronko amesema wanataka kusikia kwenye bajeti hiyo, kuhusu wigo wa huduma za kibingwa na kibobezi nchini umefikia wapi.

Amesema wanataka kusikia huduma za kibingwa zimeimarishwa kwa kiasi gani katika hospitali za rufaa, ambazo zinatakiwa angalau ziwe na madaktari bingwa wasiopungua 14.

Amesema hivi sasa zipo hospitali za rufaa zisizopungua sita, ambazo zina upungufu wa madaktari bingwa kati ya sita hadi saba.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bunge, bajeti hiyo itafuatiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari huku Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ikifunga dimba kwa wiki hiyo.