Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mashamba ya bangi yateketezwa Bunda

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo akiongoza shughuli ya kutetekeza bangi iliyofyekwa kwenye mashamba yenye ukubwa wa zaidi ya ekari nne katika Kijiji cha Mekomariro wilayani Bunda.  Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Wamiliki wa mashamba hayo wamedaiwa kutoroka, hivyo jeshi hilo limetangaza operesheni maalumu ya kuwasaka ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria

Bunda. Jeshi la Polisi mkoani Mara limeteketeza ekari nne za mashamba ya bangi yaliyogundulika Kijiji cha Mekomariro, wilayani Bunda, katika operesheni maalumu ya kudhibiti kilimo na usambazaji wa dawa za kulevya.

Hata hivyo, wamiliki wa mashamba hayo wamedaiwa kutoroka, hivyo jeshi hilo limetangaza operesheni maalumu ya kuwasaka ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza wakati wa kufyeka na kuteketeza mashamba hayo leo Juni 14,2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo amesema jeshi hilo limeanzisha operesheni endelevu kusaka na kuteketeza mashamba ya bangi ndani ya mkoa huo.

"Lengo ni kuteketeza dawa za kulevya zikiwa shambani na hata zikiwa zimechakatwa kiwandani, tunatambua fika kuwa bangi wakati mwingine inachakatwa inawekwa kwenye kete, inakuwa puli na kusafirishwa kwenda mikoa mingine na hata nje ya nchi," amesema.

Askari polisi wakishirikiana na wananchi kufyeka bangi katika Kijiji cha Mekomariro wilayani Bunda mkoaniMara.  Picha na Beldina Nyakeke

"Wananchi watumie maeneo haya kulima mazao yenye tija, kwani tumeona yanafaa kwa kilimo cha nyanya, mahindi, karanga na mengine mengi ambayo yanaweza kuwasidia kuboresha na kuimarisha uchumi wao badala ya kilimo cha bangi ambacho kwa sasa kitakuwa ni hasara kwao kwani hakuna shamba tutakaloliacha," amesema

Amesema kugundulika kwa uwepo wa mashamba hayo kumetokana na ushirikiano kati ya jeshi hilo na wananchi, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano huo, hatua itakayoleta matokeo chanya katika mapambano dhidi ya wahalifu na uhalifu.

Katika hatua nyingine, jeshi hilo linawashilikia watu wanne  wakiwamo watatu wa familia moja kwa tuhuma za kukutwa na majani makavu yanayodhaniwa ni bangi.

Watu hao wakazi wa Kijiji cha Mekomariro wilayani Bunda mkoani Mara wamekamatwa na majani hayo yenye uzito wa kilogram 53.5.

Kamanda Lutumo amewataja watuhumiwa hao Nyangi Mkanga (65), Mwita Mkanga (34), Amos Mkanga na Rhobi Daudi.

Baadhi ya wakazi wa Bunda wamesema bado kuna changamoto ya kilimo cha bangi ndani ya wilaya hiyo, hivyo jitihada zinahitajika ili kukomesha kilimo hicho.

Julius Ikwabi amesema baadhi ya watu wamekuwa wakijihusisha na kilimo hicho kwa ajili ya kujipatia kipato na kwamba ni zao ambalo halina usumbufu wala changamoto kuanzia kilimo hadi mavuno.

"Tunaomba Serikali iangalie namna ya kuwasaidia wakulima hasa vijijini ili wawe na mazao ya uhakika ya biashara kwa sababu kuna changamoto nyingi sana kwenye kilimo biashara kuanzia pembejeo, mabadiliko ya tabia nchi na hata  masoko," amesema.

Isaya Mauma,  amesema Serikali inatakiwa kuwawezesha wananchi ikiwa ni pamoja na kuanzisha kilimo cha umwagiliaji sambamba na kutoa elimu juu ya kilimo cha kisasa.

Nora Obedi amependekeza ushirikishwaji wa viongozi wa Serikali za vijiji katika mapambano dhidi ya kilimo na matumizi ya bangi ndani ya mkoa utakuwa na matokeo chanya.

"Bangi inalimwa mashambani hasa vijijini na viongozi wa vijiji wanajua, kwa hiyo kama watashirikishwa watakuwa na mchango mkubwa wa kukomesha kilimo hiki, watakuwa wanatoa taarifa mapema na wahusika kukamatwa na mashamba kuteketezwa kabla hayajavunwa,"amesema.