Mapato ya misitu yapaa kwa asilimia 43, watalii waongezeka
Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji, akizungumza wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis
Muktasari:
- Waziri Kijaji amesema ongezeko la watalii ni sawa na asilimia 20 ikilinganishwa na watalii 275,723 waliotembelea vivutio vya utalii ikolojia katika kipindi kama hicho mwaka jana, huku mapato yakiongezeka kwa asilimia 43 kutoka Sh2.2 bilioni hadi kufikia Sh3.1 bilioni.
Dodoma. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetajwa kuwa miongoni mwa sekta zilizoongeza idadi ya watalii wa misitu hadi 329,753 na kukusanya zaidi ya Sh3.09 bilioni ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Takwimu hizo zimebainishwa bungeni leo Ijumaa, Mei 15, 2026 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Waziri Kijaji amesema ongezeko la watalii ni sawa na asilimia 20 ikilinganishwa na watalii 275,723 waliotembelea vivutio vya utalii ikolojia katika kipindi kama hicho mwaka jana, huku mapato yakiongezeka kwa asilimia 43 kutoka Sh2.2 bilioni hadi kufikia Sh3.1 bilioni.
Waziri amesema mbali na mafanikio ya utalii, Serikali imeendelea kupambana katika vita dhidi ya uharibifu wa misitu na biashara haramu ya mazao ya misitu, ambapo ilifanya doria za kimkakati 363 na doria za kawaida 12,854 na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 1,925 wa uhalifu wa misitu.
“Kupitia operesheni hizo, Serikali ilikamata na kutaifisha magunia 39,900 ya mkaa, mbao 31,046 zenye ujazo wa mita za ujazo 1,321, magogo 1,556 na mifugo zaidi ya 29,000 iliyokuwa ikiingizwa kwenye maeneo ya hifadhi kinyume cha sheria,” amesema Dk Kijaji.
Katika hatua nyingine amesema TFS imeendelea kuimarisha vita dhidi ya moto wa misitu kwa kutumia teknolojia ya satelaiti kubaini matukio mapema na kutoa mafunzo kwa vikosi 45 vya zimamoto na wananchi zaidi ya 20,000 wanaoishi jirani na hifadhi.
Amesema Serikali imeendelea kuwekeza kwenye upandaji miti na urejeshaji wa mazingira yaliyoharibiwa, na katika mwaka wa fedha 2025/26 TFS imeanzisha mashamba mapya ya miti ya Geita na Rwamgasa yenye ukubwa wa hekta 28,000, sambamba na kuzalisha miche milioni 32.8 ya miti iliyogawiwa kwa wananchi na taasisi mbalimbali kwa ajili ya upandaji.
Amesema katika mwaka wa fedha 2026/27 Serikali itaongeza nguvu katika uhifadhi, utalii na biashara ya mazao ya misitu kwa kuandaa mipango ya usimamizi wa hifadhi 99 zenye ukubwa wa zaidi ya hekta 2.3 milioni, kufanya doria 2,439 na kuimarisha ulinzi wa misitu ya asili, mashamba ya miti pamoja na mikoko.