Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mamia wamzika Zephania Ubwani wa The Citizen

Waandishi wa habari mbalimbali wakiwa kwenye kaburi la mwanahabari mkongwe aliyekuwa akiandikia gazeti la The Citizen, Zephania Ubwani (70) aliyezikwa leo. Picha na mpiga picha wetu

Hanang. Mamia ya watu wamejitokeza kumzika aliyekuwa mwandishi mwandamizi wa gazeti la The Citizen, Zephania Ubwani (70), leo Jumatano Aprili 10, 2024 katika Kijiji cha Simbay, wilayani Hanang, Mkoa wa Manyara.

Ubwani, aliyefanya kazi kwa muongo zaidi ya mmoja na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), alifariki dunia Aprili 6, mwaka huu akiwa kwenye majukumu ya kikazi katika Hoteli ya Kibo Palace, mkoani Arusha baada ya kuugua ghafla.

Alikimbizwa katika Hospitali ya AICC ambako alifariki dunia wakati akifanyiwa uchunguzi.

Mamia hao wakiongozwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mefunya Gipchochiga, waliungana na familia ya Ubwani kijijini hapo kumpumzisha katika makaburi ya familia yao, huku ibada ya mazishi ikiendeshwa na mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Measkron, Mtaa wa Simbay kwa kushirikiana na viongozi wa Usharika wa Kimamdolu, Arusha.

Akimzungumzia marehemu, kiongozi huyo amesema kifo hicho ni pigo kubwa si kwa familia yake wala kijiji pekee, bali na kwa Taifa kwa ujumla.

“Marehemu alikuwa mstari wa mbele kuhimiza maendeleo ya hapa kijijini na wilaya ya Hanang, alitumia muda mwingi kushauriana na wazee na watu wa rika lake katika kuhamasisha maendeleo hadi ya huduma za kijamii na mazingira.

“Alitumia kalamu yake kuandika masuala mengi ya mazingira na uhifadhi na alikuwa mahiri sana katika maeneo hayo," amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), Claud Gwandu alisema kifo cha Ubwani ni pigo kubwa kwa waandishi wa habari wachanga ambao walitumia muda mwingi kuwafundisha na kuwaelekeza masuala mbalimbali ya uandishi wa habari.

“Ubwani alikuwa ni sawa na maktaba, alikuwa na kumbukumbu ya masuala mengi na mambo mengi, alikuwa ni rejea kwa waandishi wengi ambao walikuwa wanataka kujua mambo mbalimbali ya kimazingira na yanayohusiana na nchi za Maziwa Makuu, ni waandishi wachache sana walikuwa na kumbukumbu kama za mzee Ubwani.

"Ubwani alifia kazini na hiyo inadhihirisha jinsi alivyokuwa anajali kazi yake, alipenda taaluma yake na ni mfano wa kuigwa kwa wanahabari wote," ameongeza Gwandu.

Kabla ya kuzikwa, jana wadau mbalimbali wa kitaifa na kimataifa waliongoza waombolezaji katika ibada fupi ya kuuga mwili wa Ubwani, nyumbani kwake eneo la Kimandolu, jijini Arusha.

Ubwani alianza taaluma yake ya uandishi wa habari katika gazeti la Daily News, linalomilikiwa na Serikali, lakini baadaye akahamia kampuni ya MCL.

Ubwani alizaliwa Septemba 12, 1953 na ameacha mjane na watoto wanne.