Prime
Mambo 10 yanayoendeleza ajali za bodaboda

Dodoma. Licha ya jitihada za Serikali za kudhibiti ajali za pikipiki maarufu bodaboda nchini, bado kuna mambo 10 yanayoendelea kusababisha vifo na majeruhi kupitia usafiri huo.
Mambo hayo ni kutovaa kofia kwa waendeshaji na abiria wao, kubeba abiria zaidi ya mmoja (mishikaki), kubeba mizigo mikubwa zaidi, uvaaji viatu kwa waendeshaji na kutojali alama za barabarani.
Mengine ni kung’oa vioo vya kutazama nyuma, kukata vifaa vya kutolea moshi na kusababisha milio mikubwa yenye ushawishi wa kukimbiza chombo, mwendo mkali, ulevi na kukosa mafunzo sahihi ya udereva.
Takwimu ambazo zimekuwa zikitolewa zinaonyesha ajali za pikipiki huchukua karibu asilimia 20 ya ajali zote za barabarani na chanzo chake kikuu ni miongoni mwa mambo hayo 10.
Kulingana na takwimu za Wizara ya Mambo ya Ndani, Julai 2021 hadi Machi 2022, Tanzania ilikuwa na matukio 1,594 ya ajali za barabarani ambapo ajali 300 zilisababishwa na madereva wa bodaboda.
Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) Machi mwaka huu ilieleza kuwa majeruhi tisa hadi 10 wa bodaboda wanapokewa kwenye taasisi hiyo kwa siku.
Hiyo ni sawa na kusema majeruhi 70 hupokelewa kwa wiki na 280 kwa mwezi kutokana na ajali za hizo za pikipiki.
Daktari wa Mifupa katika Hospitali ya Benjamini Mkapa Dk Afred Anold amesema katika wodi ya majeruhi, walio wengi ni ajali za pikipiki ambao ni vijana wa umri wa kuanzia miaka 15 hadi 35 na wengi hupelekwa wakiwa na mivunjiko.
Hata hivyo kumekuwa na juhudi mbalimbali kutoka kwa wadau likiwemo Jeshi la Polisi katika kupambana na mambo yanayochangia ajali hizo, ingawa bado zinapuuzwa na madereva.
Ni bahati mbaya
Mwenyekiti wa Waendesha pikipiki katika Kituo cha Mipango jijini Dodoma, Jumanne Omary anasema suala la ajali halipaswi kuangaliwa kwa upande mmoja wa waendeshaji pekee, hata watumiaji wengine wa barabara wamekuwa ni sehemu ya chanzo chake.
Jumanne alisema mara nyingi watu wameishi kwa kukariri, ikitokea ajali basi wa kulaumiwa ni bodaboda hata katika maeneo ambayo hawahusiki, wao hubebeshwa mizigo hiyo.
“Utakuta kuna dereva wa gari mzembe anakwenda kukusababishia ajali, mtu akishagongwa au kugonga na akifika hospitali wanasema sisi ni wazembe, hivi kwa nini huwa hawataki kuchunguza ajali za bodaboda?” alihoji Jumanne Omary.
Kwa mujibu wa dereva huyo ambaye amedumu kwenye kazi hiyo kwa miaka mitano, anaeleza kuwa hata wao hawapendi kufa wala kupata ulemavu lakini ikitokea ni bahati mbaya.
Agness Stephen, mkazi wa Mpamaa anasema huu ni mwaka wa sita akipanda pikipiki lakini ukweli ni kwamba madereva wengi wanazitafuta ajali wenyewe.
Agness anasema hata dereva anayemwendesha, mara kadhaa humuona akiwa amechangamka kuliko hali kawaida yake na hapo ndipo humtia hasara kwa kuwa akishafika humwambia ameghairi safari, hivyo humlipa fedha za usumbufu na yeye huchagua dereva mwingine.
Alisema anaunga mkono zaidi suala la mwendo kasi kuwa chanzo namba moja cha ajali za pikipiki na pili ni kupuuza alama za barabarani.
Utii wa sheria
Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji kwa njia ya barabara (TAROTWU), Shukuru Mlawa anasema ajali nyingi za pikipiki husababishwa na kudharau au kutokutii sheria za barabarani kwa baadhi ya madereva.
“Ingawa ziko ajali ambazo mtu anasababishiwa, ukweli utabaki kuwa nyingi zinasababishwa na uzembe wa madereva wenyewe kutokuchukua tahadhari na kudharau,” alisema.
Kiongozi huyo anasema vijana wengi wanaoendesha pikipiki hawavai kofia ngumu, hawajali sheria za barabarani, huendesha kwa mwendo kasi hata katika maeneo ambayo hayaruhusiwi huku wengine wakibeba mizigo bila kuzingatia uwezo wa chombo.
Katibu wa Tarotwu Mkoa wa Dodoma, Mussa Nsese anaongeza kuwa ulevi kwa waendeshaji wa vyombo vya moto hususani pikipiki ni jambo lisilokuwa na ubishi miongoni mwa vyanzo vya ajali za vyombo hivyo.
Wabunge na sheria
Mbunge wa Viti Maalumu, Janet Masaburi katika mkutano uliopita wa Bunge alilalamikia ajali za pikipiki akisema zinasababisha ulemavu wa kudumu kwa watu wengi na vifo visivyo na idadi.
Masaburi alitaja chanzo cha yote kuwa ni sheria ya usalama barabarani ambayo inatoa nafasi kwa waendesha pikipiki kufanya wanavyotaka.
Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini alisema Muswada wa marekebisho ya sheria hiyo umeishasomwa kwa mara ya kwanza bungeni lakini ulirejeshwa serikalini kwa ajili ya maboresho.
Sagini alisema hivi sasa muswada huo uko katika hatua za mwisho za marekebisho hasa kwenye maeneo ambayo wabunge waliona yana changamoto na kwamba baada ya maboresho hayo utasomwa mara ya pili na kupitishwa.
Kuhusu madai kuwa Serikali imeshindwa kuwadhibiti bodaboda wasiofuata sheria, Sagini alisema haijashindwa ila walichojifunza tatizo ni namna wanavyoingia kwenye uendeshaji wa vyombo hivyo bila mafunzo lakini Jeshi la Polisi limeanza hatua za kuwapa mafunzo.
Sitasahau ajali ya pikipiki
Miongoni mwa watu wenye kumbukumbu mbaya ya ajali za Bosaboda ni Keneth Chumi wa Ipagala mkoani Dodoma anayeeleza namna ilivyompa ulemavu wa kudumu na kumsababishia mambo yake mengi kukwamba.
Keneth (36) alipaja ajali ya pikipiki katika eneo la njia panda ya Nzuguni akiwa na dereva asiyemfahamu ambaye alipoteza maisha palepale siku ya tukio.
“Nilipanda pipikipi kutoka Nzuguni mashariki nilikokwenda kuangalia biashara ya nguruwe, ile tunaingia barabara ya lami yule kijana hakuchukua tahadhari na kwanza alikuwa mwendo mkali ingawa nilimuonya kabla, kumbe kuna basi dogo linaingia kwetu likatugonga nikarushwa mbali huko, mwenza akaangukia uvunguni mwa gari,” anasema Chomola ambaye alipoteza jicho moja la kulia na mkono wa upande huo kuvunjika.