Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mali za Jaji Mfalila zilivyozua mgogoro wa usimamizi mahakamani

Muktasari:

  • Wanawake wawili wanavutana mahakamani kuhusu usimamizi wa mali za Jaji mstaafu Lameck Mfalila kila mmoja akidai ndiye mke halali wa jaji huyo, lakini mtoto wa Jaji Mfalila na mama yake wa kambo wanamkana mwanamke anayedaiwa alikuwa hawara, ambaye  Mahakama ilimkubali.

Dar  es Salaam/Arusha. Suala la usimamizi wa mali za Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufaa nchini, Lameck Mfalila, anayesumbuliwa na maradhi, limeibua mgogoro baada ya kujitokeza wanawake wawili kila mmoja akidai kuwa ndiye mkewe halali anayestahili kuwa msimamizi.

Awali mwanamke mmoja anayejitambulisha kwa jina la Lenna Mfalila alifungua shauri la maombi Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam, akiomba amri ya kuteuliwa kuwa msimamizi wa mali zake.

Katika shauri hilo la maombi Lenna aliieleza Mahakama kuwa yeye ni mke halali wa Jaji Mfalila, akieleza kuwa jaji huyo amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya akili yanayosababisha apoteze kumbukumbu.

Mahakama hiyo katika uamuzi wake wa Desemba Mosi 2023, ilikubaliana naye ikamteua kuwa msimamizi wa mali zake ikiwamo udhibiti  wa akaunti benki, pensheni, bima ya afya na rasilimali nyinginezo.

Mmoja wa watoto wa Jaji Mfalila, Chellu Mfalila, amefungua shauri la mapitio Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, kuupinga uamuzi huo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi.

Kisha mwanamke mwingine, anayejitambulisha kwa jina la Rehema William Mbulumi au Rehema Mbulumi Mfalila naye alifungua shauri la maombi mahakamani hapo dhidi ya Lenna Mfalila, Chellu Mfalila na Jaji Mfalila mwenyewe.

Katika shauri hilo la maombi, Rehema aliomba kuunganishwa katika shauri la mapitio lililofunguliwa na Chellu, kupinga Lenna kuwa msimamizi wa mali za Jaji mstaafu Mfalila.

Lenna na wakili wake  alipinga Rehema kuunganishwa katika shauri hilo.

Hata hivyo, mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa Desemba 28, 2025 na Jaji Elizabeth Mkwizu imekubaliana na maombi na hoja za Rehema na imeamuru hati ya maombi ilivyofanyiwa marekebisho kwa kujumuisha Rehema iwasilishwe mahakamani ndani ya siku 14.


Aliyoyasema Rehema

Rehema kwa mujibu wa  kiapo chake kilichounga mkono maombi ya kuunganishwa kwenye shauri hilo, ndiye mke halali wa ndoa wa Jaji Mfalila, ndoa waliyoifunga Oktoba 20, 1979, katika Kanisa la Moravian, wilayani Sikonge, mkoani Tabora.

Walifungua ndoa hiyo  kufuatia kifo cha mke wa awali wa Jaji Mfalila, Esther Godfrey Mlela, ambaye ndiye mama wa watoto wa Jaji Mfalila akiwemo Chellu.

Amekuwa akimtembelea nyumbani kwake Tabora anakoangaliwa na binti zake na amekwisha kusafiri naye (Jaji Mfalila) nje ya nchi kwa matibabu, akitumia utaalamu wake kama ofisa wa matibabu.

Oktoba 19,2024, Chellu alimjulisha Rehema kuwa amefungua shauri la kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, wa Desemba Mosi 2023, uliomtangaza Lenna kuwa mke halali wa Jaji huyo na msimamizi wa mali zake.

Rehema alidai alishtushwa na uongo wa Lenna kwa kudai aliwahi kuolewa na Jaji Mfalila.

Alidai mahakama ilikubali kimakosa madai hayo ya Lena na kumruhusu kusimamia mambo ya Jaji Mfalila (zikiwemo mali) akidai yeye alipaswa kupewa nafasi kueleza upande wake kwa kuwa ndiye mke halali wa Jaji Mfalila, lakini hakuhusishwa.

Rehema alidai kuwa kujumuishwa  katika shauri  hilo ni muhimu ili kulinda haki yake kama mke halali wa Jaji Mfalila, kwani kushindwa kufanya hivyo ni kusababisha ukiukwaji mkubwa wa haki.


Aliyoyasema Chellu,

mtoto wa Jaji Mfalila 


Chellu ambaye ni mjibu maombi wa kwanza katika shauri hilo la  Rehema kuomba kujumuishwa katika shauri la mapitio alilolifungua Chellu kupinga Lenna kuwa msimamizi wa mali za Jaji Mfalila, aliunga mkono maombi hayo ya Rehema.

Alieleza kuwa baba yao alifunga ndoa ya Kikristo na Rehema, katika Kanisa la Moravian, wilayani Sikonge, mkoani Tabora, Oktoba 20,1979, kufuatia kifo cha mama yao, Esther aliyekuwa mke wa kwanza wa Jaji Mfalila

Alimkana Lenna kuwa anajitambulisha isivyo ni mke wa Jaji Mfalila na amepata amri ya Mahakama ya kusimamia mali  za baba yao zikiwemo akaunti za benki, jambo ambalo lina madhara kwa mwombaji, Rehema na kwa Jaji Mfalila mwenyewe.

Lenna alivyochochea mgogoro

Kwa upande wake Lenna, alipinga maombi na madai ya Rehema akidai kwamba siyo mke wa Jaji Mfalila.

Alidai kuwa Rehema alitengana na Jaji Mfalila tangu mwanzoni mwa miaka ya 1980, kisha akaolewa na mwanamume mwingine aitwaye Mathew Kayenga ambaye alizaa naye watoto wawili Andrew Kayenga na Osimiel Kayenga.

Hivyo alidai kuwa Rehema hana madai yoyote dhidi ya  Jaji Mfalila wala masilahi katika shauri hilo, akisisitiza kuwa safari za nje ya nchi na Jaji Mfalila kwa ajili ya matibabu hazionyeshi uhusiano wa ndoa.

Badala yake alidai kuwa yeye (Lenna) aliishi na Jaji Mfalila kuanzia Septemba 17, 1983 hadi Desemba 2018.

Alidai kuwa  mwaka 2014 alipokuwa akimuuguza  Jaji  Mfalila katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, iliamuliwa kuwa mgonjwa anapaswa  kwenda India kwa matibabu, lakini mtoto wa kwanza wa Jaji Mfalila alifanya mipango akamruhusu Rehema kuambatana naye (mgonjwa India).

Aliendelea kuwa waliporejea yeye aliendelea kuishi na mgonjwa, Jaji Mfalila, huko Mbezi Beach (Dar es Salaam) mpaka mwaka 2018, Chellu alipomchukua baba yao akampeleka Kigamboni na baadaye Tabora, bila ridhaa yake (Lenna).

Akizungumzia maombi ya Rehema kujumuishwa katika shauri la mapitio lililofunguliwa na Chellu kumpinga yeye (Lenna), kusimamia mali za Jaji Mfalila, Lenna alidai kuwa Rehema anachanganya masuala yanayohusiana na usimamizi wa mali na migogoro ya ndoa.

Msimamo wa Jaji Mfalila

Jaji Mfalila ambaye ni mjibu maombi wa tatu katika shauri hilo la maombi ya Rehema, alibainisha mapema kutokuwa na nia ya kuwasilisha kiapo kinzani kupinga masuala ya kisheria.

Hivyo, hakushiriki kupinga suala lolote la kisheria lililoibuliwa katika kiapo cha Rehema.


Waliyoyasema mawakili

Wakili wa Rehema (hajatajwa jina) alidai kuwa wakati wa ndoa yao, Jaji Mfalila alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Lenna.

Alidai uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi kumruhusu Lenna kusimamia mali za Jaji Mfalila unakiuka masIlahi yake (Rehema) kama mke halali wa Jaji Mfalila.

Huku akirejea uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika mashauri mbalimbali alidai kuwa mwombaji (Rehema) kama upande wa tatu, na mwenye masilahi alipaswa kuunganishwa katika shauri la msingi (alilolizungumzia Lenna),

Hivyo, alidai kuwa ana haki ya kutafuta kulinda masilahi yake kwa kujumuishwa katika shauri la mapitio, kama sheria inavyoelekeza.

Wakili wa Lenna alipinga maombi ya Rehema akidai kuwa Sheria ya Ukomo inamzuia kujumuishwa katika shauri la mapitio (lililofunguliwa na Chellu), akidai kuwa alifungua maombi hayo nje ya muda, miezi 11 baada ya uamuzi unaopingwa badala ya siku 60.

Pia, alidai kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Akili ya mwaka 2008, masuala ya kupinga uamuzi wa usimamizi wa mali za mtu mwenye matatizo ya akili, mwombaji alipaswa kurudi katika mahakama ya awali kutumia nafuu zinazopatikana huko, kutenguliwa na kuondolewa katika usimamizi.

Vile vile alidai kuwa ili mtu aonekane kuwa upande muhimu katika shauri kwanza, lazima kuwe na nafuu zinazoombwa dhidi yake na mbili, aoneshe kuwa tunzo stahiki na haiwezi kutolewa bila yeye kujumuishwa.

Alidai kuwa Rehema alishindwa kufaulu vipimo hivyo na kwamba madai tu ya kuwa ni mke halali wa Jaji Mfalila hayawezi kufanya kustahili kujumuishwa kwenye shauri kama upande muhimu, bali alipaswa kuonesha masilahi ya moja kwa moja.

Wakili wa Rehema alidai kuwa katika hatua hiyo mwombaji hawajibiki kwa kanuni ya ukomo na kwamba asingeweza kurudi tena kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi wakati tayari kuna shauri la mapitio  linalohusu jambo lilelile.

Alisisitiza kuwa Rehema ni mke halali wa Jaji Mfalila, hivyo  ana masilahi yanayofungana na shauri hilo, na uamuzi wa shauri la Lenna kuwa msimamizi wa mali za Jaji Mfalila, unamuathiri, hivyo anastahili kujumuishwa katika shauri la mapitio la kumpinga Lenna.


Uamuzi

Jaji Mkwizu katika uamuzi huo amesema kuwa hoja hizo za pingamizi hazina mashiko, kwani hakuna sheria inayoelezea ukomo wa muda kwa upande muhimu kujumuishwa kwenye kesi au shauri au maombi.

Pia, amesema kuwa nafuu mbadala iliyopendekezwa na wakili wa Lenna, katika hali iliyopo isingekuwa sahihi.

Amesema malalamiko ya Rehema yamejikita katika hadhi yake kama mke halali wa Jaji Mfalila, ambaye kulingana na Rehema, mali zake zilikabidhiwa kimakosa kwa Lenna kwa mujibu wa uamuzi unaopingwa.

Amesema kuwa  hakuna pingamizi la msingi lililoibuliwa kuhusiana na uhalali wa ndoa baina ya mwombaji (Rehema) na mjibu maombi wa tatu  (Jaji Mfalila).

"Nimeshawishika kwamba kama mke halali wa Jaji Mfalila, ana masilahi katika shauri ambayo yanahitaji kuunganishwa kama mmoja wa wadaawa," amesema Jaji Mkwizu

Amesema kuwa mwombaji (Rehema) amethibitisha kwa kiasi cha kuridhisha masilahi halali katika mwenendo kuthibitisha maombi yake na kwamba amekidhi vigezo vya kisheria vya kuomba kuunganishwa katika shauri la mapitio.

"Maombi yanakubaliwa. Shauri la mapitio hilo linapaswa kurekebishwa kumuunganisha mwombaji, Rehema William Mbulumi Mfalila,  kama mjibu maombi wa nne.”

"Maombi yaliyofanyiwa marekebisho sharti  yawasilishwe ndani ya siku 14, kutoka tarehe ya amri hii,” alisema Jaji Mkwizu na kuhitimisha