Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mzazi fanya haya kumsaidia mwanao kuhimili hisia kali

Muktasari:

  • Wazazi wana nafasi muhimu katika kuwasaidia watoto wao kujifunza jinsi ya kudhibiti hisia kali na kuzielekeza katika njia sahihi ili wasiharibu maisha yao mbeleni.

Katika safari ya maisha, watoto hukumbana na changamoto mbalimbali zinazoweza kuwafanya wapitie hisia kali kama hasira, huzuni, hofu, au msongo wa mawazo.

Hisia hizi zisipodhibitiwa mapema, zinaweza kuwa na athari mbaya katika maendeleo yao ya baadaye.

Hivyo wazazi wana nafasi muhimu katika kuwasaidia watoto wao kujifunza jinsi ya kudhibiti hisia kali na kuzielekeza katika njia sahihi ili wasiharibu maisha yao mbeleni.

Kumsaidia mtoto kuhimili hisia kali ni mchakato unaohitaji uvumilivu, upendo na uelewa mkubwa kutoka kwa wazazi.

Kwa kutumia mbinu kama kuwasikiliza, kuwa kielelezo bora, kuwapa zana za kudhibiti hasira na hofu na kuwaimarisha kiakili na kihisia, wazazi wanaweza kuwajengea watoto wao uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha kwa njia chanya.

Na kwa kufanya hivyo, watoto wanakuwa watu wazima wanaojitegemea, wenye uwajibikaji wa kihisia na wenye uwezo wa kufanya uamuzi bora katika maisha yao ya baadaye.

Wataalamu wa masuala ya malezi wanasema wazazi wanaweza kuwasaidia watoto wao kwa kuwauliza maswali kama unajisikiaje au nini  kimekufanya uhisi hivyo!.

Wanasema njia hii huwasaidia watoto kuelewa hisia zao na kujifunza jinsi ya kuzidhibiti badala ya kuzirekebisha kupitia matendo yasiyofaa kama vurugu au kwa kujitenga.

Na tukumbuke kuwa watoto mara zote hujifunza kwa kuiga, hivi kama ndivyo, basi wazazi wanapaswa kuwa mfano mzuri kwa kuonyesha jinsi wanavyoshughulikia hisia zao wenyewe kwa njia chanya.

Mfano, badala ya kupandwa na hasira na kupiga kelele, mzazi anaweza kuonyesha njia za utulivu kama vile kupumua kwa kina au kuzungumza kwa upole.

Inaelezwa hivyo kwa sababu watoto wanahitaji mbinu halisi za kudhibiti hasira na hofu, kama vile kupumua kwa utulivu, kuhesabu hadi kumi kabla ya kujibu, au kuzungumza na mtu mzima anayeaminika.

Mbinu hizi zinawasaidia kupunguza athari za hisia kali na kuwawezesha kufanya uamuzi sahihi.

Na mazungumzo ya wazi kati ya mzazi na mtoto yanajenga uaminifu na kumfanya ajisikie salama kuelezea hisia zake.

Lakini pia badala ya mzazi kutafuta suluhu ya mar kwa mara, anapaswa kuwasaidia kufikiria njia mbadala za kutatua changamoto wanazokabiliana nazo.

Hili linajenga ujasiri na kuwasaidia watoto kuwa na mtazamo wa kutatua matatizo badala ya kukata tamaa au kukasirika na kuzira.

Mara zote mtoto anayejithamini, anao uwezekano mdogo wa kushindwa kudhibiti hisia zake kwa njia mbaya.

Lakini mzazi anapaswa kutambua kuwa mtio mar azote anahitaji kuelewa kuwa hisia zake ni halali, lakini si kila matendo ayafanyayo yanayochochewa na hisia hizo.

Hivyo kumfundisha nidhamu kwa upendo bila vitisho au adhabu kali pia itamsaidia kujifunza kuwa na uwajibikaji wa kihisia. Lakini tunaambiwa pia kumfundisha mtoto kujali na kushirikiana na wengine, nayo ni dawa ya kudhibiti hisia kali.

Kwa sababu kama mtoto anajifunza kuwa na huruma kwa wengine, siyo rahisi kujikuta kwenye lindi la hisia kali.

Ikiwa mzazi atagundua kuwa mtoto wake anashindwa kabisa kudhibiti hisia zake, anaweza kuwa muhimu kumtafutia msaada wa kitaalamu kama mshauri wa saikolojia.

Ushauri wa kitaalamu unaweza kumsaidia kupata mbinu bora zaidi za kushughulikia hisia zake.

Lakini kikubwa zaidi ni muhimu kwa watoto kujua kwamba wanaweza kuzungumza na wazazi wao bila kuhukumiwa.

Na mzazi kumsikiliza mwanawe kwa umakini na kuonyesha huruma, mara nyingi tunaelezwa kwamba humsaidia kudhibiti hisia kali inayolenga mabaya dhidi yake na jamii inayomzunguka.

Kwa maana nyingine, anapaswa pia kupongezwa pale anapofanya vizuri na si kusubiri kufokewa pale anapokuwa ametenda ndivyo sivyo.

Maneno ya faraja na uthibitisho wa mzazi yanaweza kuwa na athari kubwa katika kujenga ujasiri wa mtoto wake.

Hivyo kwa kutumia mbinu hizi, wazazi wanaweza kuwasaidia watoto wao kuhimili hisia kali na kuwatayarisha kwa maisha bora ya baadaye yenye utulivu, busara na hekima.