Makonda awaonya watakaovuruga mchakato ujenzi wa stendi, soko

Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema watakaovuruga mchakato wa kupata wakandarasi katika utekelezaji wa michakato hiyo atakula nao sahani moja kwani ujenzi wake umekuwa wimbo wa muda mrefu huku baadhi ya watu wakivuruga.
Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ameonya na kukemea chokochoko za atakayeingilia mchakato wa kumpata mkandarasi wa kujenga stendi mpya ya mabasi ya abiria na masoko mawili ya kisasa, atakula nao sahani moja.
Amesema ni mara 10 akawa mkuu wa mkoa kwa siku moja lakini kuna alama amaiweka na kuwa anataka stendi na masoko hayo yajengwe kwani kumekuwa na wimbo wa ujenzi wa stendi hiyo muda mrefu ila wanajitokeza watu wavurugaji.
Stendi ya Kisasa ya Jiji la Arusha inatarajiwa kujengwa katika eneo la Bondeni City huku masoko mawili ya kisasa ambayo ni Kilombero na Kwamrombo pamoja na uboreshaji wa bustani iliyopo Mto Themi, kupitia mradi wa Uboreshaji wa Miji Tanzania (TACTIC).
Makonda ameyasema hayo leo Ijumaa Machi 28, 2025 akizungumza katika uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia awamu ya pili iliyofanyika katika viwanja vya Ngarenaro jijini Arusha.
Amesema kila mara kumekuwa na wimbo wa stendi na masoko kujengwa ila hazikujengwa na kuwa kwa sasa kandarasi zimetangazwa za kujengwa stendi na masoko ya ujenzi huo.
“Kila siku wimbo wa stendi soko imekuwa kama chorus (kiitikio), inajengwa stendi inajengwa akiimba huyu mwingine anaitikia wakati mwingine hakuna hata vyombo vya kupigwa lakini kuna mtu anaanza pambio stendi inajengwa, hakuna stendi wala soko lililojengwa.
“Sasa ole wenu nisikie chokochoko tena za mtu anayeenda kuingilia mchakato wa kumpata mkandarasi wa kujenga soko, stendi huyo atakayeingilia nitakula naye sahani moja. Waziri, mimi ni afadhali nikawa RC kwa siku moja lakini nimeweka alama, tunataka stendi masoko yajengwe,” amesema
“Tukakimbizana tena Mwanasheria Mkuu tusaidie watu wana mkwamo, hivi tunavyoongea leo kwa taarifa tuliyonayo tenda ya kujenga masoko ya kisasa, stendi ya mkoa wa Arusha na pale Mto Themi, tunataka baada ya utaratibu huu hamtatudai stendi tunataka ijengwe angalau tufanane na majiji duniani.
Awali Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro, amesema wananchi zaidi ya milioni 43 kutoa mikoa 23, iliyopo kwenye halmashauri 154 wamefikiwa na kampeni ya sheria tangu ilipoanza.
Amesema kampeni hiyo imesikiliza kero za wananchi zaidi ya milioni 2 na kuwa wizara hiyo imeweka mikakati na mipango endelevu ikiwemo kuanzisha madawati ya msaada wa kisheria kwa kila halmashauri pamoja na kushirikisha na Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS).