Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makonda atinga na bodaboda, umati wampokea Dar

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Paul Makonda amewasili Ofisi ndogo ya makao makuu ya chama hicho yaliyopo Lumumba akiwa kwenye msafara wa bodaboda na kupokewa na umati wa wafuasi na viongozi wa chama na Serikali.

Makonda amewasili akiwa kwenye bodaboda kwa kile kilichodaiwa kuwa alishindwa kufika na gari lake kutokana na msongamano wa magari na umati wa watu uliojitokeza kwenye eneo la ofisi hiyo.

Makonda amewasili kwenye ofisi hizo saa 4:30 asubuhi na kuingia moja kwa moja kwenye ofisi za chama hicho kwenda kuwasalimia viongozi mbalimbali waliojitokeza kumlaki akiwemo Sophia Mjema aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo kwa kipindi cha miezi tisa.

Makonda aliyeteuliwa kwenye nafasi hiyo Oktoba 22 mwaka huu, baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa dakika 10 alitoka na kwenda kwenye ukumbi wa kukabidhiwa ofisi na mtangulizi wake kabla ya kuongea na vyombo vya habari.

Baada ya kuingia kwenye ukumbi huo, Mkuu wa Utawala wa chama hicho, Marko Mhanga alikuwa wa kwanza kuongea kwa kuwakaribisha viongozi na wanachama waliojitokeza kisha kutambulisha viongozi wa vitengo mbalimbali ndani ya chama hicho.

Baada ya kumaliza utambulisho huo, Marko alimkaribisha Sophia Mjema kuendelea na shughuli ya kumkabidhi ofisi Makonda aliyefanya kazi katika Serikali ya awamu ya tano huku mara ya mwisho akihudumu kwenye nafasi ya ukuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Katika tukio hilo, Sophia amesema kitengo hicho ni moyo unaotegemewa na chama hicho kuhakikisha katika chaguzi zinazokuja kinapata ushindi wa kishindo.

"Nimehudumu kwenye nafasi hii kwa kipindi cha miezi tisa nilikabidhiwa kijiti na Shaka Hamdu Shaka na juzi Oktoba 22 Chama kilifanya uteuzi na leo nakukabidhi wewe, tunaimani kubwa utatimiza azma ya chama chetu," amesema.

Amesema anafahamu kwa kuwa wote  kwa muda mrefu  walikuwa huko serikalini lakini amekuja kukitumikia chama ambacho shabaha yake ni kuendelea kushika dola.

"Una timu kubwa ya kushirikiana nayo, nawaomba watumishi ninaowaacha mpeni ushirikiano dhabiti katika muendelezo wa kukijenga chama chetu," amesema.

Makonda baada ya kukabidhiwa vitendea kazi alitumia dakika nne kuzungumza akianza kwa kumshukuru mtangulizi wake Sophia huku akieleza ni miongoni mwa viongozi waliomfundisha kazi akiwa mtumishi serikalini.

"Kwa bahati nzuri nimekuja kukitumikia chama na wewe unanikabidhi tena kijiti hiki asante sana, kikubwa nashukuru bado naendelea kwenye ulingo wa siasa kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kwenye nafasi nyingine," amesema.

"Sina maneno mengi nasema asante sana kwa kuwa mtumishi wa wengi, ni matumaini yangu mlango ambao Mungu ameufungua atanipa hekima, busara na uvumilivu na kukitumikia chama kwa uadilifu, uaminifu na mafanikio makubwa, ili nisimuabishe Mungu wala Rais aliyeniamini na kuniteua katika nafasi hii," amesema.

Ametumia fursa hiyo kuwaomba watumishi wenzake wa chama hicho kumpatia ushirikiano kumuelekeza na kumshauri.

"Duniani kote watu wanaishi kwa taarifa na taarifa zinafanya maamuzi ukiwa na chanzo kibovu utafanya maamuzi mabovu, lakini ukiwa na chanzo kizuri utafanya maamuzi sahihi wakati wote," amesema.

Amesema ni matumaini yake atapatiwa ushauri mzuri utakaosaidia ujenzi wa chama hicho ili kiendelee kupata mashiko kwa wananchi.


Makonda amkumbusha Sophia kutowasahau wajane

Amemtakia Sophia kila la kheri kwenye majukumu yake mapya, huku akimweleza kutokuwasahau wajane maana nao ni miongoni mwa kundi maalumu.

"Wewe mwenyewe umekuwa shahidi tumewapigania nilipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na sasa wewe umepata nafasi hiyo utakuwa kiungo muhimu na mimi nitakuwa na kukumbusha ujane kama sehemu ya kundi maalumu," amesema.

Baada ya mazungumzo hayo viongozi hao waliondoka kwenye ukumbi huo kuelekea kwenye ofisi za CCM, mkoa ambako sherehe za kumkaribisha kiongozi huyo zilikuwa zimeandaliwa.