Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makala aonya fitina na majungu CCM

Muktasari:

  • Chama cha Mapinduzi (CCM) kimewataka viongozi wake kufanya vikao kwa mujibu wa katiba  na sio vinavyolenga kushughulikiana.

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema chama hicho, siyo cha kushughulikiana bali ni chama tawala chenye demokrasia kwa wanachama wake.

Mbali na hilo, Makalla, amesema makundi yamekuwa yakigharimu chama hicho, akiwataka wanachama wake kuwa na umoja na kuacha fitina na majungu kwa ustawi na uhai wa chama hicho tawala.

Makala ameeleza hayo leo Jumamosi Julai 6, 2024 wakati wa kikao chake cha ndani na viongozi na wanachama wa CCM wa mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa ni maandalizi ya ziara yake ya kutembelea wilaya tano za mkoa huo itakayoanza kesho Jumapili Julai 7, 2024.

Katibu huyo wa uenezi, amewataka viongozi na wanachama kufanya vikao kwa mujibu wa katiba sio kwa lengo la kuwashughulikia watu fulani.

Amefafanua kuwa baadhi ya vikao vya CCM hasa katika ngazi mbalimbali vimekuwa vikiitishwa kwa lengo la kumshughulikia mtu fulani.

"Vikiitishwa vikao vya kawaida wajumbe hawahudhurii, lakini kukiwa na ajenda ya kumshughulikia mtu idadi inatimia," amesema Makala huku akiwahoji wanachama hapo vipi? akijibiwa hapo poa, akauliza tena imeenda hiyo? akajibiwa imeenda.

Makala aliyewahi kuwa mhazini wa CCM amefafanua kuwa siku ya vikao vya kuwashughulikia watu kunakuwa na vikao vingi vya awali na watu wajumbe wanajipanga ipasavyo.


Umoja ndani ya CCM

Makala amewataka Wana-CCM kuwa wamoja akisema chama hicho tawala hakiwezi kushinda chaguzi pasipokuwa na mshikamano. Amesema makundi hila na fitina ndizo zinazopunguza kura za CCM katika chaguzi.

"Mtu umeshachaguliwa kuwa diwani au mbunge kwa miaka mitano bado unasaka maadui zako wapi na wapi? Uchaguzi ukiisha vunja makundi fanya kazi na watu, sio kutafuta wabaya au kuendeleza visasi kwa waliokupinga.

"Lazima tuwe kitu kimoja kupiga vita makundi yanayokigharimu CCM, endeleza mshikamano ili tuwe chama kitakachoshinda chaguzi zijazo," amesema Makalla.


Kupanga safu

Suala la kupanga safu ya uongozi ni changamoto nyingine iliyotajwa na Makala kwamba inaigharimu CCM, akisema hivi sasa watu wapo ‘bize’ kupanga orodha ya madiwani na wabunge wanaowataka.

"Hii haikubaliki, ukianza kupanga safu unamkwamisha mwenyekiti wa mtaa au mbunge anayefanya kazi kwa tiketi ya CCM, kama hauwataki subiri muda wao uishe, lakini kwa sasa hawa ndiyo viongozi," amesema.

Kwa mujibu wa Makala, hivi sasa baadhi ya viongozi wa wilaya badala ya kufanya kazi za chama hicho, wamegeuka kufanya kazi alizoziita ‘mitano tena’

"Unaenda kwenye kata au majimbo unasikia mitano tena, ubunge mitano tena, unasema hii sasa hapana bali ni Rais Samia mitano tena...," amesema Makala ambaye ni mlezi wa CCM mkoa wa Dar es Salaam.


Uchaguzi wa serikali za mitaa

Akizungumzia mchakato huo, Makala amewataka viongozi wa CCM wa mkoa wa Dar es Salaam, kuhakikisha chama hicho kinaibuka kidedea katika uchaguzi huo utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.

"Tujitahidi tushinde ili mwakani tufikishe ujumbe kwamba tuna uwezo wa kushinda uchaguzi mkuu.Tushinde kwa kishindo mwaka huu. Tushirikiane tuchukue mitaa yote ya Dar ea Salaam," amesema Makalla.

Amewataka viongozi wa CCM mkoani Dar es Salaam, kuwateua wagombea wachapakazi, wanaokubalika watakaopeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi wa serikali za mitaa.


Kero za wananchi

Amesema CCM ndiyo kimbilio la wananchi wanaopeleka kero zao, akiwataka wananchi kutojitenga na matatizo yao bali wakae na kuyasikiliza ili kuyapatia ufumbuzi.

"Mkiwapa nafasi ya kuwasikiliza wataendelea kujenga  imani na CCM, sitarajii kusikia kiongozi wa chama akiwaambia wananchi nendeni Serikali (kufikisha kero zao). Hakuna uchaguzi Serikali iliwahi kupigiwa kura bali kinapigiwa chama.


Mtemvu nitajiuluzu uenyekiti

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu amesema viongozi wa maeneo mbalimbali wa mkoa huo, maeneo yao yatakayobainika kushindwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa wajiuzulu akisema hata yeye pia atajiuzulu.

"Mkimalizike kujiuzulu basi mimi nitafuata ili wachaguliwe viongozi wengine watakaofanya kazi ya kukijenga chama hiki huu ndio mwendo wa Dar es Salaam ya Mtemvu," amesema Mtemvu aliyewahi kuwa mbunge wa Temeke.