Majaliwa: Msiache kutumia dawa za Ukimwi

Muktasari:
- Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU), wameshauriwa kutoacha kutumia dawa za kufubaza virusi hivyo (ARV's) ghafla, hata kama watapimwa na wataalam wa afya na kuonekana kuwa hawana tena virusi hivyo ili kujiepusha na madhara yatakayowapata.
Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa watu wanaotumia dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV's), kutoacha kutumia dawa hizo ghafla hata kama watapimwa na kukutwa hawana tena virusi vya Ukimwi.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa wito huo leo Alhamisi Septemba 7, 2023, kwenye mkutano mkuu wa Baraza la Taifa la watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Tanzania (NACOPHA) uliofanyika Jijini Dodoma.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo kutokana na baadhi wa watu waliogundulika kuwa na VVU na baada ya matumizi ya muda mrefu ya dawa walionekana hawana maambukizi lakini walipoacha ghafla walipata madhara.
"Niwasihi hata kama ukipima mara mbili mara tatu ukigundulika kuwa hauna tena maambukizi usiache kutumia dawa ghafla, endelea kutumia mpaka wataalam watakapokwambia sasa acha kwani kuna walioacha ghafla wakapata madhara," amesema.
Aidha Majaliwa amesema Tanzania imepiga hatua kwenye mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi kwa kufika asilimia 96 ya watu wanaojijua kuwa na maambukizi ya VVU kutoka asilimia 61 iliyokuwepo mwaka 2016.
Amesema juhudi za kufikia asilimia hizo zimewafanya wadau wote wakiwemo sekta binafsi pamoja na serikali kutokana na elimu inayotolewa dhidi ya VVU na Ukimwi.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewataka watu wenye maambukizi ya VVU na Ukimwi kuendelea kutumia ARV's kwa kuwa zimethibitishwa na wataalamu duniani.
Ummy amesema serikali bado inaendelea kufanya utafiti wa dawa zingine ambazo hazina madhila makubwa kwa watumiaji ili ziingizwe nchini kwa matumizi lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU yanafikiwa.
Amesema imethibitishwa na wataalam wa afya kuwa dawa za kufubaza VVU zikitumika vizuri zina uwezo wa zuia maambukizi mapya kwa asilimia 70.
Kwa upande wake mwenyekiti wa NACOPHA Taifa, Leticia Morris ameitaka serikali kuongeza nguvu ya kuthibiti maambukizi mapya ya VVU hasa kwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 30 ambao ni asilimia 21 ya wanachama wao.
Amesema kwenye hiyo asilimia 21 ya vijana wenye VVU wanaume ni asilimia 36 na wanawake ni asilimia 63 hivyo ni lazima juhudi za makusudi zifanyike ili kuokoa nguvu kazi ya Taifa.