Majaliwa kuzindua mbio za Mwenge kesho

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadhi Haji akizungumza na waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro kuhusu tukio la kuwashwa Mwenge wa Uhuru hapo kesho. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Kwa mara ya kwanza Mwenge wa Uhuru uliwashwa mwaka 1961 na kupandishwa juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro na Luteni Kanali Alexander Nyirenda.
Moshi. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa kesho Jumanne Aprili 2, 2024 atakuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa utakaofanyika katika Chuo kikuu cha Ushirika (MoCU), Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Kwa mara ya kwanza Mwenge wa Uhuru uliwashwa mwaka 1961 na kupandishwa juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro na Luteni Kanali Alexander Nyirenda.
Siku hiyo, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alisisitiza umuhimu wa kuijenga Tanzania yenye umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi.
Akizungumza leo Jumatatu Aprili mosi, 2024 na waandishi wa habari mkoani hapa, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadhi Haji amesema jeshi hilo pamoja na vyombo vyote vya ulinzi na usalama vimejipanga kuhakikisha vinaimarisha ulinzi katika maeneo yote ya mkoa huo.
“Mgeni rasmi katika tukio hili ni Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ambaye ndiye anayetarajiwa kuwepo katika uzinduzi huo wa mbio za mwenge kitaifa, hivyo vyombo vyote vya ulinzi tumeshajiimarisha na kuhakikisha kwamba usalama unakuwepo katika maeneo yote ambayo tukio hili litafanyajika,” amesema Kamishna Haji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, baada ya kuzinduliwa tu, Mwenge utakimbizwa katika halmashauri saba za mkoa huo na utaweka mawe ya msingi 13, kuzindua miradi 14, kufungua miradi miwili na utatembelea miradi 18.
Babu amesema miradi yote itakayohusika itagharimu zaidi ya Sh28.6 bilioni hadi kukamilika kwake.