Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majaliwa aagiza washereheshaji warasimishwe

Muktasari:

  • Imeelezwa kuwa kurasimishwa kwa umoja wa washereheshaji na wapangaji matukio, utawasaidia kupata fursa mbalimbali za kiuchumi

Arusha.  Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amelitaka Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kukirasimisha rasmi, kukitambua na kusajili Chama cha Wafawidhi wa Matukio Tanzania (Washereshaji).

Waziri Mkuu amesema endapo kitarasimishwa na kusajiliwa, wataweza kufanya shughuli zao kwa kujiamini na kwa weledi zaidi.

Pia, ameitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Basata na Wizara ya Elimu, kuandaa miongozo, mafunzo na mfumo wa urasimishaji wa washereheshaji hao nchini ili kurahisisha utendaji kazi wao.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema hayo leo, Jumapili, Aprili 13, 2025, jijini Arusha alipofungua kongamano la Chama cha Wafawidhi wa Matukio Tanzania lililoambatana na uzinduzi wa nembo na beji maalumu ya chama hicho.

Amesema kurasimishwa kwa umoja huo kutawawezesha washereheshaji na wapangaji matukio kufanya kazi zao kwa uhalali na kupata fursa ya kutoa maoni ya kitaalamu juu ya namna bora ya kuiendeleza sekta hiyo ili itambulike na kukua katika ufanikishaji wa majukumu yao.

“Basata hakikisheni mnawapa wanachama hawa mwongozo wa namna bora ya kuanza kushirikiana na Serikali na namna ya kutekeleza kazi zao kwa kuzingatia itifaki, maadili na weledi wa hali ya juu,” amesema Majaliwa.

“Ili hili lifanikiwe, hakikisheni wanasajiliwa rasmi, wanatambuliwa na wanapewa vibali vya kazi ili wawe na uhakika na ujasiri wanapotekeleza majukumu yao, wasikutane na vikwazo visivyo vya lazima.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ameiagiza Ofisi ya Rais Tamisemi pia kuhakikisha washereheshaji waliotambuliwa na kurasimishwa wanapewa fursa ya kuendesha matukio yote kwenye ngazi ya halmashauri, wilaya na mikoa.

“Sio tena maofisa wa Serikali kila mara kukimbizana na maandalizi ya matukio, kushika nyundo na mbao kutengeneza majukwaa. Kuanzia sasa, wapeni kazi wataalamu hawa waliobobea ili waoneshe weledi wao, wajenge mahusiano mazuri na Serikali na waongeze tija kiuchumi kupitia sekta yao.”

Hata hivyo, Majaliwa ametoa angalizo kwa washereheshaji nchini kutumia vema mitandao ya kijamii kwa uangalifu na kuzingatia maadili ya Taifa, huku wakiepuka matumizi ya lugha na mitindo isiyofaa.

Mwenyekiti wa chama hicho, Ester Kimweri amesema chama chao chenye wanachama 450 kimeanzishwa kwa lengo la kuimarisha taaluma ya ushereheshaji katika shughuli mbalimbali zikiwamo za kijamii, kiutamaduni, hafla za Serikali, sekta binafsi, siasa na uratibu wa matukio yenye tija kwa Taifa.

Amesema licha ya mafanikio wanayoyapata, lakini wanakabiliwa na changamoto kubwa ya  ukosefu wa mwongozo rasmi wa kitaifa unaoitambua sekta hiyo kama taaluma rasmi, inayoweza kutoa ajira na kuchangia uchumi wan chi.

Hivyo, ameiomba Serikali iwafanyie mchakato wa kuwatambua rasmi na kuhakikisha vijana wanaoingia katika taaluma hiyo, wanapatiwa mafunzo na vyeti vya kitaaluma, badala ya mitazamo potofu kuwa kazi hiyo ni rahisi.

Mshereheshaji wa kitaifa, Odilo Kalinga amesemakurasimishwa kwa sekta hiyo kutasaidia kuleta heshima, kuongeza fursa za kazi na kuchangia uchumi kwa wanaoifanya taaluma hiyo.