Majaji watakaoamua hatima ya Katiba Mpya

Muktasari:
- Mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya ulitarajiwa kuhitimishwa kwa kura ya maoni kuikubali au kuikataa, Aprili 30, 2015, lakini hatua hiyo iliahirishwa Aprili 2, 2015 kwa muda usiojulikana. Miaka takriban 10 baadaye mwanasheria Barunguza amekwenda mahakamani kuomba amri ya Mahakama kuhitimisha mchakato huo.
Dar es Salaam. Hatima ya upatikanaji wa Katiba mpya sasa imewekwa mikononi mwa jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Adam Mambi. Majaji wengine katika jopo hilo ni Dk Zainabu Mango na Frank Mirindo.
Jopo hilo ndilo lililokabidhiwa na Jaji Kiongozi, Mustapher Siyani, dhima ya kuamua shauri la kikatiba linalolenga kufufua na kuhitimisha mchakato wa Katiba mpya.
Shauri hilo la maombi mchanganyiko limefunguliwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo, Tabora na mwanasheria, Alexander Barunguza dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), zamani Tume ya Taifa ya Uchaguzi – (Nec) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Katika shauri hilo, Barunguza pamoja na mambo mengine ameiomba Mahakama hiyo iamuru wadaiwa wafanye marekebisho ya Sheria ya Kura ya Maoni na pia iamuru upigaji wa kura ya maoni ufanyike wakati wowote kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Akizungumza na Mwananchi, leo Jumanne Aprili 15, 2025, Barunguza amesema jopo hilo lilipangwa na Jaji Siyani tangu Aprili 11, 2025 siku moja tu baada ya Jaji Mango, aliyekuwa amekabidhiwa kulisikiliza katika hatua ya awali kurejesha kwake jalada la shauri hilo.
Barunguza amesema jopo hilo ndilo litakalosikiliza shauri hilo lililopangwa kuanza mahakamani hapo Mei 15, 2025, kuanzia mwanzo mpaka kutoa uamuzi.
Mwanzo na mwisho wa
mchakato wa Katiba Mpya
Mchakato wa Katiba Mpya ulianza rasmi mwaka 2011 kwa utungwaji wa sheria za kuratibu na kusimamia utekelezaji wa upatikanaji Katiba mpya.
Hizi ni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyoelekeza kuundwa vyombo vya kuratibu mchakato wa katiba, yaani Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mabaraza ya Katiba na Bunge Maalum la Katiba (BMK), pamoja na Sheria ya Kura ya Maoni.
Sheria hizo ziliainisha namna ya ushiriki wa wananchi katika hatua zote za mchakato wa utungwaji Katiba Pendekezwa na utaratibu wa upigaji kura ya maoni ya Katiba Pendekezwa.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba iliratibu mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu ya Kwanza ya Katiba iliyohaririwa na Mabaraza ya Katiba na kupata Rasimu ya Pili ya Katiba.
Rasimu ya Pili ya Katiba iliwasilishwa kwenye BMK, ambalo licha ya mvutano wa kiitikadi wa wajumbe uliosababisha baadhi ya wajumbe wa kususia majadiliano na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), lilijadili na Oktoba 2, 2014 lilipitisha Katiba Pendekezwa.
Oktoba 8, 2014, aliyekuwa mwenyekiti wa BMK, Samwel Sitta aliikabidhi Katiba Pendekezwa kwa Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, ambayo ilizinduliwa rasmi siku hiyo kwa ajili ya kuendelea na hatua nyingine.
Mkwamo wa mchakato
Kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni, kama alivyoirejea Barunguza, ndani ya siku 14 baada ya kupokea Katiba Pendekezwa, Rais alipaswa kuchapisha katika Gazeti la Serikali, amri kuielekeza Nec kuanzisha mchakato wa kura ya maoni.
Mchakato huo ni pamoja na kuchapishwa kwa Katiba Pendekezwa, kuainisha muda wa kuanza kampeni za kura ya maoni, tarehe ya kupiga kura, kuandaa na kuchapisha wa swali la kura ya maoni ndani ya siku saba baada ya Katiba Pendekezwa kuchapishwa.
Mambo mengine ni ndani ya siku 14 baada ya kuchapishwa swali la kura ya maoni, kutoa taarifa kuainisha muda wa uhamasishaji na kutoa ufahamu kwa umma kuhusu kura ya maoni.
Mchakato wa kura ya maoni ulipangwa kuanza Kupitia GN
Kwa mamlaka aliyopewa na Sheria, Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, Oktoba 17, 2014 alitangaza kampeni za kura ya maoni zingeanza Machi 30 mpaka Aprili 29, 2015, na kupiga kura ya maoni ni Aprili 30, 2015.
Tarehe hiyohiyo, Nec ilichapisha swali la kura ya maoni lililouliza; “Unaikubali Katiba Inayopendekezwa?”
Hata hivyo, Aprili 2, 2015 Tume, ilitangaza kuahirisha kura ya maoni ya Katiba Pendekezwa kutoka Aprili 30, 2014 hadi itakapotangazwa tena. Mpaka leo haijatangazwa.
Sababu Barunguza
kwenda mahakamani
Hata hivyo, baada ya ukimya wa takriban miaka 10 baadaye, ndipo Barunguza amefungua shauri hili.
Barunguza amedai alishiriki kikamilifu katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba kuanzia ukusanyaji wa maoni mpaka utungwaji wa Katiba Pendekezwa.
Amedai kuwa Nec haikutekeleza wajibu wake wa kikatiba kutekeleza masharti ya Sheria ya Kura ya Maoni ndani ya muda uliolezwa kwa takriban miaka 10 sasa.
Hata hivyo amedai kuwa wadaiwa wamezuia utekelezaji wa mchakato huo bila kuueleza umma sababu au kwa sababu zisizo wazi na halali, bila kushauriana na kuhusisha ushiriki wa wananchi, wala bila kujali muda, fedha na rasilimali zilizotumika katika mchakato wote.
Amedai huo ni ukiukwaji wa Ibara ya 18(d) ya Katiba, inayotoa haki ya kupewa taarifa muda wote kuhusiana na matukio muhimu ya maisha na shughuli za watu na masuala yenye umuhimu kwa jamii.
Hivyo amedai kuwa kusitishwa mchakato huo kumemnyima fursa ya kikatiba kunufaika na haki zake za kikatiba kushiriki katika mambo ya nchi na haki yake ya kufahamishwa sababu za kusitishwa mchakato huo kwa zaidi ya miaka tisa sasa.
Pia amedai kuwa amenyimwa haki yake ya kuwa na nchi ya kidemokrasia inayozingatia utawala wa sheria na mgawanyo wa madaraka, kwa kuwa Katiba ya mwaka 1977 haikutokana na mchakato shirikishi.
Amedai kuwa si yeye tu aliyeathirika na mkwamo huo bali hata Watanzania walio wengi waliotoa maoni yao kwa upana yaliyowezesha kupatikana Katiba Pendekezwa.
Nafuu anazoziomba
Barunguza anaiomba Mahakama itamke kuwa Nec/Inec ilikuwa na wajibu kikatiba kutekeleza masharti ya Sheria ya Kura ya Maoni ndani ya muda ulioelezwa na kutokutekeleza masharti hayo, ilikiuka Katiba Ibara ya 26(1), inayotoa wajibu kila mtu kufuata na kutii Katiba na Sheria.
Pia anaiomba Mahakama hiyo itamke kuwa kusitishwa kwa mchakato huo ni kinyume na ibara ya 21(1) na (2) ya Katiba ya Nchi, kuhusu haki ya raia wote kushiriki katika masuala ya umma, na Mkataba wa Kimataifa kuhusu Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR).
Hivyo anaiomba Mahakama iwaamuru wadaiwa wafanye marekebisho yote muhimu ya Sheria ya Kura ya Maoni kuwezesha upigaji kura hiyo, muda wowote kabla ya Julai 30, 2025 au kabla ya kuanza kwa uchaguzi mkuu Oktoba 2025.