Maisha ya furaha ya Fadina yalivyogeuka kuwa majonzi

Fadina Namponda akila chakula
Mtwara. Julai 26, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, mama wa makamo aliangua kilio dakika chache baada ya hakimu kutoa hukumu ya kesi aliyofungua dhidi ya mumewe.
Fadina Mussa Namponda, mkazi wa Tandahimba alimshtaki mumewe, Shaibu Mtepa, aliyemkata viganja vya mikono yote miwili na kumkata kwa panga kichwani. Mahakama baada ya kumtia hatiani mshtakiwa, ilimhukumu kutumikia kifungo cha miaka 13 jela.
Uamuzi huo haukumridhisha Fadina, aliyeshindwa kuficha hisia zake, hivyo kuangua kilio akilalamika adhabu iliyotolewa ni ndogo ikilinganishwa na kosa lililofanyika na madhila anayopitia.

Timu ya waandishi wa Mwananchi ilifunga safari ya saa 12 kutoka Dar es Salaam hadi Mtaa wa Summit wilayani Tandahimba, nyumbani kwa Fadina kufanya mahojiano maalumu.
Akiwa amevaa juba anatupokea kwa bashasha na tabasamu tele akisema, “Karibuni, sikutarajia kama watu wangetoka Dar kuja kuniona mimi Fadina nisiye na chochote, kweli Mungu yupo. Karibuni Tandahimba mjisikie mko nyumbani.”
Nje ya banda analoishi lenye chumba na sebule, ukatandikwa mkeka, akatukaribisha. Akavua juba tukaanza mazungumzo yaliyotawaliwa na simanzi.
Wanaume watatu
Fadina, mama wa watoto watano analalama namna jitihada zake za kutafuta maisha zilivyokatishwa na mtu aliyeamini ni mwenza wa maisha yake baada ya ndoa mbili za awali kuvunjika.
Mtepa, mtalaka wake aliyemkata viganja walikutana na kuanzisha urafiki ulioishia katika ndoa, ikiwa ni miezi minne baada ya kutalikiana na mume wake wa pili, Rashid Mkavimila.
Ndoa ya kwanza alifunga na Mohamed Seif, baada ya kuhitimu elimu ya msingi. Alizaa naye watoto wawili kabla ya kutalikiana miaka saba baadaye.
Fadina akiwa mke wa pili kwa Mkavilima walibarikiwa kupata watoto watatu. Ndoa yao ilidumu kwa miaka 15 na kufikia ukomo Januari 2, mwaka 2014.
Mei 25, mwaka 2014 alifunga ndoa na Mtepa. Shughuli hii ilifanyika nyumbani kwa baba wa Fadina katika kitongoji cha Nachunu wilayani Tandahimba, ikihudhuriwa na ndugu wa pande zote mbili.
Baada ya ndoa anasema alianza maisha na Mtepa aliyekuwa na watoto watano, hivyo familia kuwa na jumla ya watoto 10. Familia hii ya watu 12 iliishi kwenye nyumba ya vyumba vitatu.

Pia ilimiliki shamba la mikorosho lisiloendelezwa na nje ya nyumba kulikuwa na matofali kwa ajili ya ujenzi.
Uhusiano na Mtepa
“Huyu mwanamume nilikutana naye nikiwa kwenye harakati za kufanya biashara ndogondogo. Akaniambia amenipenda na kuomba anioe, sikuona sababu ya kukataa ombi lile kwa sababu mimi si mtu wa kuhangaika, nikaona kama mwanamume anataka kunioa ni jambo jema.
“Kwa hiyo haikunichukua muda mrefu baada ya kumaliza eda kutokana na kuvunjika ndoa yangu, nikaingia kwenye hii nyingine na maisha yalikuwa mazuri. Upendo ulitawala kati yetu,” anasema Fadina. Anasema baada ya muda alibaini mumewe hakuwa mwajibikaji na aliacha kazi ya ulinzi, hivyo hakuwa na shughuli yoyote ya kumuingizia kipato.
Kutokana na hilo, anaeleza aliamua kujiongeza ili maisha yaende akizingatia kuwa ana watoto wa kuwahudumia. Akarejea kufanya biashara ndogondogo. “Wakati tuna mipango ya ndoa sikuwahi kugundua chochote kumuhusu. Nilipoolewa watani zake wakaanza kuniambia nimeolewa na mwanamume mvivu, hataki kulima wala kufanya shughuli yoyote na hata wanawake haishi nao. Nilisikiliza utani wao, nikiulinganisha na uhalisia wa maisha ndani ya nyumba yetu naona kabisa kuna uhusiano.
Alipataje mtaji?
Fadina anasema alikwenda kwenye shamba la mtalaka wake wa ndoa ya pili, Rashid Mkavimila pasipo ridhaa yake akachimba viazi na kwenda kuuza.
Siku ya kwanza ya biashara anasema alipata Sh9,000. Kwa mtaji huo, anaeleza alinunua viazi kwenye mashamba ya watu na kwenda kuuza Tandahimba mjini. Kwa kila tenga la viazi alilouza anasema alipata faida ya Sh10,000, fedha alizompatia Mtepa kuzitunza. Baada ya wiki mbili anasema walikusanya Sh140,000 walizotumia kununua dawa ya kupuliza kwenye mikorosho katika shamba la Mtepa la ekari tano aliloachiwa urithi na baba yake, lakini halikuwa na matunzo wala hakuliendeleza.
“Nilipoolewa tukaanza kuliendeleza. Nilikotoka pia nilipewa shamba ambalo msimu wa mwaka ule nilipata korosho za mwanzo kilo 120, nilipoziuza nikapata Sh120,000. Fedha hizi zote nikaziingiza kwenye mtaji wa maandazi ambayo tulibadilishana na korosho na nyingine alikusanya kutoka shambani kwake na kwenda kuuza. “Fedha zote za mauzo niliendelea kumkabidhi mume wangu, hilo halikuwa tatizo kwa sababu tulikuwa na maelewano mazuri. Hata alipoamua kurejea kwenye kazi yake ya ulinzi bado aliendelea kushika fedha zote,” anasema.
Anasema miezi minne baada ya Mtepa kurejea kazini, fedha za mshahara na walizokusanya kwenye biashara, mume wake alishauri wajenge nyumba nyingine mbali na wanafamilia wengine.
Fadina anaeleza alikubali na alishirikiana na mafundi katika ujenzi, ikiwa ni pamoja na kusomba matofali na kuchota maji. Nyumba hiyo ya vyumba vitatu na sebule ikasimama.
Anasema wakiendelea na kazi, nyumba ya awali waliyokuwa wakiishi ilitakiwa kubomolewa kupisha ujenzi wa barabara, hivyo wakalazimika kuiboma na kujenga mpya eneo lililosalia.
Fadina anasema walishirikiana kujenga nyumba hizo mbili, zilipokamilika alimsikia mume wake akizungumza maneno yaliyoashiria yeye ndiye amewezesha ujenzi.
“Kauli ile sikuipenda, nilipoisikia mara ya kwanza nilihisi amekosea. Siku nyingine nikamsikia anasema ulinzi ndiyo umemwezesha kujenga nyumba, hapo kengele ya hatari ikagonga kichwani. Nikamwambia kwa nini tusifunge mkanda tutafute maisha yetu ili tulivyonavyo tuwaachie watoto.
“Akakubali kwa shingo upande. Shamba langu mapato yote nikawa naelekeza kusomesha watoto, baiskeli nikampa kijana mmoja awe anaendesha na vitu vingine vidogovidogo nikawapa watoto,” anasema.
Mke mwenza
Fadina anaeleza, “Suala hili mwenzangu hakulipenda, nikaanza kusikia analalamika huko nje kwamba mwanamke huyu sasa amekuwa kila kitu anashirikisha watoto wake, hivyo wacha atafute mwingine anayeweza kufanya naye maisha. Niliposikia nikasema yote heri, wacha nisubiri anitamkie.”
Haikupita muda mrefu anasema Mtepa akachumbia kimyakimya. Ilipofika siku ya ndoa ndipo alipomtaarifu, naye aliridhia aoe mke mwingine kwa kuwa dini yao inaruhusu.
Baada ya mke wa pili kuolewa, anasema uhusiano kati yake na Mtepa ulizidi kudorora. “Ilipita miezi tisa mume wangu ameninyima unyumba, alipotea kabisa kwangu maisha yake yakawa kwa mke mdogo. Nilienda kwa viongozi wa dini akiwamo sheikh aliyetuozesha nikamueleza malalamiko yangu akaniambia kwa namna anavyomfahamu mume wangu hawezi kuingilia, tukalimalize suala hilo nyumbani.
“Mambo yalizidi kuwa magumu nikaomba talaka, ilipofika Novemba 9, mwaka 2018 nikapewa talaka ya mdomo. Sikuridhika, nilimfuata mwenyekiti wa Serikali ya mtaa aje kuwa shahidi na yeye akatimiza wajibu wake,” anaeleza.
Mgawo wa mali
Licha ya kupewa talaka, Fadina anasema aligoma kuondoka kwenye nyumba hadi atakapopewa mgawo wa mali walizochuma pamoja, akilenga nyumba walizojenga na shamba aliloshiriki kuliendeleza.
Anaeleza alikaa kwenye nyumba hiyo miezi miwili bila usumbufu kutoka kwa Mtepa hadi Januari 10, mwaka 2019 walipokaa kikao cha kutathmini mali zilizopo. Kikao hicho anasema kilihusisha mwenyekiti wa Serikali ya mtaa na wazee wa pande zote mbili.
Tathmini ilianza kwa vitu vya ndani ambavyo anasema waligawana pasipo changamoto yoyote. Shida anaeleza iliibuka walipofikia nyumba mbili walizojenga na shamba la mikorosho la Mtepa.
“Mwenzangu alikiri wazi kwamba nguvu yangu kubwa ilitumika kuendeleza shamba ambalo awali lilikuwa pori na pia katika ujenzi wa nyumba. Akasema yupo tayari kunipa Sh2 milioni. Nikamuuliza fedha hiyo anayo au ahadi, akanijibu ni ahadi.
“Nikasema kama ni ahadi basi aniongezee maana itanilazimu kuifuatilia, nikaomba aongeze Sh3 milioni ili jumla iwe Sh5 milioni, hapo nilikuwa tayari kumuachia kila kitu nikaanze maisha mapya,” anasema na kuongeza, ombi hilo alilikataa na akaanza kutoa lugha ya matusi.
“Mwenyekiti akasema hawezi kuendelea na kikao wakati kuna lugha zisizo za staha zinatolewa, akaondoka na kikao kikafungwa. Mwenyekiti akasema ambaye hajaridhishwa na uamuzi aende ofisini kwake. Nikamfuata akanipa barua ya kwenda kwa mtendaji,” anasema Fadina.
Mwenyekiti wa kitongoji
Akizungumzia hilo, Rashid Twalib, aliyekuwa mwenyekiti wa kitongoji cha Nasuvi walichoishi wanandoa hao, anakiri kushirikishwa kwenye uamuzi wa wawili hao kutengana na alishiriki kikao cha kwanza cha kugawana mali.
“Nilishiriki kuanzia kutengana, niliitwa kama shahidi na yule baba akaruhusu mkewe aendelee kukaa hapo kwa muda wakati suala la mgawanyo wa mali linawekwa vizuri. Niliitwa pia katika kikao cha kugawana mali, tulianza vizuri wakagawana vitu vya ndani bila matatizo yoyote. Shida ikaanza ilipofika kwenye nyumba, shamba na baiskeli.
“Mtepa alianza kuwa mgumu, halafu yanatolewa maneno yasiyofaa na wale ni watu wazima kwangu, nikaona jambo hilo limevuka juu ya uwezo wangu nikawaacha. Mama yule alikuja ofisini nikampa barua ya kwenda kwa mtendaji wa kijiji kwa ajili ya hatua zaidi,” anasema Twalib.
Fadina anasema baada ya kupokea barua aliipeleka kwa mtendaji wa kijiji, Lai Hemed aliyewaita kwenye kikao cha pamoja na Mtepa. Anasema safari hii hakukuwa na ndugu aliyeshiriki.
“Mtendaji alimuuliza mume wangu ana kiasi gani, akajibu yuko tayari kutoa Sh2 milioni. Akaniuliza nataka kiasi gani, nikamwambia Sh5 milioni. Mtendaji akasema haoni tatizo kuwa kubwa, suala hilo linaweza kumalizwa kwa kuzungumza na kufikia muafaka.
“Mwenzangu hakukubali, akahoji ni kitu gani kikubwa nilichofanya. Mtendaji akamueleza wazi kwa mfumo uliopo suala la mali zilizochumwa pamoja kugawana ni jambo la kawaida,” anasema.
Anaeleza Mtepa alishikilia msimamo, hawezi kutoa fedha hizo, akatoka ndani ya ofisi akimuacha mtendaji na yeye kabla hata mazungumzo hayajaisha.
Hemed akizungumza na Mwananchi anasema alishindwa kuwaweka sawa kutokana na Mtepa kutokuwa tayari kumpa Fadina kiasi hicho cha fedha. “Nilijaribu kadiri ya uwezo wangu kumshawishi ayamalize mambo kwa busara lakini ilishindikana, alisema yuko tayari kwenda popote kujibu kesi lakini hana fedha za kutoa,” anasema Hemed.
Kutokana na hilo, Hemed anasema alimuandikia Fadina barua aliyoipeleka Bakwata (Baraza Kuu la Waislamu Tanzania), ambao waliwaita.
Anasema Mtepa alipohojiwa iwapo atatoa Sh2 milioni ili viongozi wazungumze na Fadina kwa misingi ya imani, alijibu hayuko tayari na hana mpango wa kutoa hata Sh500,000.
Alisema yuko tayari kwenda mahali popote kujibu shtaka na baada ya kauli hiyo aliondoka kwenye kikao kabla ya kuahirishwa.
Kesi Mahakama ya Mwanzo
Anasema Bakwata ilimuandikia barua Fadina aliyoipeleka Mahakama ya Mwanzo ambako kila mmoja akatakiwa kupeleka mashahidi kuonyesha uhalali wa umiliki wa mali.
Kwa maelezo yake, kesi ilisikilizwa, ushahidi ukatolewa, uhakiki wa mali ukafanyika na hatimaye uamuzi ukatolewa. Mtepa akatakiwa kumpa Fadina baadhi ya vitu, ikiwamo nyumba yenye vyumba viwili.
“Tulikuwa na nyumba mbili, Mahakama ikaamua anipe ile ya vyumba viwili halafu yeye abaki na ya vyumba vinne, akatakiwa pia anipe baiskeli. Kulikuwa na masinki mawili ya choo yakagawanywa kwa kila mmoja wetu. Hakimu pia akaamua nipewe Sh5 milioni kutokana na ushiriki wangu kuendeleza shamba lake katika kipindi cha miaka minne na miezi saba nilichokuwa kwenye ndoa,” anasema.
Mtepa hakuridhishwa na uamuzi wa Mahakama akakata rufaa, shauri hilo likaenda Mahakama ya Wilaya Tandahimba, huko mambo yakawa mazuri upande wake. Hakimu aliamuru Fadina apewe theluthi moja ya thamani itakayotajwa katika mali zote. “Hakimu alisema mali hainitambui kinguvu wala ushiriki wangu katika kuipata ila inanigusa kwa mahusiano ya ndoa, sikuridhishwa na uamuzi ule nikamtafuta kijana mmoja mwanasheria nikamuelezea, naye akanipa mwongozo wa kukata rufaa. Nilifuata hatua hizo nikakata rufaa kesi ikapelekwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara,” anasema.
Anaeleza uamuzi wa jaji ulielekeza kutekelezwa uamuzi ule wa Mahakama ya Mwanzo ambayo pia ilipewa jukumu la kusimamia ugawaji mali. Mtepa hakukubaliana na uamuzi huo, kwa maelezo ya Fadina na kwamba, aliahidi angekata rufaa lakini hakufanya hivyo hadi Mahakama ya Mwanzo ilipoandika barua kwa mtendaji asimamie mgawanyo wa mali.
Jukumu hilo likarudi mikononi mwa Hemed, aliyewasiliana na Mtepa baada ya kupokea barua ya Mahakama, akimweleza amepewa muda maalumu wa kutoa ripoti ya utekelezaji wa maelekezo hayo.
Fadina akatwa viganja
Desemba 3, mwaka 2021, mtendaji wa kijiji cha Malopokelo alipanga kwenda kusimamia mgawanyo wa mali, jukumu lililopangwa kutekelezwa asubuhi.
Siku hii kamwe haiwezi kutoweka katika kumbukumbu za Fadina na familia yake. Anaeleza ndiyo aliyopata ulemavu wa kudumu baada ya kukatwa viganja, tukio lililobadili kabisa mwelekeo wa maisha yake.
Akiwa ameambatana na mjomba wake, Samuli Nanchochi, anasema alifika kwenye ofisi ya mtendaji wa kijiji cha Malopokelo saa nne asubuhi na kuungana na Mtepa ili kukamilisha mgawanyo wa mali.
“Kulingana na uamuzi wa Mahakama mama alipewa nyumba ya vyumba viwili. Tulikwenda hadi pale tukakuta imefungwa lakini mazingira yalionyesha kuna watu wanaishi. Nilimuuliza Mtepa akasema anaishi mtoto wake lakini ataondoka, basi nikamwambia ikifika Jumatatu awe ameondoka ili nimkabidhi mmiliki.
“Nikamuuliza kuhusu baiskeli na sinki, ambavyo anatakiwa kupewa Fadina, akanijibu vipo nyumbani kwake kitongoji cha Nasuvi. Tukaongozana kuelekea huko ili nimkabidhi mhusika,” anasema Hemed, mtendaji wa kijiji hicho.
Anasema safari ya kuelekea Nasuvi, umbali wa kilomita moja haikuwa na mazungumzo, ilitawaliwa na ukimya. Mtendaji anaeleza walipofika yeye, Fadina na mjomba wake walikaa juu ya matofali yaliyokuwa chini ya mkorosho jirani na nyumba.
Mtepa aliingia ndani wakiamini anakwenda kutoa baiskeli na sinki ili amkabidhi Fadina kama walivyokubaliana. “Aliingia ndani alikokaa kwa dakika kadhaa. Kilichonishangaza alitoka bila kitu chochote, nikamuuliza vitu viko wapi; akanijibu viko ndani tuingie. Nikamwambia hakuna sababu ya kuingia ndani kwa kuwa vinabebeka avitoe nje. “Yule bwana akaingia tena ndani na kutoka mikono mitupu, aliporejea alisogea tulipo na kuchomoa panga kwenye suruali. Lilikuwa tukio la ghafla, panga lilitua kichwani mwa Fadina, alipoweka mikono kukinga, likakata mkono wa kushoto,” anaeleza Hemed na kuongeza;
“Nikajaribu kumsaidia sikufanikiwa, Mtepa alikuwa akisema mtendaji nilisema nitafanya kitu kibaya na leo ndiyo siku yenyewe.”
Hayo yakiendelea, Nanchochi, mjomba wa Fadina alikimbia kuokoa maisha yake. “Nilitaharuki, uamuzi wangu wa haraka ulikuwa ni kukimbia maana tangu mgogoro unaanza hadi kesi mahakamani nilikuwa na Fadina na ndiye shahidi yake. Nikaona kama yeye amekatwa kwa panga anayefuata ni mimi. Nikiwa pale nilishuhudia panga likishuka mwilini mwa mwanangu mara tatu. Nikaamua kukimbia na kwa bahati mbaya nikajikwaa na kuanguka, hadi sasa mguu wangu una shida,” anasema Nanchonchi ambaye wakati wa tukio hilo alikuwa na miaka 71.
Hemed anaeleza, baada ya kuzidiwa nguvu na Mtepa alikimbia kuelekea ilipo barabara na kwa bahati akakutana na gari alilolisimamisha na kuomba msaada wa kumpeleka kituo cha polisi.
Haikuchukua muda mrefu mtendaji kufika kituo cha polisi cha wilaya alikotoa taarifa. Lilitolewa gari likiwa na askari kuelekea eneo la tukio.
Hemed anasema walimkuta Fadina akiwa ameanguka pembezoni mwa barabara jirani na nyumba ya Mtepa. “Wakati tukifika na gari la polisi, mtu wa kwanza kumuona ni Mtepa, aliyesimama katikati ya barabara akiwa amenyoosha mkono juu, kisha nikamuona Fadina ameanguka. Nikawaambia polisi mtuhumiwa ni yule pale, wakasimama na kumzingira, wakamkamata, kumfunga pingu na kumuingiza kwenye gari.
“Nikashuka kwenda kwa Fadina aliyekuwa amekatwa kwa panga, chini kulikuwa na dimbwi la damu, hakuna aliyefikiria kama anaweza kuwa hai. Nilimuinamia kusikiliza mapigo yake ya moyo nikamsikia akisema kwa sauti ya chini, nakufa kwa sababu ya kupambania jasho langu,” anasimulia Hemed.
Anasema polisi walimpeleka hospitali kiganja kimoja kikining’inia na kingine kikiwa kimeshikiliwa na mfupa ambao ulikatwa kwa panga.
Anasema katika Hospitali ya Wilaya ya Tandahimba, Fadina alipokewa na timu ya wataalamu waliomhudumia. Anasema aliongezwa chupa sita za damu.
Hemed anasema baadaye alikwenda kituo cha polisi kuandika maelezo kuhusu tukio hilo.
Anasimulia kuwa, kwa saa kadhaa Fadina alipoteza fahamu, akiwa na majeraha makubwa kichwani, usoni na mikononi. Alirejewa na fahamu siku iliyofuata.
Kwa mujibu wa Fadina, baada ya mtendaji na mjomba wake kuondoka eneo la tukio, Mtepa aliendelea kumshambulia hadi mke mdogo alipopiga kelele kumsihi asimuue mwanamke mwenzake.
“Yule mwanamke alipiga kelele kumwambia usimuue, Mtepa akaniacha na kumfuata mke mwenzangu kwenda kumnyamazisha, hapo nilipata upenyo wa kutoka na kukimbia kuelekea barabarani. Sikuwa na nguvu nikaanguka jirani na barabara, akanifuata na kuendelea kunikata,” anasimulia Fadina.
Nanchonchi anasema, “Nilishangaa mno. Tumekuwa naye karibu tangu amuoe Fadina alikuwa ni mtu mtaratibu anayeonekana kuwa mwenye upendo na hatujawahi kusikia ugomvi kati yao zaidi ya huu wa kutengana, na nikaitwa kuwa shahidi kwenye kugawana mali.
“Nashindwa kuelewa kitu gani kilimkuta baba yule hadi kufanya ukatili wa namna hii kwa mtoto wetu. Fadina kwetu alikuwa jembe, yeye ndiye mpambanaji. Mwepesi katika mambo ya famiIia. Inatuumiza mno kumuona katika hali hii anarudi kuwa tegemezi na afya yake inadhoofika.”
Swedi Mussa, mtoto wa kaka yake Mtepa anaeleza familia ilishtushwa na tukio hilo kwa kuwa baba yake mdogo alikuwa mtu mwenye busara na kiunganishi cha wanafamilia.
“Naweza kusema tumeumizwa kwa hili lililotokea kwa sababu, baba ndiye alikuwa kiongozi wa familia, hakuna aliyetarajia kwamba kuna siku angefanya jambo la aina hii, ikizingatiwa nje ya familia pia kwenye eneo alilokuwa akiishi aliaminika na kupewa uongozi. Alitarajiwa kuleta amani si hiki kilichofanyika.
“Siku ya tukio kila mtu alichanganyikiwa, hakuna aliyekuwa na majibu kwa nini amefanya hivi. Binafsi sidhani kama ni tukio la kawaida, hivyo tumelipokea kama lilivyo. Baada ya kesi hakuna kikao tulichokaa kwa ajili ya hatua nyingine. Tumepokea uamuzi wa Mahakama kwa adhabu ambayo amepewa na hadi sasa hatuna mpango wa kukata rufaa,” anasema Mussa.
Itaendelea kesho.
Imeandikwa kwa kushirikiana na Bill & Melinda Gates Foundation