Mahakama yatoa maelekezo kwa Serikali kesi bosi wa Jatu

Muktasari:
- Hii ni mara ya tatu kwa Gasaya anayekabiliwa na mashitaka mawili likiwemo la kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu, kumwandikia barua DPP ya kuomba kukiri mashitaka.
Dar es Salaam. Baada ya upelelezi kusuasua katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya (33) Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa maelekezo kwa Serikali.
Gusaya anakabiliwa na mashitaka mawili ambayo ni kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha kiasi hicho cha fedha.
Maelekezo hayo ni pamoja na kuhakikisha tarehe ijayo, Serikali inakuja na majibu na kueleza upelelezi umefika hatua gani.
Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Geofrey Mhini, ametoa maelekezo hayo, leo Jumatano Julai 9, 2025 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Mhini amefikia hatua hiyo, baada ya mshtakiwa kuwasilisha madai mahakamani hapo yakiwemo ya Serikali kushindwa kukamilisha upelelezi wa kesi yake kwa wakati, pia barua zake za kukiri na kuomba kufanya majadiliano na DPP ya kuimaliza kesi yake, hazijajibiwa.
Gasaya amedai kuwa kesi yake ndio iliyochukua muda mrefu kutokukamilika kwa upelelezi katika Gereza la Keko.
"Mheshimiwa hakimu, nasikitika sana kesi yangu imefikisha miaka mitatu hadi sasa bila upelelezi kukamilika na wakili wangu amefanya jitihada binafsi za kwenda Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) na akaambiwa upelelezi umekamilika, lakini hapa upande wa mashitaka wanatueleza bado upelelezi haujakamilika na hawajafanya juhudi zozote za kuhakikisha wanakamilisha mapema," amedai Gasaya na kuongeza:
"Na kesi yangu ndio iliyokaa muda mrefu katika Gereza la Keko, bila upelele kukamilika na hata walivyokuja gerezani (mawakili wa Serikali) waliniambia upelelezi umekamilika, sasa kwa nini hapa mahakamani upande wa mashitaka unadai upelelezi bado wakati kule Takukuru walieleza upelelezi umekamilika," amehoji.
Mshtakiwa huyo ameendelea kudai hata maombi yake ya kufanya majadiliano ya kuimaliza kesi ambayo ameshaandika barua tatu, hajajibiwa mpaka muda huu.
"Mheshimiwa hakimu, kwa hali hii naomba mahakama yako iingilie kati suala langu," ameomba Gasaya.
Akijibu hoja hizo wakili wa Serikali, Frank Rimoy amedai kuwa hawezi kujua mchakato wa upelelezi wa kesi hiyo umefikia hatua gani kwa sababu wakili anayesikiliza kesi hiyo yupo likizo.
"Kuhusu upelelezi umefikia hatua gani, siwezi kujua labda tarehe ijayo ndio tunaweza kuwa na majibu na kule Takukuru wanaweza kusema upelelezi umekamilika, lakini upande wa mashitaka wao ndio wenye mamlaka ya kutangaza kuwa upelelezi umekamilika na sisi hatuna nia mbaya na mshtakiwa, kama upelelezi umekamilika, tutaieleza Mahakama," amedai Wakili Rimoy.
Rimoy baada ya kutoa taarifa hiyo, ameomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Mhini baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, ameelekeza upande wa mashitaka tarehe ijayo waje na majibu juu ya upelelezi umefikia hatua gani.
"Nataka tarehe ijayo upande wa mashitaka mje na majibu mmefikia hatua gani katika upelelezi wa kesi hii ili Mahakama ijue na mshtakiwa ajue pia," amesema Hakimu Mhini na kuongeza.
"Pia tarehe hiyohiyo nataka niambiwe jalada lipo katika hatua gani? Bado lipo Takukuru linachuguzwa au lipo kwenu," amehoji Hakimu Mhini.
Baada ya kutoa maelekezo hayo, hakimu Mhini ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 23, 2025 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shitaka la kutakatisha fedha linalomkabili, halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, mshtakiwa anakabiliwa na mashitaka mawili ambayo ni kujipatia kiasi hicho cha fedha pamoja na kutakatisha Sh5.1 bilioni katika kesi ya uhujumu uchumi ya mwaka 2023.
Katika shitaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa, katika ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam, akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh5.1 bilioni kutoka Saccos ya Jatu.
Shitaka la pili ni kutakatisha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam.
Siku hiyo ya tukio na eneo hilo, mshtakiwa akiwa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa Jatu Saccos, alijihusisha na muamala wa Sh5.1 bilioni kutoka katika akaunti ya Jatu Saccos iliyopo benki ya MNB tawi la Temeke kwenda katika akaunti ya Jatu PLC iliyopo katika benki ya NMB tawi la Temeke, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.