Mahakama yapokea fomu sampuli DNA, kesi mauaji dada wa Bilionea Msuya

Muktasari:
- Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imepokea fomu ya vinasaba (DNA) kama kielelezo cha tano cha upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji ya Aneth Msuya.
Dar es Saalaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imepokea fomu ya vinasaba (DNA) kama kielelezo cha tano cha upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji ya Aneth Msuya.
Fomu hiyo ya ridhaa ya mshtakiwa wa pili Revocatus Muyella ambaye kakubali kuchukuliwa sampuli za DNA kwa ajili wa uchunguzi kuhusiana na vielelezo vilivyokutwa eneo la tukio.
Hatua hii inafuatia Mahakama hiyo kutupilia mbali pingamizi la mawakili wa utetezi, waliopinga kupokewa kwa fomu hiyo kuwa kilelelezo.
Pingamizi hilo lilitolewa na Wakili Peter Kibatala anayemtetea mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Miriam Mrita, mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Arusha, Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya.
Wakili Kibatala alipinga kupokewa kwa fomu hiyo pamoja na mambo mengine akidai kuwa haikidhi matakwa ya kisheria.
Hata hivyo katika uamuzi wake leo Juni 14, 2023, Jaji Edwin Kakolaki anayesikiliza kesi hiyo alikataa pingamizi hilo la upande wa utetezi akisema kuwa halina mashiko.
Jaji Kakolaki alisema kuwa Mahakama hii inaona kwamba utaratibu uliotumika kuchukua sampuli kwa mtuhumiwa haukumdhuru na upande wa utetezi haujasema kama ulikuwa na madhara yoyote.
Pia alisema kuwa mahakama inaona kwamba fomu hiyo haina tofauti sana na jinsi inavyoonekana katika jeswali la Sheria ya Vinasaba vya Binadamu na kwamba hata marekebisho yaliyodaiwa kufanya kwenye fomu hiyo hayana athiri.
"Hivyo Mahakama inaona kwamba hapakuwa na madhara kwa sababu hizo masharti yote matatu ya upokeaji kielelezo yamekidhi na Mahakama inaona mapingamizi ya upande wa utetezi hayana mashiko na inaelekeza kwamba kielelezo hi ho linapaswa kupokelewa.” alisema Jaji Kakolaki
Pamoja na mambo mengine katika pingamizi lake, wakili Kibatala alidai kuwa shahidi huyo hana mamlaka ya kutoa fomu hiyo ya ridhaa kwani Sheria ya DNA ya Binadamu inaelekeza kuwa mwenye mamlaka ya kutoa fomu hiyo ni afisa sampuli na si mamlaka ya kuomba kufanya vipimo hivyo, ambazo ni pamoja na askari Polisi.
Pia alidai kuwa hata kama wakiiona kuwa fomu hiyo ni halali kutolewa na shahidi huyo, lakini imefanyiwa marekebisho kwa kuongezewa taarifa nyingine ambazo hazimo katika fomu ya msingi na hawakusaini kuonesha kuthibitisha marekebisho hayo.