Prime
Mahakama yajiweka kando kesi Dk Malisa anayempinga Samia kuwa mgombea urais

Jaji kiongozi: Mahakama kuu kujipanga matumizi ya akili mnemba
Muktasari:
- Malisa yuko kwenye mchakato wa kufungua shauri la kupinga uteuzi wa Rais Samia kupeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu 2025 kwa nafasi ya urais. Hivyo aliomba asifukuzwe uanachama wa CCM hadi shauri hilo analokusudia kulifungua litakapoamuriwa.
Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Moshi imejiweka kando kusikiliza shauri la maombi ya kulinda uanachama wa kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Godfrey Malisa, anayepinga uteuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea pekee wa urais kwa tiketi ya chama hicho.
Badala yake Mahakama hiyo imemwelekeza Dk Malisa afungue shauri hilo Mahakama Kuu, Masjala ya Moshi.
Dk Malisa amelieleza Mwananchi uamuzi huo ulitolewa Aprili 24, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Proches Mushi aliyekuwa amepangwa kusikiliza shauri hilo.
Kwa mujibu wa Dk Malisa, shauri hilo halikupaswa kufunguliwa mahakamani hapo badala yake lilipaswa lifunguliwe Mahakama Kuu.
"Kwa kuwa Mahakama imeelekeza shauri hili lihamishiwe Mahakama Kuu ambayo ndio inaweza kuisikiliza," amesema Dk Malisa.
Amesema kutokana na uamuzi na maelekezo hayo ya Mahakama ya wilaya, sasa anatarajia kufungua rasmi shauri hilo Mahakama Kuu Moshi, kesho Jumatatu, Aprili 28, 2025.
Katika shauri hilo la maombi ya madai mchanganyiko Dk Malisa alikuwa akiiomba Mahakama hiyo itoe zuio la kufukuzwa uanachama mpaka shauri la kupinga uteuzi wa Rais Samia kuwa mgombea pekee wa chama hicho analokusudia kulifungua litakapoamuriwa.
Dk Malisa aliyejiunga na chama hicho mwaka 2020 alifungua shauri la maombi mahakamani hapo, dhidi ya Baraza la Wadhamini wa CCM na Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Kilimanjaro.
Mtia nia huyo wa urais na baadaye mgombea kiti cha Spika wa Bunge la Tanzania mwaka 2015, kupitia Chama Cha Kijamii (CCK), alifungua shauri hilo baada ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro kutangaza kumvua uanachama wa chama hicho.
Uamuzi wa CCM Kilimanjaro kumvua Dk Malisa uanachama wa chama hicho ulitangazwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Merce Mollel, kwa tuhuma za kukiuka katiba na maadili ya chama hicho.
Chama hicho kilichukua hatua baada ya Dk Malisa kutangaza hadharani msimamo wake wa kupinga uteuzi wa Rais Samia kuwa mgombea pekee wa urais mwaka 2025 kupitia CCM, huku alitangaza kwenda mahakamani kupinga mchakato na uamuzi huo.
Alinukuliwa na Mwananchi alikuwa hajapewa barua kumjulisha uamuzi huo, bali alisikia tu taarifa hizo kupitia vyombo vya habari, hivyo kutokanana taarifa hizo, ndipo akafungua shauri hilo la maombi ya zuio la kufukuzwa uanachama.
Katika shauri hilo, Dk Malisa aliomba ulinzi wa uanachama wake akidai kama atafukuzwa hatakuwa na haki ya kufungua shauri la kupinga uteuzi wa Rais Samia kuwa mgombea wa urais wa chama hicho, katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Shauri hilo liliambatana na kiapo cha Wakili wake, Emanuel Anthony, akiomba lisikilizwe kwa dharura kwa kuwa mteja wake anakusudia kuishitaki Bodi ya Wadhamini ya CCM na watu wengine kuhusiana na uamuzi huo.
Alidai yuko katika mchakato wa kufungua shauri hilo kwa utaratibu wa kumteua Rais Samia kama mgombea urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025 ulikiukwa na chama hicho.
Alijitambulisha kuwa yeye ni kada wa CCM tangu Novemba 2020 na ana kadi ya CCM iliyotolewa Novemba 20, 2020.
Alieleza Januari 19, 2025, CCM kilifanya mkutano na katika mkutano huo, Rais Samia aliteuliwa kupeperusha bendera ya CCM katika nafasi ya urais na kwa kuwa suala hilo halikuwa kwenye agenda, kada huyo hakuridhishwa na maamuzi hayo.
“Kutoridhishwa kwangu ni kwa sababu kulikiukwa taratibu. Kutokana na kukiukwa huko kwa taratibu nilikiomba chama changu (CCM) kupitia vyombo vya habari, kufuta maamuzi hayo na kurudi kufuata taratibu,” alieleza.
“Pia niliwajulisha viongozi wa chama changu juu ya nia yangu ya kwenda mahakamani ili uteuzi huo utenguliwe.”
Ameeleza wakati akisubiri majibu, alishtushwa na taarifa za kufukuzwa uanachama wa CCM, huku akidai kuwa binafsi hakuwahi kupewa huo uamuzi na kwamba hakuna mwenendo wowote kuhusiana na kupewa mashitaka na yeye kujitetea na hukumu.
“Kwa hiyo ninakusudia kufungua maombi kupinga utaratibu uliotumiwa na CCM baada ya kufuata taratibu zinazohitajika ikiwamo kumpelekea notisi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” ameeleza Dk Malisa katika maombi hayo.
“Hii itawezekana tu kama uanachama wangu utalindwa kwani bila hivyo sitoweza kudai haki yangu ya kisiasa na kiraia kupinga ukiukwaji huo wa taratibu. Kumshtaki Rais katika kesi ya madai kunahitaji nimtumie notisi,” amesema.
Dk Malisa ameeleza kuwa Februari 11, 2025, aliandika barua kwenda kwa Rais akimjulisha nia yake kukifungulia kesi ya madai chama chake na barua hiyo aliituma kwenda kwa Rais Machi 13 na kuambatanisha nakala ya barua hiyo.
“Nina ushahidi kuthibitisha kuwa Katiba ya CCM ilikiukwa," ameeleza katika maombi hayo huku akiambatanisha Katiba ya CCM ya mwaka 2022.
Siku mbili kabla ya shauri hili kuondolewa mahakamani hapo, Baraza la Wadhamini la Chama Cha Mapinduzi (CCM), liliwasilisha notisi ya kuwasilisha pingamizi la awali, kupinga shauri hilo.
Majibu ya CCM yaliandaliwa na kuwasilishwa mahakamani na idara ya Sheria ya Makao Makuu ya chama hicho Dodoma.
Notisi ya pingamizi hilo la awali, iliwasilishwa mahakamani hapo Aprili 22, 2025, ikiambatanishwa na kiapo kinzani cha mjumbe wa bodi ya wadhamini CCM, John Chiligati, akijibu kiapo cha hoja za Dk Malisa.
Katika notisi hiyo ya pingamizi hilo, bodi hiyo ya wadhamini kupitia kiapo hicho cha Chiligati, ilisema shauri hilo haliko sawa kwani linaungwa mkono na hati ya kiapo yenye kasoro.
Hivyo bodi ya wadhamini iliomba maombi hayo yatupiliwe mbali na muombaji aamriwe kulipa gharama za kesi.
Kwa mujibu wa kiapo hicho, mjibu maombi wa pili hana uwezo wa kisheria wa kushtaki au kushtakiwa na kwamba mzigo wake unabebwa na mjibu maombi wa kwanza ambaye ana uwezo wa kisheria kwa niaba ya mjibu maombi huyo.
Kuhusu kiapo cha Dk Malisa, Chiligati kupitia kiapo kinzani alisema wanapinga madai ya mwombaji Dk Malisa katika kiapo chake na kwamba atatakiwa kuthibitisha yale anayoyasema.
Hivyo aliiomba mahakama ilitupilie mbali shauri hilo.