Mahakama yaikataa ripoti ya video ya uhaini wa Lissu
Muktasari:
- Jamhuri kupitia shahidi wake wa tatu katika kesi ya uhaini inayomkabili Lissu iliiomba mahakama hiyo ipokee ripoti ya uchunguzi wa video inayomuonesha Lissu akitamka maneno hayo yanadaiwa kuwa ya uhaini, lakini mtuhumiwa huyo aliweka pingamizi ili mahakama isipokee ripoti hiyo, ambapo hoja yake imekubaliwa.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, imeikataa ripoti ya uchunguzi wa uhalisia wa picha mjongeo (video clip) ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini, yenye maudhui yanayodaiwa kuwa ya uhaini.
Upande wa mashtaka katika kesi hiyo jana Jumatano, Oktoba 22, 2025 kupitia shahidi wake wa tatu iliiomba mahakama iipokee ripoti hiyo kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.
Hata hivyo, Lissu aliweka pingamizi dhidi ya ripoti hiyo isipokewe akidai shahidi huyo hana mamlaka ya kisheria kuiwasilisha mahakamani wala kuiandaa ripoti hiyo kwa kuwa si mtaalamu wa uhalifu wa kimtandao.
Licha ya upande wa mashtaka kupinga hoja zake kuwa hazina mashiko kisheria, lakini Mahakama katika uamuzi wake leo Alhamisi Oktoba 23, 2025 imekubaliana na pingamizi lake baada ya kuridhia na hoja zake, hivyo ikaikataa ripoti hiyo ikieleza kuwa shahidi huyo hana mamlaka ya kisheria kuwasilisha ripoti hiyo kwa kuwa si mtaalamu wa masuala ya uhalifu mtandao.