Prime
Jamhuri ilivyomjibu Lissu pingamizi video ya hotuba yake
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu akiwa katika chumba cha Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.
Muktasari:
- Ijumaa iliyopita, Jamhuri kupitia shahidi wake wa tatu katika kesi ya uhaini inayomkabili Lissu iliiomba Mahakama ipokee video inayomuonesha Lissu akitamka maneno yanadaiwa ya uhaini lakini Lissu aliweka pingamizi na akatoa hoja zake
Dar es Salaam. Hatima ya kupokewa kwa picha mjongeo (video) inayomuonesha Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu kama kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya uhaini inayomkabili, itafahamika keshokutwa Jumatano, Oktoba 22, 2025, wakati Mahakama itakapotoa uamuzi wa pingamizi lililowasilishwa na upande wa utetezi.
Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa na Mahakama Kuu Masjala Ndogo, inayosikiliza kesi hiyo mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Mfawidhi, Dunstan Ndunguru akisaidiwa na majaji James KarayemahanaFerdinand Kiwonde.
Pingamizi hilo liliwasilishwa na mawakili wa Lissu wakipinga kupokewa kwa video hiyo kama kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.
Leo Jumatatu Oktoba 20, 2025 baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahakama imepanga kutoa uamuzi wake Jumatano.
Video hiyo inadaiwa kumwonesha Lissu akitoa hotuba yenye maneno yanayotafsiriwa kuwa ya uhaini, wakati wa mkutano wake na waliokuwa watia nia wa chama hicho waliotarajia kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Katika kesi namba 19 ya mwaka 2025, Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini akidaiwa kutoa maneno ya kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Anadaiwa kutamka maneno hayo Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania mwenye utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa kauli zinazodaiwa kuashiria nia ya kuitishia Serikali na baadaye kuchapisha maneno hayo kwenye mitandao ya kijamii.
Sehemu ya maneno hayo yanayonukuliwa katika hati ya mashtaka ni pamoja na, “wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli..., kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko..., kwa hiyo tunaenda kukinukisha..., sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli..., tunaenda kukinukisha vibaya sana...”
Kesi hiyo ipo katika hatua ya ushahidi wa upande wa mashtaka.
Shahidi wa tatu ni mkaguzi wa polisi, Samweli Kaaya (39), mtaalamu wa picha kutoka Kitengo cha Picha cha Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi ya Jinai (Forensic Bureau), Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam.
Katika ushahidi wake wa msingi, Kaaya alieleza kuwa, Aprili 8, 2025 alipokea flash disk na memory card zenye video ya Lissu yenye maudhui yanayodaiwa kuwa ya uhaini, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu, Dar es Salaam kuchunguza uhalisia wake.
Shahidi huyo, ameiomba Mahakama izipokee flash na kadi hiyo picha hizo (video) ziwe kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.
Hata hivyo, Lissu amepinga kupokewa kwa vihifadhi data hivyo vyenye video yake kuwa kielelezo akibainisha sababu nne
Lissu amezitolea ufafanuzi wa kina katika mizania ya kisheria na msimamo wa Mahakama ya Rufani katika uamuzi wa mashauri mbalimbali kuhusiana na hoja hizo.
Katika sababu ya kwanza Lissu, amedai kuwa upokewaji wa video hizo kuwa kielelezo umekiuka kifungu cha 263(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Marejeo ya Mwaka 2023.
Amedai kuwa hazikuwahi kuoneshwa kwenye Mahakama ya Ukabidhi (committal court), Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam Kisutu, kama Sheria hiyo inavyoelekeza.
Katika sababu ya pili amedai kuwa video hizo ziliwasilishwa kabla ya wakati zilipaswa zitanguliwe na taarifa ya uchunguzi wa uhalisia wake.
Sababu ya tatu amedai kuwa, shahidi huyo hana ustahili wa kisheria kuwasilisha video hivyo akidai kuwa si mtaalamu aliyeteuliwa na mamlaka husika.
Mwisho, amedai kuwa Jamhuri haikuweza kujenga mnyororo wa utunzaji wa vielelezo hivyo, tangu zilizopatikana mpaka zilipomfikia shahidi huyo na kuziwasilisha mahakamani.
Hata hivyo, Jamhuri katika majibu yake, imepinga hoja zote za Lissu ikidai kuwa, hazina mashiko ya kisheria na kuomba Mahakama izipuuze na izitupilie mbali pingamizi lake hilo.
Katika majibu hayo leo, Jamhuri nayo imefafanua kwa kina hoja moja baada ya nyingine katika mizania ya kisheria na msimamo wa Mahakama ya Rufani katika uamuzi wa mashauri mbalimbali kuhusiana na hoja hizo.
Usikilizwaji wa pingamizi hilo umehitimishwa kwa Lissu kujibu hoja za Jamhuri na baada ya kusikiliza hoja za pande zote.
Mahakama imesema itaamua iwapo video hiyo itapokewa au la kama sehemu ya vielelezo vya ushahidi baada ya kupitia hoja zote zilizowasilishwa.
Jaji Ndunguru ameahirisha kesi hiyo mpaka keshokutwa kwa ajili ya uamuzi.
Ni uamuzi huo utakaomaliza ubishi, upande mmoja utaibuka na ushindi baada ya Mahakama kushawishika na hoja zake kilingana na msimamo wa kisheria
Majibu ya Jamhuri
Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga katika hoja ya kwanza amedai kuwa video hizo zilioneshwa katika Mahakama ya Ukabidhi huku akiialika Mahakama kusoma ukrasa wa 92 na wa 93 wa kumbukumnu za Mahakama ya Ukabidhi.
Amedai kuwa, kumbukumbu za mwenendo kabidhi, zimeeleza wazi kuwa video zilichezwa kwa mshtakiwa na kwamba matakwa ya kifungu cha 263 yametekelezwa.
"Mwenendo anao na alikuwa na nafasi ya kusoma, lakini hakuna hata siku amewahi kuulalamikia kuwa una makossa," amesema Wakili Katuga.
Kuhusu hoja ya video hizo kuwasilishwa kabla ya ripoti ya uchunguzi wake, Wakili Katuga amedai hakuna sheria mahsusi inayoelekeza kuwa pale, shahidi mtaalamu anapofanya uchunguzi na kuandika ripoti, lazima kwanza awasilishe ripoti yake.
Amedai kuwa, ndio maana hata mshtakiwa hajaielekeza Mahakama katika kifungu chochote cha sheria kinachotoa sharti hilo na kwamba huo unakuwa ni mpango wa upande wa mashtaka tu.
Amerejea katika shauri moja la rufaa ya Jinai namba 413/20216 katika Mahakama ya Rufani, akisema mkemia alianza kuwasilisha mahakamani dawa alizozifanyia uchunguzi kabla ya ripoti yake.
Hoja ya tatu, ni kwamba shahidi hana mamlaka kuwasilisha vielelezo mahakamani.
"Tunasema shahidi wetu pamoja na vielelezo hivi anakidhi matakwa ya kanuni kwa kuwa kielelezo kinachotakiwa kutolewa na shahidi anayehusika anastahili," amesema Wakili Katuga.
Amesisitiza kuwa, anastahili kwa kuwa kwanza ameieleza Mahakama kuwa ndiye aliyefanyia kazi vielelezo hivyo, pili ameeleza utaalamu.
Akirejea uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika uamuzi wa mashauri mbalimbali amesema shahidi ana ufahamu wa kitu husika kama vile mmiliki, mtunzajii au aliyekifanyia kazi.
Amesema kuwa shahidi katika ushahidi wake alieleza kuwa, mtaalamu wa picha za mnato na jongefu ametangazwa katika Gazeti la Serikali (GN) namba 516 la mwaka 2022 na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Sylvester Mwakitalu, kuwa mchunguzi wa picha na kutoa taarifa.
Katika hoja ya nne ya kutokuwa na mnyororo wa utunzaji vielelezo, hasa kwa kutokuwepo nyaraka za makabidhiano, Wakili Katuga amedai kuwa mnyororo wa utunzwaji vielelezo hauthibitishwi na shahidi mmoja tu.
Pia, amedai hiyo si moja ya sifa tatu zilizoainishwa na Mahakama ya Rufani katika upokewaji wa vielelezo.
Katuga pia amesisitiza kuwa, suala la mnyororo wa utunzwaji kielelezo ni kwa ajili ya Mahakama kujiridhisha kuwa hazikuchezewa na ni halisi, akisisitiza hilo alithibitishwi na shahidi mmoja.
Hata hivyo, Lissu amesisitiza hoja zake akisema kuwa video hizo zilitajwa tu kwenye Mahakama ya Ukabidhi lakini hazikuwahi kuoneshwa na kwamba shahidi alipaswa kuwasilisha ripoti ya uchunguzi kabla ya video hizo.
Pia, Lissu amesisitiza kuwa shahidi huyo aliteuliwa kuwa mtaalamu wa picha za kawaida.