Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama ya Afrika yatupilia mbali hoja za Rwanda, mgogoro wake na DRC

Baadhi ya majaji wa mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu katika ya Rwanda na DRC leo

Muktasari:

  • Kesi hiyo yenye namba za usajili 007/2023 ilifunguliwa rasmi Octoba 2023 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiituhumu nchi ya Rwanda kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ndani ya ardhi ya Kongo, unaohusiana na mzozo wa kivita katika mikoa ya mashariki mwa nchi hiyo.

Arusha. Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) imetupilia mbali hoja za awali zilizowasilishwa na Rwanda katika kesi iliyofunguliwa mahakamani hapo na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kutokana na mzozo unaoendelea mashariki mwa DRC.

Katika uamuzi wake uliotolewa leo Alhamisi Juni 26, 2025, katika makao makuu ya Mahakama hiyo jijini Arusha, mbele ya jopo la majaji 11 likiongozwa na Rais wa Mahakama hiyo, Modibo Sacko kutoka Mali, imetangaza kuwa Mahakama ina mamlaka kamili ya kusikiliza kesi hiyo, kwa mujibu wa mikataba mbalimbali Afrika hasa zinazohusu haki za binadamu.

Mahakama, pia, iliagiza Jamhuri ya Rwanda kujibu hoja zote zilizowasilishwa na DRC ndani ya siku 90 kuanzia tarehe ya hukumu hii (kabla ya Septemba 24, 2025).


Msingi wa kesi

Kesi hiyo yenye namba za usajili 007/2023 ilifunguliwa rasmi Oktoba 2023 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiituhumu Rwanda kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ndani ya ardhi ya DRC, unaohusiana na mzozo wa kivita katika mikoa ya mashariki mwa nchi hiyo.

Tangu mwaka 2021, DRC imekuwa ikipambana na waasi wa kundi la M23, ambalo Serikali ya Kinshasa inadai linaungwa mkono na kufadhiliwa kijeshi na kifedha na nchi ya Rwanda.

Katika shauri hilo, Serikali ya DRC inadai Jeshi la Rwanda na washirika wake wamehusika na uhalifu mkubwa ikiwemo mauaji ya halaiki, unyanyasaji wa kingono, uhamishaji wa watu kwa nguvu, na uharibifu wa miundombinu ya msingi.

Aidha, kutokana na hayo, DRC inadai kuwa vitendo hivyo vinakiuka Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, hasa Ibara ya 1 inayozitaka nchi wanachama kutambua na kuheshimu haki za binadamu.

Nchi hiyo, pia, inakumbusha kuwa mgogoro wa sasa ni mwendelezo wa uvamizi iliyoanzia mwaka 1998 hadi 2002 na baadaye 2012 hadi 2013, ambapo majeshi ya Rwanda na makundi ya waasi walioungana nayo walihusika.

Hata hivyo, wanadai kuwa Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ilishawahi kuikuta Rwanda na hatia ya ukiukaji wa haki katika kipindi hicho cha nyuma na kupendekeza fidia.

Rwanda, iliyowakilishwa na timu ya wanasheria wanane wakiongozwa na Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu, Emmanuel Ugirashebuye ilipinga uwasilishaji wa kesi hiyo kwa hoja kuwa Mahakama ya Afrika haina uwezo wa kushughulikia migogoro ya kisiasa kama vita kati ya mataifa.

Pia, walidai kuwa kama kuna watu wameonewa, kukatiliwa au kunyanyaswa ingefaa wao ndio waje kushtaki na kuonyesha ushahidi wa jinsi wameonewa, kunyanyaswa au kuumizwa na siyo Serikali ya DRC kama walivyokuja.


Uamuzi ya mahakama

Hata hivyo, Mahakama ilikataa vikali hoja hizo na kuthibitisha kuwa ina mamlaka ya kushughulikia kesi hiyo na kwamba inakubalika kisheria.

Mahakama ilibainisha kuwa mfumo wa haki za binadamu wa Afrika unairuhusu Mahakama hiyo kusikiliza migogoro kati ya mataifa ikiwa inahusisha ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Kutokana na hayo, mahakama imeiamuru serikali ya Rwanda kujibu hoja zote zilizowasilishwa na Kongo kwa ushahidi au hoja za kisheria, kabla ya tarehe ya mwisho.

Awali, katika ombi lake, DRC iliitaka Mahakama kutangaza kwamba Rwanda imekiuka wajibu wake wa kimataifa chini ya Mkataba wa Afrika.

Pia, iamuru Rwanda kuondoa mara moja majeshi yake na kusitisha msaada wowote kwa waasi wa M23.

DRC inaitaka Mahakama kuilazimisha Rwanda kulipa fidia stahiki kwa madhara yaliyosababishwa kwa taifa la DRC na wananchi wake, pamoja na kuilipa DRC gharama zote za kesi.

Akizungumza nje ya Mahakama jijini Arusha, Waziri wa Sheria wa DRC, Samuel Mbemba, aliishukuru Mahakama hiyo kwa uamuzi wa awali wa kihistoria unaoleta matumaini kwa wananchi wote wa DRC.

“Tunaishukuru Mahakama kwa uamuzi huu wa kihistoria. Tunatumaini kuwa utaitekelezwa kikamilifu,” amesema Mbemba na kuongeza:

“Mpaka sasa, maelfu ya watu wetu wamekufa, wanawake wengi wametendewa unyama na kubakwa, watoto wanateseka kila siku bila chakula, elimu wala makazi, yote haya ni matokeo ya vitendo vya kibinadamu vilivyopuuza haki zao za msingi.

“Uamuzi wa leo ni ishara ya matumaini kuelekea amani na utulivu, siyo tu kwa Kongo, bali kwa ukanda mzima. Wananchi wetu wana matumaini.”