Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mafuriko yasomba reli, abiria watumia mabasi

Muktasari:

Abiria hao walikwama jana katika eneo hilo wakitokea katika mikoa ya Kigoma, Mwanza na Tabora wakielekea Dar es Salaam na Morogoro.

Dodoma. Abiria 1,090 wa treni waliokuwa wakienda Dar es Salaam, wamekwama katika stesheni ya Mzaganza iliyopo Dodoma, baada ya sehemu ya reli kusombwa na mafuriko.

Abiria hao walikwama jana katika eneo hilo wakitokea katika mikoa ya Kigoma, Mwanza na Tabora wakielekea Dar es Salaam na Morogoro.

Tukio hilo liliulazimu uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kukodi mabasi 17 ili kuwapeleka abiria hao katika mikoa hiyo.

Mkuu wa Usafirishaji wa Abiria na Mizigo wa TRL Dodoma, Haruna Mwano alisema TRL imefanya utaratibu ili abiria hao waweze kuendelea na safari zao.

Alisema kuwa, abiria hao walianza safari jana jioni na wamerudishiwa fedha ya chakula ili waweze kujikimu wawapo njiani kwenda waendako.

Mkuu huyo wa usafirishaji alisema kuwa, TRL walitumia mabasi 17 kuwasafirisha abiria hao na bado hajajua huduma za treni zitarejea lini katika hali yake ya kawaida.

Wakati huohuo, uongozi wa kampuni hiyo umetangaza kusitisha huduma za usafiri kwa muda kuanzia juzi baada ya eneo la reli kati ya Kilosa mkoani Morogoro na Gulwe mkoani Dodoma kukumbwa na mafuriko.

Taarifa iliyotolewa jana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Elias Mshana ilisema taarifa za kifundi katika eneo lililoathiriwa na mafuriko ni kubwa, hivyo wahandisi na mafundi wa TRL wapo eneo la hilo kutathmini ukubwa wake.

Kwa mujibu wa Mshana haijulikani rasmi ni lini huduma za usafiri wa treni zitarejea na abiria husika wametakiwa kufika katika vituo vya reli walikokata tiketi ili warejeshewe fedha zao.

Uongozi wa kampuni hiyo ulisema kuwa utatoa taarifa kamili kuhusu lini huduma za TRL kwenda Bara zitaanza tena.