Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mafuriko ilivyokata mawasiliano Mwanza, Tanroads yaomba radhi

Wakazi wa Mwanza wakipita kwenye ukingo wa Daraja la Mkuyuni baada ya kina cha maji kupungua kufuatia kufurika maji usiku wa kuamkia leo Jumanne Aprili 8, 2025 na kukata mawasiliano. Picha na Mgongo Kaitira.

Muktasari:

  • Miongoni mwa waliokumbana na kadhia ya mvua iliyoanza kunyesha maeneo mbalimbali jijini Mwanza kuanzia saa 9:30 usiku wa kuamkia leo hadi saa 11:30 alfajiri leo Aprili 8, 2025, ni wenye vyombo vya moto, wafanyabiashara na wanafunzi

Mwanza. “Ni kilio.” Ndivyo unavyoweza kusema baada ya wakazi wa Jiji la Mwanza kukwama kufika katikati ya jiji hilo kwa wakati asubuhi ya leo Jumanne, Aprili 8, 2025 kutokana na mafuriko ya mvua kuvunja Daraja la Mkuyuni jijini humo.

Miongoni mwa waliokumbana na kadhia ya mvua hiyo iliyoanza kunyesha maeneo mbalimbali jijini Mwanza kuanzia saa 9:30 usiku wa kuamkia leo hadi saa 11:30 alfajiri leo Aprili 8, 2025, ni wenye vyombo vya moto, wafanyabiashara na wanafunzi waliokuwa wakienda shuleni.

Wakazi wa Mwanza wakiwa pembezoni mwa Daraja la Mkuyuni jijini Mwanza lililojaa maji kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha jijini humo. Picha na Mgongo Kaitira

Maji hayo yamepita juu ya Daraja la Mkuyuni na kuvunja mawasiliano kati ya wananchi waliokuwa wakienda na kutoka Nyegezi kuelekea katikati ya jiji.


Wananchi walia

Akizungumzia kadhia hiyo, Mkazi wa Mkuyuni, Charles Lulinga amesema mafuriko hayo yamesababishwa na ufinyu wa mitaro na daraja lililopo eneo hilo ambalo upanuzi wake umeanza Januari mwaka huu huku akieleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wake.

Lulinga amesema kwa kipindi kirefu ameshuhudia magari ya mkandarasi katika eneo hilo bila kuona maendeleo yoyote ya ujenzi wa mradi huo jambo ambalo amedai siyo tu ni kero kwa wananchi wanaoteseka mvua inaponya, pia inapunguza imani ya wananchi kwa Serikali.

“Ni kweli mkandarasi tunamuona hapa anajenga lakini hatuoni mabadiliko yoyote hadi muda huu mvua zimeanza kunyesha tena. Hatujui kama yupo ama ameshaondoka, Serikali iingilie kati hili suala hili daraja limeshatuchosha,” amesema Lulinga.

Mwendesha pikipiki maarufu kama bodaboda akipita juu ya daraja lililofurika la maji la Mkuyuni jijini Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira



Kauli ya Lulinga inaungwa na mkono na mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Amani, Kata ya Mkuyuni jijini humo, Leokadia Hwago amesema daraja hilo limeanza kukarabatiwa miezi zaidi ya kadhaa iliyopita huku akisema halionyeshi dalili ya kukamilika.

“Wananchi tunawakera, wanalipa kodi na hii miundombinu ya hapa ni mibovu. Na kama mkandarasi anadai pesa zake alipwe kama amelipwa basi afanye kazi yake kwa wakati ili wafike kwa wakati kwenye shughuli za ujenzi wa taifa,” amesema Hwago.


Wanafunzi wakosa mitihani

Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Pamba jijini Mwanza, Victoria Fredrick amesema kutokana na daraja hilo kufurika kumesababisha achelewe kwenye mitihani ya kujipima shuleni.

“Imeniathiri kwa sababu hatujaenda shule hadi muda huu (saa 3:20) asubuhi na tulikuwa na mitihani kwa hiyo tunaomba Rais wetu (Samia Suluhu Hassan) atusaidie waliinue ili tusiwe tunapata changamoto kuvuka kila mvua inaponyesha,” amesema Victoria.

Victoria amesema pamoja na kuwepo vijana wanaohatarisha maisha yao na kuvusha watu kwa kuwabeba mgongoni kwa Sh500, wanafunzi waliokwama eneo hilo hawawezi kumudu gharama hiyo kutokana na kupatiwa fedha ya nauli ya kwenda na kutoka shuleni pekee.

Mwanafunzi wa kidato cha nne Sekondari ya Nyaburogoya jijini humo, Irene Paulo amesema changamoto ilianzia eneo la Mabatini baada ya kukutana na foleni ya magari iliyosababishwa na mafuriko huku akisema hofu yake ni kufokewa atakapofika shuleni kwa kuchelewa.

“Kutokana na mvua ya leo kuna vipindi nitachelewa. Hii changamoto imekuwa ikitukumba kila mara mvua inaponyesha tukifika hapa huwa daraja linafurika,” amesema Irene.


Kauli ya Polisi

Maofisa wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza wamelazimika kufika eneo hilo kuanzia saa 11 alfajiri baada ya kuwepo msongamano wa magari huku baadhi ya watu wakilazimisha kuvuka kwa kukatiza kwenye mafuriko hayo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema jeshi hilo lilifanikiwa kuwadhibiti watu waliokuwa wakilazimisha kuvuka juu ya daraja hilo likiwa limefurika jambo linalohatarisha maisha yao.

Pia, amewataka wenye magari kutumia barabara mbadala kufika mjini hususan Barabara ya Sahwa na Usagara kupitia Kisesa hadi katikati ya jiji hilo ili kuepuka kupoteza muda kwenye foleni iliyosababishwa na mafuriko hayo.

“Tuko hapa tangu saa 11 alfajiri baada ya mvua kupungua na tulipopewa taarifa kuwa kuna foleni hapa. Bado polisi hatujapata taarifa ya maafa yoyote kwa raia ama mali ila tunachohimiza ni kwamba wananchi wasilazimishe kuvuka wanapoona maji yamekata barabara,” amesema kamanda Mutafungwa.


Tanroads, Mkandarasi

Akizungumzia changamoto hiyo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mwanza, Pascal Ambrose amethibitisha daraja hilo kufurika kutokana na mafuriko hayo huku akiomba radhi kwa wananchi kutokana na changamoto hiyo.

“Wenzetu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) katika kujenga mradi wao wa SGR walijenga tuta kubwa kwa hiyo linafanya maji na kuyapitisha sehemu moja. Kwa hiyo yale maji yote yanalazimika kupitishwa katika daraja hilo la Mkuyuni ambalo uwezo wake ni mdogo kwenda Ziwa Victoria,” amesema Ambrose.

Ambrose amesema Serikali kwa kutambua changamoto hiyo imeanza utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa daraja hilo ulioanza Desemba 2024, kwa gharama ya Sh5.5 bilioni huku likitarajiwa kukamilika Novemba 2025.

“Huo mradi unahusisha upanuzi wa daraja na ujenzi wa barabara kwa urefu wa mita 500 kila upande. Kwenye ujenzi lazima kuna adha zinajitokeza tunawaomba samahani, lakini hapo tutakapokuwa tumekamilisha ujenzi wa hilo daraja tutasahau yote haya,” amesema Ambrose.

Akizungumzia kusuasua kwa mradi huo, Mwakilishi wa Kampuni ya Jasco inayotekeleza ujenzi huo, Nestory James amesema ujenzi wake umesuasua kutokana na mchoro wa awali kuonekana kutofaa, hivyo wamelazimika kuboresha mchoro huo.

“Awali, usanifu ulionekana kuwa lijengwe daraja la kawaida lakini kutokana na changamoto ya maji kuwa kubwa tumelazimika kuchora mchoro mwingine na tayari umekamilika wiki hii ujenzi utaendelea,” amesema James.

Amesema mradi huo utakapokamilika utawezesha kingo za mto na daraja hilo kuinuliwa jambo litakaloondoa kabisa changamoto ya mafuriko eneo hilo na kutoa fursa kwa wananchi kupita bila kikwazo chochote wakati wa masika.