Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maeneo salama ya kutembelea leo Krismasi

Dar es Salaam. Wakati maelfu ya Wakristo nchini na Watanzania kwa ujumla wanasherehekea Sikukuu ya Krismasi leo, familia nyingi zimekuwa na utamaduni wa kutumia siku hiyo kwenda sehemu za starehe kwa ajili ya mapumziko na kujiburudisha.

Licha ya baba, mama na watoto wao huenda maeneo hayo, pia vijana wasio na familia nao hawako nyuma, hutumia siku hiyo kwenda sehemu za starehe na kujumuika na marafiki zao.

Kwa kawaida maeneo hayo siku kama ya leo hukutanisha watu wengi, hivyo kunakuwapo na changamoto za watoto kupotea, matukio ya uhalifu au ajali zinazosababisha majeruhi na hata vifo.

Kutokana na hali hiyo, Mwananchi linakubainishia maeneo unayoweza kwenda na familia na kurudi nyumbani salama.

Kwanza, unapochagua eneo la kwenda kuburudika, jiridhishe kwamba lina usalama wa kutosha kwa maana ya ulinzi na pia vifaa vitakavyotumiwa na watoto viwe na usalama, mfano, mabwawa ya kuogelea ni muhimu yawe na waokoaji muda wote.

Vilevile, hakikisha eneo hilo halina msongamano wa watu wengi, ili hata inapotokea changamoto iwe rahisi kujiokoa na kutoa msaada wa haraka kwa familia yako.
Mkazi wa Mburahati, Maria Huruma anasema anapendelea sehemu yenye muziki wa bendi kwa sababu sikukuu watu hujaa kwenye baa na usalama unakuwa mdogo.

“Napenda bendi, hivyo sikukuu nitakwenda eneo hilo, kwani watu wanajaa kwenye baa, wenyewe tunaita fungulia mbwa hata wasiokwenda baa huwa wanaruhusiwa hiyo siku,” anasema Maria.
 

Maadili kwa watoto

Wazazi wazingatie wanawapeleka watoto maeneo yanayozingatia maadili, ili wasikutane na mambo yatakayoathiri makuzi yao kwa kutazama au kusikia mambo yasiyofaa.

Akizungumzia hilo, Stanslaus Kadanye mkazi wa Kinyerezi, jijini Dar es Salaama anashauri wazazi wawaepushe watoto na muziki wenye lugha isiyo na staha, wanaocheza nusu uchi au picha chafu za video zinazoonyeshwa kwenye baadhi ya kumbi za starehe.

Anasema yeye binafsi hutumia siku kama ya leo, mchana kufurahi na watoto akiwa eneo analoona linafaa kukaa na familia.

Anasema jioni huwarudisha watoto nyumbani, naye hutoka na mkewe kwenda kwenye hoteli zenye baa kwa sababu zina usalama.
 

Maduka makubwa

Siku ya sikukuu hekaheka pia huwepo maeneo yenye maduka makubwa, sehemu hizo hupendwa sana na watoto kutokana na bidhaa zinazouzwa. Pia kutokana na punguzo la bei linalotolewa siku kama ya leo.

Pia wazazi na walezi hupenda kutembelea maeneo hayo, licha ya kuwa na msongamano mkubwa, lakini yana nafasi kubwa ya watu kukaa kwa usalama.
Lakini pia inaelezwa kuna ulinzi wa kutosha, cha msingi ni kwa mzazi kuhakikisha anawaangalia watoto wake wakati wote, kwani pia kunakuwapo na michezo mbalimbali ya watoto.

Neema Mbarawa, anasema kwa kufanya hivyo kunasaidia watoto na wazazi wao kusherehekea sikukuu kwa amani na furaha na kisha kurejea nyumbani wakiwa salama.
 

Sababu familia kupenda kuyatembelea

Sophia Zephania, mkazi wa Mbezi anasema hupendelea kwenda kwenye maduka hayo kwa sababu kunakuwa na punguzo la bei, hivyo sikukuu kwake ni kwa ajili ya kufanya manunuzi.

“Mimi na marafiki zangu huwa tunakwenda kwenye Mall kununua nguo na pochi kwa sababu asilimia kubwa huwa wanashusha bei,” anasema.
Dk James Lwanga, mkazi wa Mikocheni anasema huwa anawapeleka watoto wake kwenye michezo iliyopo maeneo ya Mall ili kuwakutanisha na watoto wengine.

“Muda mrefu wanakuwa shule na siku za kawaida hatupati nafasi ya kuwapeleka kutembelea sehemu hizo kutokana na majukumu tuliyonayo, hivyo ikifika sikukuu nawapeleka sehemu za kubembea na kuendesha magari,” anasema.
 

Fukwe za bahari

Fukwe za bahari ni sehemu nzuri kwa ajili ya matembezi ya sikukuu kwa sababu yanawakutanisha watu wengi na yana upepo mzuri wa bahari ambao wengi wanaukosa siku za kawaida kutokana na kutopata nafasi hiyo.

Hata hivyo, ni muhimu kuzingatia suala la usalama. Tambua kwenda ufukweni si lazima uogelee, unaweza kuangalia mawimbi ya bahari na kupigwa na upepo mwanana. Kukutana na watu wapya pia ni jambo zuri la kutarajia ufukweni.

Eneo hilo linahitaji uangalizi wa karibu wa watoto kutokana na fukwe nyingi za umma kutokuwa na usimamizi mzuri, jambo linaloweza kuwaweka watoto hatarini kama kuzama majini au kufanyiwa vitendo vya ukatili. Msimamizi wa bwawa la kuogelea lililopo eneo la Mbezi Beach, Hamisi Heri anasema wameongeza umakini katika kuhudumia wageni wao, ili kuepukana na changamoto zinazojitokeza ikiwepo kuzama au kubanwa kwa misuli wakati wa kuogelea.

Anasema kitu cha kuzingatia kwa familia siku ya leo na kesho ni kuwa karibu na watoto wao kutoka na wingi wa watu katika maeneo ya kuogelea.

“Ninatoa tahadhari kuna watu hawajui kuogelea wao na watoto wao waseme mapema ili tuwaweke kwenye uangalizi, hata linapotokea tatizo tunajua ni namna gani ya kuwasaidia,” anasema Heri.

 

Tembelea ndugu, jamaa

Krismasi ni siku ambayo familia nyingi zinatembeleana na kula chakula pamoja. Watoto wanapata nafasi ya kufahamiana kwa karibu na kujenga ukaribu utakaowasaidia hata wakiwa watu wazima.

Ni vema ukaitumia siku hii kuwatembelea ndugu, jamaa na marafiki, ili kuimarisha uhusiano wa familia zenu. Siku hii ni muhimu kwa kuwa inawaleta karibu, tofauti na siku nyingine ambazo watoto wanakuwa shule na wazazi wanakuwa na kazi nyingi.

Mkazi wa Tabata, Hanson Kaijage anasema,“Hii ni fursa ya kukaa na ndugu, jamaa, majirani na marafiki ili kupata la kuzungumza mbali na salamu za asubuhi na za jioni pale mnapokutana kwa bahati mbaya.”

Mbali hilo, unaweza kutumia sikukuu yako kwa kusaidia wasio na uwezo na wenye mahitaji maalumu. Kama una uwezo, unaweza kutembela familia za watoto yatima, wazee, wajane na wengine ambao sikukuu kwao ni kama siku nyingine za kawaida.
 

Polisi laimarisha usalama

Jeshi la Polisi limesema limejipanga vizuri kuimarisha ulinzi maeneo mbalimbali yakiwepo nyumba za ibada ambako ibada za mkesha na sikukuu zinafanyika.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Davis Misime alisema watashirikiana na vikundi vya ulinzi shirikishi na kampuni binafsi za ulinzi kufanyaa doria maeneo mbalimbali.

“Kwa wale watakaoshindwa kujitambua na kujithamini na kujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu wa jinai na kutokuzingatia sheria za usalama barabarani, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani,” alisema.

Misime alisema wanaendelea kutoa wito kwa wananchi katika kusheherekea sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya ili waendelee kuwa salama wakiongozwa na kaulimbiu isemayo “usalama unaanza na mimi mwenyewe kwanza.”