Maendeleo ya Jamii waja na mpango kizazi cha Tanzania ya 2050
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima akizungumza wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis
Muktasari:
- Utekelezaji wa vipaumbele hivyo umegusia katika eneo la kujenga mtaji watu wa Taifa na kizazi cha Tanzania ya 2050, kinachozingatia maadili, uzalendo, haki, usawa, ustawi na maendeleo jumuishi na kuimarisha huduma za ustawi, malezi na makuzi ya watoto.
Dodoma. Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, imetaja vipaumbele saba itakavyovitekeleza katika mwaka wa fedha 2026/27 kupitia bajeti ya Sh108.02 bilioni iliyoomba kuidhinishiwa na Bunge.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo bungeni leo Jumatatu, Juni Mosi, 2026, Waziri wa wizara hiyo, Dk Dorothy Gwajima amesema vipaumbele hivyo vinalenga kujenga mtaji watu wa Taifa na kizazi cha Tanzania ya mwaka 2050 kinachozingatia maadili, uzalendo, haki, usawa, ustawi na maendeleo jumuishi.
Waziri Gwajima amesema eneo lingine la kipaumbele ni kuimarisha huduma za ustawi, malezi na makuzi ya watoto pamoja na mifumo ya ulinzi wa kijamii na uthabiti wa Taifa ili kuendeleza mshikamano, ustahimilivu na utu wa kibinadamu.
“Nyingine ni kuimarisha mifumo ya uwezeshaji wa wanawake, usawa wa kijinsia na kutokomeza ukatili wa kijinsia ili kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo. Pia tutafanya mageuzi ya uchumi wa makundi maalumu na sekta isiyo rasmi kutoka uchumi wa kujikimu kwenda uchumi rasmi wa kibiashara,” amesema Dk Gwajima.
Ametaja kipaumbele kingine kuwa ni kuimarisha matumizi ya teknolojia ya kidijitali na takwimu katika utoaji wa huduma za kijamii ili kuboresha utendaji na maamuzi yanayotegemea ushahidi wa kitaalamu.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, wizara pia inalenga kujenga jamii yenye amani, uwajibikaji na mshikamano pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za dini, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima na Naibu waziri wake, Maryprisca Mahundi wakipongezana mara baada ya kuwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis
Dk Gwajima amesema mwelekeo wa bajeti hiyo umeandaliwa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayosisitiza uwezo wa watu na maendeleo ya jamii, pamoja na mipango ya kimkakati ya wizara na taasisi zake.
“Dira 2050 haitajengwa kwa saruji na majengo pekee, bali kwa watu wenye uwezo, jamii zenye mshikamano, wanawake wenye nguvu, watoto wenye maadili na wananchi wanaoshiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia wizara hiyo itaendelea kujenga msingi wa Tanzania yenye ustawi wa jamii, usalama wa kijamii, uchumi jumuishi na maendeleo endelevu kuelekea mwaka 2050.
Katika utekelezaji wa bajeti hiyo, wizara inalenga kuongeza upatikanaji wa mikopo, mitaji na huduma za kifedha kupitia taasisi mbalimbali za fedha pamoja na kuongeza idadi ya wanufaika wa mikopo yenye masharti nafuu.
Wakati huohuo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo na Ustawi wa Jamii imeishauri Serikali kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu kwa wafanyabiashara wadogo kuhusu umuhimu wa kujiandikisha katika mifumo rasmi ya utambuzi na usajili.
Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo, Mwenyekiti wake, Hawa Chakoma amesema Serikali inapaswa kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo kwa wafanyabiashara hao pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa marejesho ili wananchi wengi zaidi wanufaike na fursa hizo.
Pia, ameitaka Serikali kuajiri maofisa ustawi wa jamii zaidi ili kukidhi mahitaji yaliyopo nchini na kuhakikisha wataalamu hao wanapatikana katika hospitali, shule, mahabusu, mahakama na maeneo mengine muhimu ya kijamii.
Aidha, kamati hiyo imependekeza kuundwa kwa bodi ya wataalamu wa ustawi wa jamii ili kuimarisha taaluma hiyo na kuhakikisha wanaozalishwa nchini, wanakidhi mahitaji ya soko la ajira.
“Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi na sekta binafsi, iongeze kasi ya ujenzi wa vituo salama vya malezi ya watoto ili huduma hizo ziwafikie wananchi wengi zaidi nchini,” amesema Chakoma.
Kamati hiyo pia imeishauri Serikali kufanya mapitio ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ili kuondoa maeneo yanayokinzana na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, sambamba na kutafuta njia bora ya kutekeleza sera ya matibabu bure kwa makundi maalumu.
Wakijadili hoja, baadhi ya wabunge wametoa maoni kuhusu masuala ya maadili, usawa wa kijinsia na mapambano dhidi ya ukatili kwa wanawake na watoto.
Mbunge wa Viti Maalumu (Wenye Ulemavu), Nasriya Nasir Ali amesema pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali, mapambano dhidi ya ukatili yanahitaji ushirikiano mkubwa zaidi wa wadau mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika kutokomeza vitendo hivyo.
Amesema jukumu hilo halipaswi kubebwa na wizara pekee, bali linahitaji ushiriki wa jamii nzima kwa lengo la kulinda haki na ustawi wa wanawake na watoto nchini.