Serikali kuwabana wanaotukana mtandaoni, mawakili wapewa jukumu
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Juma Homera, akizungumza leo Jumatatu Mei 18, 2026 katika mafunzo kwa Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OSG), jijini Arusha.
Muktasari:
- Serikali imeanza kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuitukana.
Arusha. Serikali imesema haitawavumilia wanaotumia mitandao ya kijamii na majukwaa mbalimbali ya kidijitali kuitukana, kusambaza taarifa za uchochezi na maudhui yanayokiuka maadili ya Kitanzania.
Kauli hiyo imetolewa leo, Jumatatu Mei 18, 2026 jijini Arusha na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Juma Homera, alipokuwa akizungumza katika mafunzo ya mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
Amesema Serikali inatambua haki ya wananchi kueleza maoni yao, lakini haitavumilia matumizi ya mitandao kwa ajili ya upotoshaji, uchochezi na kusambaza taarifa za uongo dhidi ya Serikali.
“Wananchi wana haki ya kusema yale ambayo ni ya kweli na yenye msingi kuhusu Serikali. Lakini kwa yale ya kubuni, ya uongo na yenye lengo la kupotosha jamii, haitasita kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Amesema tayari Serikali, kwa kushirikiana na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima, imeandaa orodha ya watu wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya kukiuka maadili mitandaoni.
“Kuhusu watu wanaoitukana Serikali na kutoa maneno ya uchochezi, nitoe shaka kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuchukua hatua. Kwa kushirikiana na Waziri Gwajima tayari tuna orodha ambayo imekabidhiwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,” amesema.
Amesema Serikali inaendelea na juhudi za kuhakikisha amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa unadumishwa sambamba na kulinda maadili ya jamii ya Kitanzania.
“Kuna sheria mbalimbali ikiwemo sheria za mitandao ambazo zinaendelea kutekelezwa kuhakikisha wanaopotosha jamii kwa makusudi wanachukuliwa hatua,” amesema.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro, amewataka mawakili wa Serikali kuhoji nafasi yao katika kipindi ambacho mashambulizi na upotoshaji dhidi ya Serikali vinaongezeka.
“Sisi kama wanasheria majukumu yetu ni nini tunapoona Serikali inatukanwa mtandaoni kwa jambo la uongo ambalo ni kinyume cha sheria? Tutawaachia TLS peke yao bila sisi kusimama?” amehoji.
Amesema huo ni mtihani kwa wataalamu wa sheria kuja na mikakati ya namna ya kulitumikia Taifa siyo mahakamani pekee, bali hata nje ya mahakama.
Migogoro ya ardhi yatishia amani
Katika hatua nyingine, Dk Ndumbaro amesema migogoro ya ardhi imeendelea kuwa changamoto nchini na inaweza kuhatarisha amani ya Taifa endapo haitapatiwa ufumbuzi wa haraka.
Amesema takwimu za kampeni ya Samia Legal Aid zinaonyesha kuwa asilimia 36 ya migogoro yote iliyoripotiwa nchini inahusiana na ardhi.
Amewataka wataalamu wa sheria kufanya tafiti na kuibua suluhu za kisheria na kimfumo ili kudhibiti migogoro hiyo kabla haijaendelea kuathiri utulivu wa nchi.
Kwa upande wake, Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Ally Possi, amesema kuanzia Julai 2025 hadi Machi 2026 ofisi yake ilihitimisha mashauri 641 ya madai. Serikali ilishinda 565 sawa na asilimia 88.1.
Amesema ushindi huo uliisaidia Serikali kuokoa zaidi ya Sh316.2 bilioni.
Aidha, amesema mashauri 18 ya usuluhishi yaliyohitimishwa katika kipindi hicho yaliisaidia Serikali kuokoa Sh6.8 bilioni pamoja na Dola za Marekani 418.1 milioni (zaidi ya Sh1.09 trilioni) ambazo Serikali ingelipa kama ingeshindwa.
“Mafanikio haya yametokana na usimamizi madhubuti wa mashauri pamoja na matumizi ya majadiliano na usuluhishi katika kutatua migogoro kabla haijafikishwa mahakamani,” amesema.
Dk Possi, amesema ofisi yake pia ilifanyia kazi notisi 765 za siku 90 za nia ya kuishtaki Serikali, hatua iliyosaidia kufikia mwafaka katika baadhi ya migogoro na kuokoa gharama kubwa za kesi, riba na fidia.