Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Madhara ya kiafya wanayoweza kupata wasugua miguu, kucha

Muktasari:

  • Biashara ya kutengeneza kucha na kusafisha miguu ni maarufu, hasa katika miji mikubwa hapa nchini.

Biashara ya kutengeneza kucha na kusafisha miguu ni maarufu, hasa katika miji mikubwa hapa nchini.

Katika jiji la Dar es Salaam, mitaa mingi kuna wafanyabiashara hiyo kuanzia Posta hadi Buza kwa Lulenge, achilia mbali wanaopita mitaani wakitafuta wateja.

Wafanyaji wakubwa wa biashara hii ni vijana wa kiume, ambao hukaa chini kati ya saa 8 mpaka 10 kwa siku wakiwasugua wanawake miguu na kuwabandika kucha.

Gazeti la Mwananchi lilipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na kufanya mahojiano na baadhi ya vijana wanaojihusisha na biashara hiyo ambao walikuwa na mengi ya kusema, lakini kubwa kukabiliana na uchovu wa kukaa siku nzima.

“Pesa tunapata, siwezi kutaja bei kwa sababu inategemea mhusika anataka kufanyiwa nini na nini, ila nachoka sana, ikifika saa mbili usiku ninakuwa hoi,” anasema Rajabu Biyagaze, anayefanya shughuli zake eneo la Sudan, Temeke.

Naye Joseph William anayefanya shughuli zake maeneo ya Tabata Bima anasema kuwa anadhani siku zijazo itabidi aweke vijana wa kumsaidia kwa sababu anakosa muda wa kupumzika.

“Nilipoanza nilikuwa nina wateja wachache, siku hizi wamekuwa wengi karibu kila siku ninaamka na oda, achilia mbali wale wanaokuja bila kutoa taarifa.

“Nachoka sana, ninashinda nimekaa kuanzia saa mbili asubuhi mpaja saa 12 jioni siku za kawaida, mwisho wa juma mpaka saa 2 usiku inanikuta hapa hapa,” anasema William.

Kuhusu wapi hasa anasikia maumivu au ni uchovu tu, anasema: “Kwa kweli mgongo, si unajua hizi kazi unainama kuwasugua miguu na kubandika kucha.

“Hata kama kuna vifaa, kuinama ni lazima ndiyo maana mgongo ndiyo unaochoka na kuuma, wakati mwingine nasikia maumivu hadi kifuani, najua ni kwa sababu ya kuinama muda mwingi,” anasema.

Naye Zubeir Kiemena anasema anawafuata wateja mitaani kwa kuzunguka, mara nyingi anaitwa kwenye saluni za wanawake kwa ajili ya kuwasafisha kucha na kuwasugua miguu.

Anasema tofauti na wenzake wanaowakosha kwenye mabeseni yenye maji mengi, yeye huwasugua na kuwasafisha kwa kuwanyunyizia maji machache na kuwafuta na taulo.

“Ninapata pesa sikosi Sh50,000 na kuendelea kila siku, ila ninachoka natembea sana mpaka miguu na mgongo vinauma, lakini ndiyo kazi.

“Nina karibu miaka mitano nafanya kazi hii kiasi naona nimeyazoea maumivu, kuna siku siyasikii kabisa,” anasema Kiemena, aliyetoka Kigoma miaka sita iliyopita kuja kufanya kazi hiyo baada ya jamaa zake waliotangulia kumpa mbinu.


Madhara ya kukaa muda mwingi kiafya

Daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Dk Lemery Mchome anasema uzoefu unaonyesha watu saba kati ya 10 wanaofika kliniki hapo wanalalamika maumivu ya mgongo bila kujua chanzo chake.

Dk Mchome alisema kitaalamu dakika za kukaa zinategemeana na uzito, umri na afya ya mtu huku makadirio yakiwa ni kati ya dakika 45 hadi saa nne.

“Watu kati ya 20 hadi 30 tunaowapokea kliniki malalamiko yao yanafanana, atakwambia naumwa mgongo, mwingine ukiangalia diski kweli zimetoka anatakiwa kufanyiwa upasuaji, lakini wengine unakuta misuli imekaza na inauma,” alisema Dk Mchome.

Alisema pia aina ya viti vinavyotumika kukalia, vikiwamo vya chini sana vinavyoweza kusababisha mgandamizo wa diski hizo, huku akitilia shaka viti vingi kutozingatia mahitaji ya kulinda viungo, ukiwamo mgongo.


Afya

“Biashara hii inahusisha utumiaji wa vitu vyenye ncha kali, hivyo umakini wa hali ya juu unahitajika,” anasema Iddy Khamis maarufu Mtoto Iddy anayefanya shughuli zake Sinza, Dar es Salaam.

“Kuna kifaa maalumu hapa (huku anakionyesha) kwa ajili ya kuchemsha na kusafisha vifaa vyote vya chuma na kila siku asubuhi huwa tunaviingiza katika mashine hiyo na kuhakikisha mataulo yanakuwa masafi muda wote,” anasema.

Quiz Life yeye alisema kwenye ofisi yake usafi unafanyika kama kawaida, mataulo yanafuliwa kwa maji ya moto na vifaa vya kusafisha kucha pia wanaviweka kwenye maji ya moto.

“Kuna kifaa kinaitwa nail fale ni cha kutolea uchafu ndani ya kucha, kina ncha kali hivyo lazima kiwekwe kwenye maji ya moto, japo wapo wateja wasiopenda kutumia na watu wengine wananunua kipya kila wanapokuja,” anasema.

Anasema kuwa wateja miguu yao ina fangasi, hivyo wakisafishwa lazima taulo na vifaa vilivyotumika vifuliwe na maji ya moto ili kuepusha kuambukiza wengine magonjwa.


Kipato

Akizungumzia kuhusu anavyonufaika na biashara hiyo, Iddy anasema siku ikiwa nzuri anapata Sh300,000 au wakati wa sikukuu anaweza kupata hadi Sh500,000 kwa siku kwa sababu wateja wanakuwa wengi na siku akikosa kabisa hapati chini ya Sh100,000.

Quiz anasema fedha anayoingiza kwa siku inategemea na wateja, kwani kuna wakati anaweza akaondoka na Sh80,000 au Sh 100,000 na siku nyingine hata Sh5,000.


Changamoto

Patrick na Mr. Kucha wao wanasema changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni vishawishi kutoka kwa wanawake wanaokwenda kupata huduma katika ofisi zao.

“Kama huna Mungu hii kazi ina changamoto kubwa sana, kwani kuna wakati anaweza akaja mwanamke amevaa nguo fupi ukampa taulo ajifunike anakataa kwa madai kuwa haamini usafi wake,” anasema Mr. Kucha.

Patrick anasema “kuna wakati wateja wanatupa vishawishi kwa kututega, kwani wapo wale wanaotuitaga tukawatengeneze kucha wakiwa nyumbani, ukifika wanaanza kukushika, lakini kwa sababu ndio kazi tuliyoichagua na ndiyo inayotuweka mjini inabidi tuwe na roho ngumu,” anasema Patrick.

Pia wameongeza kuwa changamoto nyingine wanayokumbana nayo ni baadhi ya wanawake kutaka huduma lakini wanakuwa hawana fedha ya kulipia jambo linalochangia kuwarudisha nyuma.