Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Madereva bajaji, trafiki ngoma nzito Mbeya

Picha mbalimbali za Bajaji jijini Mbeya zikiwa zimefungwa ngao maalumu kwa ajili ya usalama wa vyombo hivyo, abiria na madereva

Muktasari:

  • Madereva wa bajaji Mbeya wamegomea ngao, wakitaka abiria wanne huku Polisi wakisisitiza kusimamia sheria.

Mbeya. Madereva wa bajaji jijini Mbeya wamepinga agizo la Jeshi la Polisi la kuondoa ngao zilizowekwa kwenye vyombo vyao, wakidai ni sehemu ya ulinzi dhidi ya uharibifu unaosababishwa na magari mengine pamoja na dharau wanazokutana nazo barabarani.

Hayo yamebainishwa leo Julai 23 wakati wa kikao maalumu cha umoja wa madereva Bajaji jijini humo, kilichohusisha Jeshi la Polisi mkoani humo, ambapo pamoja na mambo mengine walijadili muelekeo mpya wa kundi hilo katika majukumu yao.

Pia, wameeleza changamoto zinazowakabili katika shughuli zao, zikiwemo kukamatwa mara kwa mara kwa bajaji, ushuru na faini mbalimbali, pamoja na kucheleweshewa leseni licha ya baadhi yao kukidhi vigezo.

Aidha, wameahidi kushirikiana na vyombo vya dola kuwafichua madereva wa bajaji wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu.

Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Bajaji Jijini Mbeya, Lucas Mwakyusa, amesema madereva hao ni walipa kodi wanaochangia uchumi wa nchi, hivyo wanahitaji ushirikiano na malezi badala ya kukamatwa mara kwa mara.

Amesema ombi lao kubwa ni kuruhusiwa kuendelea kutumia ngao kwenye bajaji kwa kuwa zimekuwa zikiwalinda dhidi ya uharibifu unaotokana na kugusana na magari makubwa, hususan daladala.

Waendesha bajaji jijini Mbeya wakiwa katika mkutano wao maalumu uliofanyika leo Julai 23, 2026 jijini Mbeya

"Hatujaweka ngao kwa bahati mbaya, ni kwa ajili ya kulinda vyombo vyetu. Ni kweli baadhi ya madereva hawafuati sheria, lakini sisi wenyewe tuko tayari kuwachukulia hatua na kuwafichua wanaokiuka taratibu," amesema.

Mwakyusa amekiri pia kuwa baadhi ya madereva wamekuwa wakibeba abiria zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa kisheria, akisema hali hiyo inachangiwa na kupanda kwa gharama za uendeshaji, ikiwemo mafuta.

Naye dereva wa bajaji, Jackson Mwaisunga, amesema pamoja na kupongeza elimu iliyotolewa na Jeshi la Polisi, bado hawakubaliani na agizo la kuondoa ngao.

"Kwetu sisi ngao ni kinga ya chombo, dereva na hata abiria dhidi ya magari mengine. Tunafahamu sheria inaruhusu kubeba abiria watatu, lakini kutokana na gharama za mafuta wakati mwingine tunapata hasara. Hata hivyo, suala la stika na leseni ni muhimu na tuko tayari kulizingatia," amesema.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, Notker Kilewa, amesema kila dereva anatakiwa kuwa na leseni halali ya udereva na bima ili kulinda usalama wake na wa watumiaji wengine wa barabara.

Kilewa amesema Jeshi la Polisi halitasita kuendelea kutoa elimu na kusimamia sheria, huku akitoa agizo kwa wamiliki wa bajaji kuondoa ngao zilizowekwa kwenye vyombo hivyo.

"Kuanzia Jumatatu, wenye bajaji zilizowekwa ngao waziondoe kwa sababu zinaharibu magari mengine zinapogongana. Kuanzia Agosti 1 tutaanza operesheni dhidi ya bajaji zisizo na stika. Hatutaki kukamata watu, tunataka sheria zifuatwe," amesema Kilewa.

Aidha, amesema madereva wote wenye vyeti vinavyokidhi vigezo wanapaswa kufuata utaratibu ili wapatiwe leseni bila kucheleweshwa.



"Jukumu langu ni kutoa elimu na kusimamia sheria. Ningeweza kuanza operesheni ya kuwakamata wasio na leseni, bima au wanaobeba abiria kupita kiasi, lakini nimeamua kuanza na elimu kwa kuamini watatekeleza sheria kwa hiari," amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa huo, SACP Antony Mkwawa, amewataka madereva kushirikiana na Jeshi la Polisi katika mapambano dhidi ya uhalifu.

"Tunaomba mtusaidie kuwafichua wahalifu na kujitokeza kutoa ushahidi ili tukomeshe vitendo vya uhalifu. Kuhusu leseni, naelekeza wale wote wenye sifa na vyeti halali waanze kupatiwa leseni kuanzia leo," amesema.