Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Madeleka, Jamhuri walivyochuana kasoro hati ya mashtaka ya upatu

Muktasari:

  • Wakili Madeleka ameibua pingamizi la hoja za kisheria kuhusiana na uhalali wa hati ya mashtaka katika ya washtakiwa wa upatu iliyokubaliwa na mahakama na kuilazimu Jamhuri kuiondoa na kwenda kuifanyia marekebisho hati ya mashtaka.

‎Dar es Salaam. ‎ Jamhuri imelazimika kuondoa mahakamani hati ya mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wa Kampuni ya Atlantic Micro-Credit Limited na kuwasilisha hati mpya iliyofanyiwa marekebisho, baada ya pingamizi la kisheria lililoibuliwa na wakili wa utetezi, Peter Madeleka.

Washtakiwa katika kesi hiyo namba 4521 ya mwaka 2026 ni Wendy Ishengoma, anayetajwa kuwa mkurugenzi wa kampuni hiyo, Sultan Mdee, Frank Tengia, Mwiga Mwiga pamoja na kampuni ya Atlantic. Wanakabiliwa na mashtaka sita ya kuongoza genge la uhalifu, kuendesha shughuli za upatu, utakatishaji fedha haramu wa zaidi ya Sh5.046 bilioni na kuendesha shughuli za kibenki kinyume cha sheria.

Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Sharmillah Sarwatt wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Mkurugenzi wa kampuni ya Atlantic Micro-Credit Ltd, Wendy Ishengoma (kushoto) ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya upatu inayomkabili na wenzake, akimsikiliza wakili wake Peter Madeleka, katika ukumbi wa mahakama, kabla ya kesi yao kuanza.

Pingamizi la Madeleka lilitolewa leo Juni 4, 2026 wakati washtakiwa wakisomewa mashtaka kwa ajili ya kuyajibu kabla ya hatua ya usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo.

Awali, Madeleka alipinga hatua ya upande wa mashtaka kueleza kuwa mshtakiwa wa kwanza, Wendy Ishengoma, anaiwakilisha kampuni ya Atlantic ilhali maelezo hayo hayakuwepo kwenye hati ya mashtaka iliyowasilishwa mahakamani. Alisisitiza kuwa hati ya mashtaka inapaswa kujieleza yenyewe na kwamba maelezo hayo hayawezi kuongezwa kwa mdomo bila kufanyiwa marekebisho rasmi.

Baada ya mjadala huo, pingamizi kubwa zaidi lilitolewa wakati wa usomaji wa shtaka la utakatishaji fedha. Madeleka alidai kuwa hati ya mashtaka ilitaja kifungu cha sheria ambacho hakipo kutokana na hitilafu ya uandishi katika rejea ya kifungu cha Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji Fedha.

Upande wa mashtaka, ukiongozwa na mawakili wa Serikali waandamizi, Frank Nchamila na Achile Mulisa, ulikubali kuwapo kwa hitilafu hiyo lakini ukadai ni kosa la kalamu na kuomba kurekebisha kwa mdomo. Hata hivyo, Madeleka alipinga hatua hiyo na Mahakama ikakubaliana naye kuwa utaratibu sahihi ni kuwasilisha hati mpya iliyofanyiwa marekebisho.

Kutokana na uamuzi huo, Jamhuri iliwasilisha hati mpya ya mashtaka na washtakiwa wakasomewa upya mashtaka yote, ambayo waliyakana.

Katika hatua ya usikilizwaji wa awali, washtakiwa walikubali majina yao pekee na kukataa maelezo mengine yote ya Jamhuri yanayoeleza namna walivyotenda makosa wanayotuhumiwa.

Mkurugenzi wa kampuni ya Atlantic Micro-Credit Ltd, Wendy Ishengoma (kushoto) ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya upatu inayomkabili na wenzake, akimsikiliza wakili wake Peter Madeleka, katika ukumbi wa mahakama, kabla ya kesi yao kuanza.

Jamhuri imeieleza Mahakama kuwa itakuwa na mashahidi 27 na vielelezo 987, ambapo 978 ni nyaraka na tisa ni vielelezo halisi vikiwemo magari. Upande wa utetezi umeeleza kuwa utawasilisha orodha ya mashahidi wake baadaye wakati kesi ikiendelea.

Jaji Sarwatt ameahirisha kesi hiyo hadi tarehe itakayopangwa ndani ya siku 30 zijazo kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi