Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Madeleka alivyoitega Jamhuri uhalali kesi ya upatu

Wakili Peter Madeleka.

Muktasari:

  • Mvutano uliibuka kuhusu hoja ya mshtakiwa kumwakilisha mshtakiwa mwingine na washtakiwa kuitwa kujibu mashtaka nje ya muda wa kikanuni.

Dar es Salaam.  Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi  imesimamisha usikilizaji wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Wendy Ishengoma, mkurugenzi wa kampuni ya mikopo ya fedha, Atlantic Micro Credit Limited na wenzake, ili kujiridhisha kwanza kama inastahili kuisikiliza.

Hatua hiyo ilitokana na pingamizi aliloliibua wakili wa washtakiwa hao, Peter Madeleka akidai mahakama hiyo haipaswi kuisikiliza kesi hiyo kutokana na upande wa mashtaka kukiuka kanuni za uendeshaji kesi za uhujumu uchumi.

Madeleka alidai moja ya kanuni iliyokiukwa ni mmoja washtakiwa kumwakilisha mshtakiwa mwenzake katika kesi hiyo na washtakiwa kuitwa kujibu mashtaka na usikilizwaji wa awali, nje ya muda uliowekwa na kanuni hizo.

Madeleka aliibua pingamizi na hoja hizo Ijumaa Mei 29, 2026, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya washtakiwa kujibu mashtaka hayo na usikilizwaji wa awali na kuibua mvutano wa hoja za kisheria baina yake na upande wa Jamhuri.

Kutokana na hoja hizo usikilizwaji wa kesi hiyo ulisimama na Jaji Sharmillah Sarwat aliiahirisha hadi Juni 3, 2026 atakapotoa uamuzi utakaotoa hatima ya kesi hiyo.

Mbali na Wendy, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni maofisa wa kampuni hiyo Sultan Mdee ambaye ni mhasibu; Frank Tengia, meneja wa tawi na Mwiga Mwiga, ambaye ni ofisa masoko.

Awali, washtakiwa hao walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu kwa ajili kukamilisha taratibu za awali na kukamilishaa upelelezi kabla ya kuikabidhi Mahakama Kuu, kwa kuwa yenyewe haina mamlaka kusikiliza kesi kubwa za uhujumu uchumi.

Washtakiwa walisomewa mashtaka matatu, ya kuongoza genge la uhalifu kwa kufanya biashara ya upatu, wakidaiwa kulitenda kati ya Januari 18, 2024 na Oktoba 11, 2024 ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Shtaka la pili ni kuendesha biashara ya upatu, wakidaiwa kuwa katika kipindi hicho walifanikisha mpango wa kuendesha biashara ya upatu kwa kutoa ahadi kwa wanachama na kuingia mikataba ya ubia yenye thamani ya zaidi ya Sh3.63 bilioni kinyume na sheria.

Shtaka la tatu ni kutakatisha fedha, wakidaiwa kuwa katika kipindi hicho jijini Dar es Salaam, walijipatia Sh3.6 bilioni na kisha kuzitakatisha wakati wakijua kuwa fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la jinai la kuendesha biashara ya upatu.

Jana Mei 29, 2026, kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya washtakiwa kujibu mashtaka hayo kukubali au kukana na kusomewa maelezo ya makossa yao, lakini kabla ya kuanza hatua hiyo ndipo Madeleka akaibua pingamizi hilo.

Katika hoja ya kwanza Madeleka alidai kuwa kuna ukiukwaji wa kanuni ya 8(1-6) ya Kanuni Sheria ya Uhujumu Uchumi za Utaratibu wa Uendeshaji Kesi za Uhujumu Uchumi za mwaka 2016.

‎Alifafanua kuwa kanuni hiyo ikisomwa pamoja na kifungu cha 260(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) inataka washtakiwa wote wasomewe mwenendo kabidhi.

Hata hivyo, alidai kuwa ‎mwenendo kabidhi  uliofanyika Aprili 16, 2026 katika Mahakama ya Kisutu, mshtakiwa wa tano (kampuni ya Atlantic) haikusomewa mwenendo huo  kwa kuwa mwakilishi wake hawepo mahakamani.

‎Alisema amri kabidhi (maelekezo ya Mahakama ya Kisutu kuwakabidhi washtakiwa kwa Mahakama Kuu) inaonesha kuwa mshtakiwa wa tano akiwakilishwa na mshtakiwa wa kwanza (Wendy) kwenye mwenendo kabidhi.

"Lakini, amri hiyo haisemi huo uwakilishi ulifanyika chini ya sheria gani," alieleza Madeleka.

Aliendelea kuwa ‎kifungu cha 110(1) na (2) cha CPA kinasema kuwa uwakilishi wa kampuni utafanywa na ofisa sheria na kwamba kifungu hicho hakimfanyi mshtakiwa kustahili kumwakilisha mshtakiwa mwingine.

‎Hivyo, alisema kwa kuwa mshtakiwa wa tano hakukabidhiwa kwa mahakama hiyo, wala utaratibu wa kuishtaki kampuni kijinai kama unavyoelezwa katika Sheria ya Kampuni na namna ya kuwashtaki wakurugenzi kwa niaba ya kampuni haukufuatwa, Mahakama haipaswi kuendelea na mwenendo wa kesi hiyo.

‎"Mheshimiwa jaji, kwa kuwa si tu mshtkiwa wa tano hakukabidhiwa kwenye mwenendo kabidhi, hata hapa mbele yako hayupo. Hiyo ni kasoro kubwa na ninaomba mahakama yako itoe amri kuhusu kasoro hiyo," alisema Madeleka.

‎Alisisitiza kuwa kanuni 8(3) inataka hakimu amsomee mwenendo kabidhi mshtakiwa husika si kuwakilishwa na kwamba  mshtakiwa wa kwanza hajashtakiwa kwa niaba ya mshtakiwa wa tano, hivyo   haiwezekani huo uwakilishi ukaonekana kwenye mwenendo kabidhi tu.

Katika hoja ya pili‎ Wakili Madeleka alidai kuwa kuna ukiukwaji wa kanuni ya 13 ya inayoelekeza washtakiwa wajibu mashtaka na kufanya usikilizaji wa awali ndani ya siku 30 baada ya Mahakama Kuu kupokea amri kabidhi.

‎Alisema kumbukumbu za kesi hiyo zinaonyesha kuwa mpaka Aprili 20, siku nne tu tangu kufanyika mwenendo kabidhi Mahakama Kuu ilikuwa imeshapokea amri kabidhi kutoka Mahakama ya Kisutu.

"‎Kwa kuanzia Aprili 20, siku 30 zinaisha Mei 20, 2026. Kwa hiyo mpaka leo Mei 29 ni siku tisa zaidi zimepita kinyume na kanuni inavyoelekeza," alisema Madeleka na kusisitiza:

 "‎Kwa maoni yangu hatua hii inafanyika kinyume na kanuni na nimesoma kanuni zote hakuna mahali ambako Mahakama imepewa mamlaka kuendesha hatua hii nje ya kanuni."

‎Aliongeza kuwa Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake kwenye moja ya rufaa, ilishasema kuwa sheria inapotaja muda rasimi, muda huo lazima uzingatiwe.

"Kwa kuwa Mahakama hii inafungwa na uamuzi wa Mahakama ya Rufani, basi hatua sahihi ni kuwaachia huru washtakiwa, kwa maana nyingine hakuna kesi mbele yako," alisisitiza Madeleka.

Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Frank Nchanila alieleza kuwa kifungu cha 110 (1) na (3) cha CPA kinatoa namna kampuni inavyoweza ikafikishwa mahakamani inapofanya makosa, kupitia ofisa wa kampuni ambaye ni pamoja na mkurugenzi.

Alisema wakili wa washtakiwa angesubiri washtakiwa wasomewe maelezo ya awali ya kesi na ushahidi utolewe kwa ‎kubainisha jukumu la kila mtu na kwamba mshtakiwa wa kwanza ni mkurugenzi wa hiyo kampuni.

"Hayo yasingeweza kuelezwa kwenye hati ya mashtaka. Kwa hiyo ni maoni yetu huyu mshtakiwa wa tano amekabidhiwa kwa mujibu wa sheria," alisema Wakili Nchanila.

‎Katika hoja ya pili, Wakili wa Serikali Mwandamizi Achile Mulisa pamoja na mambo mengine aliiomba mahakama itupilie mbali hoja za Wakili Madeleka akidai kuwa hajasema ni kwa vipi ucheleweshaji usikilizwaji kesi hiyo katika hatua hiyo anaoulalamikia umewaathiri wateja wake kiasi cha kufanya waachiwe huru.

Akijibu hoja za mawakili wa Serikali, Wakili Madeleka pamoja na mambo mengine alisema hakuna mahali kifungu cha 110 cha CPA kilichotajwa,  kinasema wakili au ofisa akiiwakikisha kampuni mahakamani  anabadilika kuwa mshtakiwa.

‎Alieleza kuwa hakueleza wateja wake walivyoathirika kwa ukiukwaji huo wa kanuni ya 13, kwa kuwa hakuna mahali kanuni inamtaka aeleze hilo, kama ambavyo hata Wakili wa Serikali hakusema kuna sheria inayomtaka kueleza namna wateja hao walivyoathirika kwa ucheleweshaji.