Mabwawa ya samaki kuinua uchumi Musoma

Muktasari:
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Vicent Naano alisema hivi karibuni kuwa, mradi huo unatekelezwa kwa lengo la kuunga mkono jitihada za Serikali inayohimiza ukuzaji wa uchumi kupitia viwanda.
Halmashauri ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kikosi jeshi namba 27 pamoja na wananchi, wametumia Sh47.315 milioni kujenga mabwawa saba ya mradi wa ufugaji wa samaki.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Vicent Naano alisema hivi karibuni kuwa, mradi huo unatekelezwa kwa lengo la kuunga mkono jitihada za Serikali inayohimiza ukuzaji wa uchumi kupitia viwanda.
“Njia hii ya ufugaji kwa kutumia mabwawa, itasaidia upatikanaji wa samaki kwa wingi, hii ni moja ya hatua za kukuza viwanda vinavyochakata samaki, licha ya kuongeza ajira lakini itaboresha lishe,” alisema.
Alifafanua kuwa mradi huo kwa jumla utagharimu Sh114.90 milioni na unatarajiwa kuwa na mabwawa 10, saba kati ya hayo yamekwishakamilika.
Mkazi wa Manispaa ya Musoma, Hashimu Hamisi anayekaanga samaki na kusafirisha katika mikoa ya mbali hapa nchini, alisema mradi huo utawasaidia kukuza kipato chao na watakuwa na uhakika wa kupata samaki wazuri.