Lwaitama atoa masharti yake kuwatetea kina Mdee

Dar es Salaam. Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, Dk Azaveli Lwaitama amesema wabunge 19 wa viti maalumu waliovuliwa uanachama wakitoka bungeni atakuwa wa kwanza kuwatetea ili waweze kurudi kwenye chama hicho.
Dk Lwaitama alieleza hayo jana, wakati akihojiwa maswali ya dodoso na wakili Ipilinga Panya katika kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama, iliyofunguliwa na Halima Mdee na wenzake 18 ambao ni wabunge wa viti maalumu.
Wabunge hao walivuliwa uanachama Novemba 27, 2020 baada ya Novemba 24, 2020 kuapishwa kuwa wabunge, huku Chadema wakidai hawakupeleka majina ya wabunge wa viti maalumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Hata hivyo, kina Mdee walipinga uamuzi huo kwa Baraza Kuu la Chadema ambalo Mei 11, 2022 lilibariki kutimuliwa kwao.
Mdee, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) na wenzake walifungua shauri hilo Mahakama Kuu Masjala Kuu ya Dar es Salaam, wakipinga kufukuzwa uanachama kwa utaratibu wa Mapitio ya Mahakama (Judicial Review).
Jana wakati akihojiwa, Dk Lwaitama aliulizwa kuhusiana na kielelezo ambacho ni video ikimuonyesha Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akieleza alivyomuita Halima Mdee Nairobi na kuzungumza kilichotokea.
Licha ya video hiyo kuonyesha Mbowe akieleza suala hilo mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu, Dk Lwaitama alidai kuwa waliwasilisha mahakamani hapo kama kielelezo ili kuonyesha chama kilivyokuwa na huruma dhidi yao na jinsi walivyotaka watubu na wasamehewe.
“Mwenyekiti alihangaika na Mdee kwa kuwa ndiye aliyekuwa na ushawishi kwa wenzake, hata leo wakitoka bungeni nitakuwa wa kwanza kuwatetea ili waweze kurudi kwenye chama.

Mjumbe wa Bodi ya wadhamini wa Chadema, Dk Azaveli Lwaitama (wa kwanza kushoto) akizungumza na jopo la mawakili linaloongozwa na Peter Kibatala (wa pili kushoto) katika Mahakama Kuu, wakati wa mapumziko wa kesi ya wabunge 19 wanaopinga kuvuliwa uanachama wa chama hicho. Picha na Sunday George
Sehemu ya mahojiano ilikuwa hivi;
Wakili Panya: Naomba uiambie mahakama nini ulitaka kuthibitisha kwa kuleta hiki kielelezo TL 6 Mahakamani?
Lwaitama: Ili kuonyesha namna chama kilivyokuwa na huruma dhidi yao na jinsi kilitamani wao watubu na wasamehewa.
Wakili Panya: Video inaonyesha akimuelezea Halima Mdee tu, je hao wengine 18 aliwaeleza?
Lwaitama: Alihangaika na Halima kwa kuwa yeye ndiye alikuwa na ushawishi kwa wenzake.
Waakili Panya: Ulijuaje kuwa alikuwa na ushawishi?
Lwaitama: Mimi najua kutoka kwenye akili yangu na nina uhakika hata wewe unajua pia.
Wakili Panya: Mkutano wa Baraza Kuu ulichukua muda gani kwenye video?
Lwaitama: Mheshimiwa Jaji mimi siyo mtaalamu wa masuala hayo, siwezi kujua hatua zote zilichukua muda gani
Wakili Panya: Unasema mwenyekiti alizungumza kabla ya Baraza Kuu kufanya uamuzi, ni kweli ulisema pia na kwenye maelezo yako? Alijua vipi kuwa baraza kuu litaamua
Lwaitama: Kwa kuwa alikuwa ameletewa rufaa na alijua baada ya Baraza Kuu likishaamua pengine atapoteza majembe kama hayo, ni kama alikuwa anawashawishi wajumbe wawasamehe.
Wakili Panya: Mbowe alizungumza kwa uzito wake kama Mwenyekiti wa Taifa?
Lwaitama: Ni kweli ila ukisikiliza kwa umakini maneno yale kuna mahali alisema ngoja nitoe ya moyoni, hilo haliwezi kuwa jambo la kitaasisi.
Wakili Panya: Jana tulizungumza kuhusu kura ya siri au ya wazi, Baraza Kuu lilifanya uamuzi wa kupiga kura ya wazi au siri?
Lwaitama: Mbele ya kikao cha Baraza Kuu wajumbe walihojiwa na kukubaliana kuwa kura iwe ya wazi na waliamua kuwa Naibu msajili abaki ukumbini.
Wakili Panya: Wakati kura zinapigwa walikuwepo watu wengine kama wewe na Sisty Nyahoza?
Lwaitama: Kura zilipigwa mbili, ya kwanza Baraza Kuu lilipiga kura ya kutaka wajumbe waalikwa wawepo, akiwemo Sisty Nyahoza na kura zote zilikuwa za wazi kwa makubaliano.
Wakili Panya: Kuna watu walioshiriki kwenye kikao kama wewe, Omary Othman, Jenerali Ulimwengu, Juma Duni Haji, Boby Wine, Askofu Emmaus Mwamakula.
Lwaitama: Wakati wa kura ya pili ya Baraza kuu hao hawakuwepo, tena nilibaki mimi Lwaitama na Sisty Nyahoza (Naibu Msajili).
Wakikli Panya: Wewe kama mdhamini wa Chadema na una katiba, moja ya jukumu ulilonalo ni kuiheshimu katiba?
Lwaitama: Naiheshimu na ndio maana ni mwanachama.
Wakili Panua: Unafuata vifungu vyote vilivyopo au kuna vifungu huvifuati?
Lwaitama: Sasa navifuataje sasa mimi nimekaa hapa muda huu.
Wakili Panya: Kwenye Katiba wajumbe wa bodi ya wadhamini siyo wajumbe wa Baraza kuu.
Lwaitama: Ndiyo siyo wajumbe.
Wakili Panya: Naomba Jaji ichezwe kielekezo HDM
Wakili Panya: Baada ya kuona hicho kielelezo HDM 08 bado unataka kusema huyo ndo mwenyekiti aliyekuwa anataka awasamehe?
Lwaitama: Kabisa
Wakili Panya: Mwenyekiti Mbowe alikuwa ni mmoja wa wapiga kura?
Lwaitama: Ni sahihi
Wakili Panya: Alipiga kura gani?
Baada ya mahojiano hayo, Jaji Cyprian Mkeha anayesikiliza kesi hiyo ameiahirisha hadi Aprili 18 na 19 kwa ajili ya Mollel kuanza kuhojiwa.
Mbali na Dk Lwaitama, wajumbe wengine wanaopaswa kuhojiwa ni Silivester Masinde, Ruth Mollel, Mary Florian Joachim, Francis Joseph Mush, Maulida Anna Komu na Ahmed Rashid Hamis.