Lukuvi awaonya wanaochangisha hela za urasimishaji kinyume na utaratibu
Dar es Salaam.Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewaonya wanaochangisha fedha kwaajili urasimishaji nje ya utaratibu na kuwataka waliofanya hivyo kuzirudisha ndani ya wiki mbili.
Lukuvi ametoa wito huo jijini Dar es Salaam baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakazi wa kata ya Kivule ya kuwepo kwa michango mingine tofauti na inayotozwa na Kamati ya urasimishaji.
Amesema gharama zilizotolewa na wizara zinafahamika hivyo hakuna anaeruhusiwa kuchangisha zaidi ya laki moja na nusu.
"Wapo wanaochangisha fedha tofauti na maelekezo, kazi ya urasimishaji iendelee lakini fedha zilizochangishwa nje ya utaratibu zirudishwe kwa wenyewe ndani ya wiki mbili wakati uchunguzi ukifanyika,"amesema Lukuvi
Pia Lukuvi amekerwa na ucheleweshwaji wa urasimishaji wa makazi kwenye kata ya Kivule na kumuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mary Makondo kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua wote walioshiriki na kusababisha uzembe tangu mwaka 2017.
Amesema wananchi 3446 wa kata hiyo ya wananchi 20,000, wamechanga zaidi ya Sh534 milioni tangu mwaka 2017 ambapo ni wananchi 22 tu ndio wameshapewa hati na kukitaka Chuo Kikuu cha Ardhi Morogoro ifikapo Juni 30,2021kiwe kimekamilisha zoezi la urasimishaji.
"Nataka chuo kianze kazi haraka na kwa gharama zao wenyewe, na wale ambao wameshawekewa mawe na kulipia wahakikishe wanapatiwa hati ndani ya miezi mitatu ,"amesema Lukuvi.
Awali akitoa taarifa kwa waziri, Katibu wa urasimishaji, Gisiri Anthon amesema kwa maazimio ya pamoja mwaka 2017 walifanya kikao cha pamoja na Chuo Kikuu cha Ardhi.
Almesema baada ya kukabidhiwa jukumu hilo hadi sasa wananchi 316 wamepata namba, 22 wameshapata hati na 3446 wameshatoa fedha kwa ajili ya urasimishaji.
"Wananchi 3446 wamechangia kiasi cha Sh534 milioni, waliopata hati hadi sasa ni watu 22 na wenye namba za ploti ni 316 tu,"amesema Anthon.