Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Askari wawili JWTZ wafariki dunia, wanne wajeruhiwa DRC

Dar es Salaam. Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limesema askari wake wawili wamefariki dunia na wengine wanne wamejeruhiwa wakitekeleza majukumu ya ulinzi wa amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo.

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumapili Februari 2, 2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Kanali Gaudentius Ilonda.

“Kufuatia mashambulizi ya mfululizo katika maeneo ya Sake na Goma yaliyofanywa na waasi wa M23 Januari 24 na 28, 2025, JWTZ limewapoteza askari wake wawili na wengine wanne kujeruhiwa. Majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu mjini Goma.

“Taratibu za kuisafirisha miili ya marehemu wetu pamoja na majeruhi waliotokana na mapigano hayo zinaendelea kupitia Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Mwenyezi Mungu awape uponyaji wa haraka majeruhi wetu na aziweke roho za marehemu mahali pema peponi, amina,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa vikundi vya JWTZ vilivyopo nchini DRC vipo salama, imara na vinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa maelekezo ya uongozi wa SADC.

JWTZ inaendelea kulinda amani kwa Mwamvuli wa SADC huko Mashariki mwa nchi ya DRC (SAMDRC) eneo ambalo limekumbwa na mgogoro uliozua mashambulizi kati ya waasi wa M23 wanaopambana na Jeshi la DRC (FARDC).


Vifo vya askari wengine

Taarifa ya JWTZ imetolewa huku kukiwa na taarifa nyingine za vifo vya wanajeshi 13 kutoka Afrika Kusini na watatu kutoka Malawi waliouawa katika mapigano Goma. Wanajeshi hao walikuwa wamepelekwa kama sehemu ya juhudi za kudumisha amani za kikanda.

Nchi za Afrika Kusini, Malawi, na Tanzania ndizo zenye wanajeshi wanaolinda amani DRC kwa mwamvuli wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SAMDRC).


Mikutano ya dharura

Mikutano ya dharura imekuwa ikiendelea kujadili hali ya usalama nchini DRC, ikiwemo mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ulioitishwa na Mwenyekiti wake, Rais William Ruto wa Kenya.

Katika mkutano huo, wanachama wa jumuiya hiyo walihimiza usitishwaji wa mapigano na kuitaka Serikali ya DRC kushiriki mazungumzo ya amani na kundi la waasi wa M23.

Aidha, mkutano wa dharura wa Utatu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (Organ Troika) ulifanyika jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, ukilenga kutafuta suluhisho la kudumu kwa mgogoro huo.

Mkutano mwingine wa dharura ulifanyika Harare, Zimbabwe, chini ya Mwenyekiti wa SADC, Rais Emmerson Mnangagwa, ambapo alisisitiza kuwa jukumu la kulinda usalama wa raia wa DRC si hiari bali ni la kisheria kwa mujibu wa makubaliano ya wanachama wa SADC.

“Kwa bahati mbaya, tangu mkutano wetu wa mwisho, hali ya usalama DRC imezidi kuzorota, huku mashambulizi ya M23 yakigharimu maisha ya wanajeshi wetu wa amani,” alisema Rais Mnangagwa.

Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Magosi, alisisitiza kuwa wanajeshi wa SADC wamekuwepo DRC tangu mwaka 2013 wakishirikiana na vikosi vya Monusco.

Alieleza kuwa SADC itaendelea kuhimiza amani na usalama katika taifa hilo kwa mujibu wa misingi yake ya kiusalama na maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Umoja wa Mataifa kupitia baraza lake la usalama umesisitiza umuhimu wa kusitisha mapigano na kutafuta suluhisho la amani kupitia mazungumzo.

Uvamizi wa M23 mashariki mwa DRC umeendelea kusababisha vifo vya wanajeshi na raia, hali inayozua taharuki na changamoto za kibinadamu.