Prime
Chadema, ACT, NCCR, CUF kuhusu ‘Ukawa’ 2025 wasema…

Muktasari:
- Sheria ya Vyama vya Siasa ya Tanzania ya mwaka 2019, inataka makubaliano ya vyama kuunda ushirikiano (coalition) wakati wa uchaguzi mkuu, kuwasilishwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa takribani miezi mitatu kabla ya uchaguzi huo
Dar es Salaam. Matumaini ya vyama vya upinzani kuunda mseto ili kukikabili Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kama ilivyotokea mwaka 2015, yako njia panda huku baadhi wakifananisha na ngamia kupita katika tundu la sindano.
Hata hivyo, ACT-Wazalendo imesema kabla ya kuunda ushirika huo, kwanza wanapaswa kuungana kushinikiza kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi huku NCCR-Mageuzi ikikumbushia namna ilivyosalitiwa uchaguzi mkuu wa 2015.
Sheria ya Vyama vya Siasa ya Tanzania ya mwaka 2019, inataka makubaliano ya vyama kuunda ushirikiano (coalition) wakati wa uchaguzi mkuu, kuwasilishwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa takribani miezi mitatu kabla ya uchaguzi huo.
Lakini uwezekano wa uwepo wa muungano huo unaelezwa ni mdogo hasa kwa vyama vinne vikubwa vya Chadema, NCCR-Mageuzi, ACT-Wazalendo na CUF kwa kuwa, sheria inataka uamuzi huo upate baraka za mikutano yao mikuu.
Mambo matatu yametajwa kuwa huenda yakawa kikwazo cha vyama kuingia katika ushirikiano huo ambao ni uhaba wa fedha kuitisha mikutano mikuu, misimamo ya vyama na muda uliobaki kufikia ndoto hiyo.
Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alipoulizwa na Mwananchi endapo kuna uwezekano wa chama hicho kuungana na chama kingine, amesema msimamo wao utajulikana baada ya viongozi wao kutoka kwenye ‘Retreat’ (fungate).
Mnyika amesema viongozi wapya wamejifungia kwa wiki moja lakini hakuwa tayari kueleza kama watatoka na msimamo tofauti na “no reform, no election,”ambao unasema kama hakuna mageuzi ya mifumo ya kisheria, uchaguzi hautakuwepo.
Mwaka 2015, vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na National League for Democracy (NLD) vilishirikiana kupitia mwavuli wa Umoja wa Katiba Tanzania (Ukawa), ulioasisiwa katika Bunge Maalumu la Katiba lililoketi mwaka 2014.
Chini ya mwavuli huo, vyama hivyo vilimsimamisha Edward Lowassa, kupeperusha bendera ya Ukawa katika nafasi ya urais na alipata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 dhidi ya John Magufuli wa CCM aliyepata kura 8,882,932 ambazo ni sawa na asilimia 58.46.
Ujio wa Lowassa aliyetotokea CCM baada ya jina lake kukatwa, aliupa Ukawa ushindi wa viti 116 vya wabunge katika Bunge la 11 na idadi hiyo ndio kubwa kuwahi kufikiwa na upinzani tangu mfumo wa vyama vingi uanze mwaka 1992.
Katika uchaguzi huo uliohusisha majimbo 258, kati ya 262, CCM ilishinda ubunge katika majimbo 188, CUF 35 na Chadema 34 huku NCCR-Mageuzi ikipata kiti kimoja na NLD haikupata kitu, hivyo ukichanganya viti maalumu wanakuwa na viti 116.
Ni mafanikio hayo mara kadhaa yamefanya baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kutamani muungano wa vyama vya siasa ili kuikabili CCM kutokana na mazingira tete ya uchaguzi nchini tangu mwaka 2019.
Pamoja na matamanio hayo, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Andrew Dawson, amesema katika uchaguzi wa mwaka huu ni vigumu kuona vyama vikiungana kwa kuwa haviaminiani hasa kutokana na kile kilichojitokeza kwenye Ukawa 2015.
“Ukiniuliza nitakuambia hivi vyama kuungana mwaka huu ni kama ngamia kupita kwenye tundu la sindano. Hawaaminiani na kuna hisia baadhi ya vyama ni washirika wa chama tawala kwa siri siri. Hilo ni tatizo labda itokee miujiza,”amesema.
NCCR-Mageuzi wadokeza ya Ukawa
Akizungumzia na Mwananchi, makamu mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini amesema umoja ni jambo zuri na wao hawajawahi hata mara moja kupuuza mwito wa kushirikiana katika uchaguzi.
Hata hivyo, kiongozi huyo amesema uamuzi mkubwa kama huo ni lazima kushirikisha wanachama na kufanyiwa uamuzi katika vikao vya chama na kwamba, wao bado hawajawahi kufanya mjadala kama huo na kufanya maamuzi.
“Pamoja na hayo, sheria ya vyama iliyorekebishwa sasa inataka ushirikiano wowote utambuliwe na ofisi ya msajili ili kujua baada ya uchaguzi vyama vilivyoshirikiana vitapata faida gani kwenye ushirikiano huo,”amesema Selasini.
“Utakumbuka kipindi cha Ukawa kulikuwa na kusalitiana sana. Makubaliano yalikiukwa kwa kiasi kikubwa katika kata na majimbo. Hadi sasa NCCR ina maumivu ambayo hayajafutika.
“Hii ni baada ya ngome zetu kuvamiwa kinyume na makubaliano hata Jimbo la Serengeti la aliyekuwa Katibu mkuu wetu Mosena Nyambabe aliwekewa mgombea wa chama kimojawapo kilichokuwa katika umoja wa Ukawa.
“Vile vile baada ya uchaguzi chama kilichopata wabunge kilichukua kila kitu. Yaani wabunge wa viti maalumu pamoja na ruzuku.Hali hiyo ilivunja wengi moyo wa kuingia katika makubaliano kama yale ambayo yalikuwa na hila nyingi.”
Hata hivyo, Selasini amesema Tundu Lissu kwa sasa amekuwa mwenyekiti ndani ya Chadema, anaweza akaleta mabadiliko kwa kuwa tayari uongozi uliopita ulikuwa na msimamo wa kutoshirikiana na chama chochote.
“Kwa sababu hiyo, sisi tunasubiri yeyote mwenye nia au mwaliko ili tuingie katika mijadala hiyo. Vinginevyo tunawakaribisha wananchi wote wenye nia ya kuomba nafasi za uongozi kama udiwani, ubunge na urais kujitokeza,”amesisitiza Selasini.
Msimamo wa Chadema, ACT-Wazalendo, CUF
Akizungumzia hilo, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita amesema ni kiu ya chama hicho kuunda ushirikiano na vingine vya upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani 2025.
Kwa mtazamo wa chama hicho, amesema ushirika utaohitajika uanzie kwenye mjadala wa pamoja kuhusu namna ya kukabiliana na hujuma za uchaguzi akirejea chaguzi za Serikali za mitaa mwaka 2019 na 2024 pamoja na uchaguzi mkuu wa 2020.
"ACT Wazalendo inataka ushirika huu uanze na mjadala wa pamoja juu ya namna ya kukabiliana na hujuma za uchaguzi ambazo ndiyo imekuwa changamoto namba moja tunayopaswa kuitafutia majibu ya pamoja kwa umoja," amesema Mchinjita.
Katika kuonyesha utashi wa chama hicho kushirikiana, Mchinjita amesema tayari wameshaviandikia vyama vingine vya upinzani ili kutengeneza umoja huo na tayari wameshakutana na baadhi ya vyama na kufanya mazungumzo ya awali.
"Kwa vile CUF na Chadema walikuwa kwenye chaguzi za ndani, tuliona ni busara chaguzi hizo zipite kabla ya kukutana. Baada ya kumalizika kwa chaguzi hizo, tayari tumeshapokea mapendekezo ya CUF kuhusu lini tukutane,”ameeleza Mchinjita.
Kuhusu Chadema, amesema wanaendelea na mawasiliano na uongozi mpya ili watimize lengo hilo huku Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu akisema muda wa kisheria wa kuunda ushirika huo na vyama vingine kama Chadema bado upo.
“Muda unaruhusu kisheria. Kabla ya kutafakari ushirikiano, tutaanza kwanza kushirikiana kushinikiza kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi. Tumekwishaviandikia vyama vinne kuhusu hili ikiwamo Chadema,” amesema Shaibu.
Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Katibu Mkuu wa Chadema, Mnyika amesema:“Tulishatangaza kujifungia kwa wiki moja kwenye retreat na uongozi mpya kujipanga. Nitafute tukishatoka kwenye retreat. Tutakuwa na msimamo”
Kama ilivyo kwa Chadema, Katibu Mkuu wa CUF, Husna Mohamed Abdallah amesema uamuzi wa kushirikiana utatokana na vikao vya chama hicho na kueleza mwezi huu, Kamati Tendaji ya chama hicho inatarajia kuketi.
Husna amesema pamoja na mambo mengine itajadili suala la kushirikiana na kuongeza kusema kuwa, “baada ya kikao hicho, nitakuwa na jibu zuri kuhusu kushirikiana na vyama vingine vya upinzani au laa."
Mseto wa vyama ni nini
Profesa Catherine Ndungo wa Idara ya Kiswahili katika chuo kikuu cha Kenyatta, Nairobi Kenya katika andiko lake la “sheria ya vyama vya siasa, toleo la umma,” anasema vyama vinaweza kuungana ili kupata kura zaidi wakati wa uchaguzi.
“Mseto ni muungano wa vyama viwili au zaidi vya kisiasa ambavyo vinaundwa kwa lengo la kufikia azimio la pamoja na ambao unatawaliwa na mkataba ambao umeandikwa na kuwasilishwa kuwa Msajili,”anasema katika andiko hilo.
“Mseto ni tofauti na vyama kuungana kwa vile vyama mbali na kushirikiana vinabakia na utambulisho wa kisheria na huwa na viongozi wake, katiba yake, wanachama wake na kadhalika.”
Profesa Catherine Ndungo amesema malengo ya miseto ni kuwa na miungano ambayo itawasaidia kutimiza malengo ya pamoja kama vile kushinda katika uchaguzi na kuunda Serikali ama kuimarisha jukumu lao kama wapinzani.