Lucas aliyetikisa ubunifu nembo ya ‘Made in Tanzania’

Muktasari:
- Nembo ya ‘Made in Tanzania’ ina inatajwa kuwa hatua muhimu ya maendeleo nchini na itaitambulisha Tanzania kimataifa kama Taifa lenye bidhaa zenye ubora, ubunifu na fahari ya Kiafrika.
Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikijivunia kuzindua rasmi nembo ya Made in Tanzania kama utambulisho wa bidhaa zinazozalishwa kwa Lucas Haule ni jambo ambalo halitakuja kusauhaulika maishani mwake.
Hiyo ni baada ya kijana huyo wa miaka 24 kuibuka kidedea katika shidano na kuandaa nembo hizo ambayo itawekwa katika kila bidhaa inayozalishwa nchini kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.
Lucas amewashinda wengine 88 ambao waliingia katika mchuano huo huku akipita katika hatua mbalimbali za mchujo kabla ya kutangazwa kuwa mshindi.
Haule ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Dodoma, aliibuka mshindi wa kwanza katika shindano hilo lililoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa ajili ya kubuni nembo ya “Made in Tanzania” (Imetengenezwa Tanzania).
Shindano hilo lilikuwa sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuhamasisha bidhaa zinazozalishwa nchini kupatiwa utambulisho mmoja kwa lengo la kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, viwanda, utalii na huduma.
“Niliiona tangazo kwenye mtandao wa Instagram lakini nilikuwa na mashaka kama nina nafasi,” amesema Haule katika mahojiano aliyofanya na Mwananchi.
Amesema mashaka aliyokuwa nayo yalitokana na kutowahi kuupima ujuzi wake katika mashindano yoyote ya kutengeneza nembo kwa wakati huo jambo ambalo lilimfanya kuweka nia na kumfanya ajipe moyo kuwa anajaribu.
“Mimi nasoma shahada ya Health Infirmation Science lakini huwa nafanya ubunifu wa nembo kama kitu ninachokipenda, nilipoona tangazo hili nilianza kujifunza kubuni nembo inayoweza kushindana kupitia masomo ya mtandaoni tu. Hata hivyo, nilihisi ninapaswa kujaribu na kufanya majaribio zaidi wakati nafanya hili hivyo sikuwa na uhakika,” amesema.
Kwa mujibu wa TanTrade, shindano hilo lilipokea mifano ya nembo 88 kutoka sehemu mbalimbali nchini ambapo washiriki 10 waliingia fainali na walipewa msaada wa kitaalamu kuboresha kazi zao.
Baadaye nembo tatu bora zilichaguliwa na kupelekwa kwa umma ili ziweze kupigiwa kura, ambapo kazi ya Haule ilipata kura nyingi zaidi.
Nembo iliyoshinda ilizinduliwa rasmi wakati wa Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), yanayojulikana pia kama Sabasaba na Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi.
Uzinduzi huo uliambatana na Siku ya Made in Tanzania, tukio la kitaifa linaloangazia uzalishaji na ubunifu wa ndani.
Alipokuwa akizindua nembo hiyo, Dk Mwinyi alisema Made in Tanzania iwe chachu ya kukuza uzalendo wa kibiashara na iwe chachu ya kila mtanzania kutumia bidhaa za ndani.
“Nitoe wito kwa Watanzania wenzangu kupenda na kuthamini bidhaa zetu ili kuzidi kuimarisha biashara na viwanda vyetu vya ndani na kuchangia ukuaji wa uchumi wetu,” alisema Dk Mwinyi.
Mafanikio ya Haule yamevutia umma siyo tu kwa kwa ubunifu wake bali pia kwa safari yake isiyotarajiwa iliyomfikisha kwenye kutambulika kitaifa.
Bila mafunzo rasmi ya ubunifu na usanifu wa nembo, alianza kujifunza mwenyewe kupitia vyanzo vya bure mtandaoni na jamii za mitandao ya kijamii.
“Ninajivunia kazi yangu kuwakilisha Tanzania kimataifa, hii inanipa ujasiri kuwa vijana, hata bila msingi rasmi wanaweza kuchangia kwa maana endapo watapewa jukwaa na imenioa nguvi ya kujaribu na kuona kila kitu kinawezekana ukiweka nia,” amesema.
Haule anatarajia kuhitimu mwaka huu sasa analenga kuanzisha kampuni ya ushauri wa ubunifu ambayo itakuwa ikihusika na vitu mbalimbali.
“Si suala la nembo pekee, pia kusimulia hadithi ambazo watu wanaweza kuzielewa na kuzigusa,” amesema.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema mpango wa kuwa na nembo ya utambulisho kwa bidhaa za Tanzania unalenga kujenga imani ya watumiaji na kuongeza mwonekano wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.
“Nembo hii si alama tu, inaakisi maono na uwezo wa Watanzania, wakiwemo vijana wetu. Ni sehemu ya jitihada za kukuza viwanda na kujitegemea kiuchumi,” amesema.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa TanTrade, Lulu Mkudde amesema chapa hiyo itawapa wauzaji wa nje jukwaa la pamoja na kupunguza gharama za masoko kwa kuunganisha bidhaa chini ya nembo moja inayotambulika na kuaminiwa.
“Lengo letu ni kuongeza utambulisho wa kimataifa wa bidhaa za Tanzania na kuboresha nafasi yake katika masoko,” amesema Mkudde. “Tunaamini nembo hii itakuwa rasilimali muhimu kwa wazalishaji wakubwa na wadogo,”amesema.