Lissu: Tusipopata Katiba Mpya kabla ya Uchaguzi tunyamaze milele

Makamu Mwenyekiti Chadema, Tundu Lissu akihutubia hadhara iliyojitokeza kwenye uzinduzi wa Operesheni +255 Katiba Mpya mkoani Tabora leo. Picha na Mgongo Kaitira.

Muktasari:

  • Chadema inaendelea na Operesheni +255 Katiba Mpya yenye lengo la kushinikiza upatikanaji wa Katiba Mpya kabla ya chaguzi zijazo za 2024 na 2025.

Tabora. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu amewataka watanzania kuungana na Chama hicho katika madai ya kupata Katiba Mpya kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (2024) na Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Lissu ametahadharisha kuwa Katiba Mpya isipopatikana kabla uchaguzi huo basi Watanzania wanyamaze huku wakitarajia kuona matendo yaliyotokea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2019 na Uchaguzi Mkuu wa 2020 yanajirudia.

Mwanasiasa huyo mkongwe ametoa tahadhari hiyo leo Mei 27, 2023 alipokuwa akihutubia maelfu ya wakazi wa mkoa wa Tabora waliojitokeza kushuhudia uzinduzi wa Operesheni +255 Katiba Mpya uliofanyika katika viwanja vya Town School mkoani humo.

"Tunahitaji kupambana na kulianzisha nchi nzima tumkabili Rais Samia, tumwambie bila Katiba Mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu hakitaeleweka. Tukikubali kwenda kwenye uchaguzi kama ilivyokuwa mwaka 2019, na tunyamaze kimya milele," amesema Lissu

Huku, akilaani matukio ya baadhi ya askari na wahifadhi wanyamapori nchini kuwashambulia raia na kutwaa mifugo yao inapoingia hifadhini, Lissu amesema binadamu hawezi kulinganishwa thamani na wanyama hivyo kuna haja ya sera na sheria za uhifadhi kuangaliwa upya.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amesisitiza kuwa ili changamoto za wananchi ikiwemo umaskini na ugumu wa maisha zitatuliwe nchi inatakiwa kuongozwa kwa kuzingatia misingi ya Uhuru, Haki, Demokrasia na Maendeleo ya Watu.

"Ndiyo maana Chadema tunasisitiza kuhusu madai ya Katiba Mpya ambayo itakuwa mwarobaini wa kupata misingi hiyo ambayo haitekelezwi na Serikali ya CCM. Tukipata Katiba Mpya tutafanikiwa kuing'oa CCM madarakani," amesema Mbowe

Naye, Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) Catherine Ruge amesema jukumu ya kubadilisha mfumo wa utawala kutoka katika mikono ya CCM halitafanikiwa kwa kufanywa na viongozi wa Chadema pekee badala yake ni mashirikiano ya wananchi na Viongozi wa chama hicho.

Chadema inaendelea na Operesheni +255 Katiba Mpya katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambapo leo imefanya mikutano ya hadhara katika Kata zaidi ya sita za mkoa wa Tabora huku kesho mikutano ya chama hicho ikitarajiwa kufanyika Wilayani Nzega mkoani humo.