Kwa nini unafuta picha za 'Ex' wako?

Muktasari:
- Licha ya kumbukumbu za matukio na mwenza wako kuongeza chachu katika huba, umewahi kujiuliza kwanini yanapofika ukomo zinageuka kuwa shubiri?
Dar es Salaam. Unakumbuka mlivyoachana na mpenzi wako ulifanya nini kumsahau? Kilikusaidiaje? Utafanya tena ikitokea kwa uliyenaye sasa?
Maswali haya yanaakisi hatua zinazochukuliwa na wengi baada ya kutengana au kugombana na wenza wao.
Kufuta kumbukumbu za matukio ya furaha zilizohifadhiwa (picha), jumbe fupi za mahaba mlizowahi kutumiana na hata kuziba mianya ya mawasiliano (block) ni baadhi ya hatua zinazochukuliwa.
Pamoja na ukweli kwamba si wote wanaofikia maamuzi hayo, lakini tamati ya mahusiano mengi huangukia huko.
Mtazamo wa vijana kuhusu hatua hiyo, ni kujipa afua ya maumivu ya moyo yatakayotokana na kuzikumbuka enzi za furaha, kama anavyoeleza Dickson Simba kijana kutoka Dar es Salaam.
"Mlipiga picha kwa furaha na mapenzi, mlikuwa mkiangalia pamoja mnacheka, sasa hayo yote hayapo kwanini ubaki nazo, unajiumiza tu" anasema.
Simba anasema ni wachache wasioumizwa na kuachwa au kuachana, akisisitiza kufuta kumbukumbu zinazofutika ni hatua moja ya kujiepusha na maumivu.
Anachokisema Simba hakitofautiani na Rukia Masoud, anayesema mbinu pekee ya kumpunguzia maumivu anapoachwa au kumuacha anayempenda ni kufuta picha zake na vingine vinavyowezekana.
"Hii inakupunguzia sio kukuondolea moja kwa moja, maana mkiachana sio kwamba siku hiyo hiyo utasahau, yale yale uliyoyafuta kwenye simu kichwani unayakumbuka, mapenzi haya jamani?," anaeleza na kuangua kicheko.
Kumbe sio kupunguza maumivu tu, uamuzi wa kufuta kumbukumbu unafungua milango ya kukaribisha penzi jipya, kama anavyofafanua Esther Milanzi mkazi wa Dar es Salaam.
"Ukibaki nazo utamkumbuka yeye tu, lakini ukifuta unaipa nafsi nafasi ya kutafakari mengine, hapo unakuwa na uwezo wa kuanzisha penzi jipya," anasema.
Wanaoshangaza ni wale wanaofuta kumbukumbu kisha wanarudiana, jambo linaloelezwa na Esther kuwa uamuzi ulichagizwa na hasira na sio ukomo wa penzi.
"Wengine mkigombana tu, mara kakublock, mara kafuta namba, mara kafuta picha zote, hizi ni hasira sio kwamba anakuwa amemaliza mapenzi, mimi nikifuta ujue moyoni haurudi Baba," anaeleza kwa msisitizo.
Mtazamo wa kisaikolojia
Kwa mtazamo wa kisaikolojia, uamuzi huo aghalabu hufanya katika wiki ya kwanza ya ama ugomvi au malumbano miongoni mwa wenza, inaelezwa na Mhadhiri wa Saikolojia, Dk Chris Mauki.
Hata hivyo, anasema uamuzi huo huchagizwa na hasira, jambo ambalo ni matokeo ya kihisia baada ya kukwazwa.
"Hii inahusisha kufuta picha mtandaoni, wengine kuvuja pete, mara nyingi inafanyika kwenye kipindi cha wiki moja au mbili baada ya kuachana," anasema.
Ingawa wengi hufanya hivyo wakidhani itawasaidia kusahau, Dk Mauki anasema uhalisia ni kinyume chake uamuzi huo hauna msaada wowote katika kukusahaulisha.
"Picha na taswira kubwa haibaki kwenye mtandao bali ni akili yako, utafuta kila kitu lakini utajikuta bado huyo mtu anakutesa na unamkumbuka," anaeleza.
Baada ya wiki hizo na hasira kupungua, Dk Mauki anasema aliyefanya jambo hilo hujiona mjinga ingawa huwa hawaelezi kwamba wanajutia.
Nini cha kufanya baada ya kuachwa/ kuachana
Katika wiki ya kwanza na pili baada ya ugomvi na mwenza, Dk Mauki anashauri vema kuvumilia bila kuchukua uamuzi wowote ili kujipa nafasi ya kuamua kwa busara.
"Katika kipindi hicho usifanye maamuzi yoyote kwa sababu kuna uwezekano wa kuyajutia baadaye," anafafanua.
Jonas Kinanda ni mhadhiri msaidizi wa idara ya saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasema uamuzi wa kufuta au kutofuta kumbukumbu za Ex wako, anasema yatokane na tathmini ya yalivyokuwa mahusiano, akisisitiza: “Kama zikibaki zitakuumiza futa, kama zinakufariji acha.”