KUTOKA MAHAKAMANI: Aliyehukumiwa kwa kumuua mvuvi mwenzake aachiwa huru

Muktasari:
- Mwinura Fuguti alihukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumuua mvuvi mwenzake
Arusha. Mahakama ya Rufani imemuachia huru Mwinura Fuguti aliyekuwa amehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya kumuua mvuvi mwenzake, Ibrahim Magesa.
Mwinura alihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama Kuu Kanda ya Musoma Septemba 22, 2020, kutokana na kesi ya mauaji iliyokuwa ikimkabili.
Katika kesi hiyo, Mwinura alidaiwa kushirikiana na mwenzake kumpiga marehemu kichwani kwa kutumia kasia, kummwagia maji ya moto kisha kuutupa mwili wake ziwani.
Hukumu hiyo ya rufaa iliyomuachia huru imetolewa Julai 18, 2024, na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani wakiongozwa na Jaji Lugano Mwandambo, Lilian Mashaka na Gerson Mdemu.
Majaji hao walifikia uamuzi huo baada ya kupitia mwenendo wa kesi na kusikiliza hoja za pande zote mbili na kubaini dosari kadhaa wakati wa usikilizwaji, ikiwamo ushahidi wa utambuzi wa mrufani katika eneo la tukio kuwa dhaifu.
Ilivyokuwa
Katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mwinura alipandishwa kizimbani kwa mauaji ya mvuvi ya Ibrahim Magesa, Agosti 21, 2017 katika Kijiji cha Kiriba, wilayani Butiama.
Shahidi wa kwanza alidai kuwa Agosti 20, mwaka huo, Magesa aliporejea kambini kutoka baa, alikuwa akipiga kelele akidai chakula.
Wenzake, akiwamo Mwinura, walimtaka aache kelele vinginevyo angepigwa.
Imeelezwa kuwa, Magesa alitii na kulala, lakini saa saba usiku alipiga kelele tena akiomba chakula.
Shahidi huyo alidai Mwinura na mwenzake walimpiga kichwani na kuutupa mwili wake ziwani.
Asubuhi ya Agosti 21, 2014, shahidi huyo alidai alienda kutoa taarifa kwa mama wa Magesa (shahidi wa pili) na kuwataja wahusika wa tukio hilo.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama, shahidi wa kwanza alidai kuwatambua Mwinura na mwenzake kupitia usaidizi wa mwanga wa mbalamwezi, na waliripoti tukio hilo Kituo cha Polisi Mugango.
Mwinura alikamatwa katika Kijiji cha Busekela mnamo Novemba 20, 2014, na kushtakiwa kwa mauaji.
Alipokutwa na hatia, alihukumiwa kunyongwa hadi kufa.
Rufaa ilivyokatwa
Katika rufaa hiyo, hoja zilizowasilishwa ni kuwa Jaji wa Mahakama Kuu alikosea kisheria kwa kushindwa kufuata utaratibu mzuri wa sheria kuhusu ushirikishwaji wa wazee wa baraza.
Katika rufaa hiyo ilidaiwa kuwa jaji huyo alishindwa kuwaeleza wazee hao wa baraza mambo muhimu ya sheria kusababisha mchakato mzima kuwa batili.
Sababu nyingine ni Jaji kukosea kisheria kumtia hatiani na kumhukumu Mwinura huku ushahidi wa upande wa mashtaka ukiwa na upungufu mkubwa, ukiwamo ushahidi wa shahidi wa kwanza kuhusu utambuzi kuwa dhaifu.
Pia, upande wa mashtaka ulishindwa kumwita mpelelezi wa polisi ambaye alikuwa shahidi muhimu katika kesi hiyo.
Katika rufaa hiyo, Mwinura aliwakilishwa na Wakili Baraka Mbwilo, huku mjibu rufaa akiwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Revina Tibilengwa. Wakili Mbwilo alieleza kuwa Jaji hakuzingatia sheria kuhusu ushiriki wa wazee wa baraza, ikiwamo kutowaeleza wajibu wao na baadaye katika majumuisho aliomba majaji hao kubatilisha mwenendo wa kesi na hukumu.
Uamuzi Majaji
Jaji Mdemu alieleza kuwa, baada ya kufungwa kesi kwa upande wa mashtaka na utetezi, Jaji alipaswa kufanya majumuisho kwa kuwaelekeza wazee wa baraza mambo muhimu ya kisheria yanayohusiana na kesi kabla ya kuwahitaji kutoa maoni yao.
Kutokueleza majukumu ya wazee wa baraza ni ukiukwaji wa kifungu cha 265 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, hivyo kufanya hukumu iliyotolewa kwa Mwinura kuwa batili.
Kuhusu hoja ya utambuzi, Jaji Mdemu alieleza kuwa uaminifu wa ushahidi wa shahidi wa kwanza juu ya utambuzi ulikuwa dhaifu sana kuweza kufanyiwa kazi na Jaji wa Mahakama Kuu, kwa sababu mazingira yalikuwa na utambulisho usio sahihi.
“Kwa kuzingatia yaliyotangulia, tunairuhusu rufaa na hukumu ya kosa la mauaji iliyotolewa hapo inawekwa kando, tunaamuru kuachiliwa mara moja kwa mrufani, ikiwa hajashikiliwa kihalali kwa sababu zingine,” alihitimisha Jaji huyo.