Kujiamini kidogo, ugumu wa maisha vichocheo vya tatizo la afya ya akili

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Africa Academy for Public Health (AAPH) Mary Sando akizungumza katika Mkutano wa kutoa Mrejesho na Taarifa zilizotokana na mradi wa Afya ya Akili kwa Vijana 'Being Mental Health Initiative' jijini Dar es Salaam leo. Picha na Sunday George

Kama una changamoto ya kushindwa kujiamini kwa kiwango kinachotakiwa na unakabiliwa na hali ngumu ya maisha, basi uko kwenye hatari ya kuwa ama kupatwa na tatizo la afya ya akili.

Hayo ni miongoni mwa mambo 12 yaliyotajwa kuwa vichocheo vilivyobainika kuwakabili vijana wanasumbuliwa na tatizo la afya ya akili.

Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Mei 2, 2024 wakati wa uwasilishwaji wa ripoti ya utafiti ya Shirika la Africa Academy for Public Health (AAPH) jijini Dar es Salaam.
Katika utafiti huo wa mwaka mmoja, imebainika kuwa yapo mambo 12 yanayochochea tatizo hilo ambalo kwa sasa takwimu zinaonyesha asilimia 33 ya Watanzania wanakabiliana nalo.

Vichocheo vingine vilivyotajwa ni pamoja na unyanyapaa ambao unatajwa kuwakwamisha vijana wengi kutafuta msaada wa kitaalam wanapopata changamoto ya afya ya akili.

Matumizi ya dawa za kulevya, kuishi na VVU, unyanyasaji, shinikizo la marafiki, malezi mabaya, imani za kitamaduni, ukuaji wa miji, mlipuko wa magonjwa kama COVID-19, na mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa vichocheo hivyo hatari vinavyosababisha tatizo hilo kushika kasi.

Utafiti huo unatolewa ikiwa ni wiki chache tangu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kubainisha upungufu mkubwa katika maeneo 12 katika utoaji wa huduma kwenye jamii, ikiwemo ongezeko la idadi ya wagonjwa na vifo vinavyotokana na matatizo ya afya ya akili.

Miongoni mwa upungufu huo ni pamoja na huduma duni ikiwemo ugunduzi katika ngazi ya jamii, rasilimali fedha, uhaba wa watumishi na upungufu wa usambazaji dawa.

Kwa mujibu Ripoti ya Ukaguzi wa Ufanisi Kuhusu Upatikanaji wa Huduma za Afya ya Akili iliyotolewa na CAG kwa mwaka 2022/2023, mambo hayo yanaongeza hofu ya kushughulikia afya ya akili kwa wananchi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa AAPH, Dk Mary Mwanyika Sando amesema utafiti ulilenga kundi la vijana kuanzia miaka 10 hadi 24 uliofanyika kupitia mradi wa afya ya akili kwa vijana ujulikanao kama 'Being Mental Health Initiative.'

Amesema unyanyapaa kuhusu afya ya akili ni jambo linalopaswa kupewa umuhimu nchini kutokana na imani za kitamaduni, uelewa mdogo katika jamii, na upatikanaji mdogo wa huduma za afya ya akili.

"Imani hizi ni pamoja na dhana kwamba watu wenye changamoto za afya ya akili kuwa "wamerogwa" na wanahitaji kutibiwa na waganga wa jadi.

"Katika utafiti wetu hili limejitokeza zaidi katika maeneo ya vijijini ambapo imani na mila nyingi za jadi bado zipo kwa kiasi kikubwa," amesema.

Kuhusu changamoto hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospital ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dk Paul Sarea amesema changamoto ya afya ya akili inaanzia ngazi ya familia na malezi yakichukua nafasi kubwa.

"Mama mjamzito anapokuwa na changamoto za afya ya akili kipindi cha mimba, hata mtoto atakayezaliwa hatokuwa sawa, pia malezi mabovu ni moja ya vitu vinavyosababisha tatizo hili nchini.

"Kwenye ngazi ya familia, tunaangalia watoto wanalelewa na nani, mazingira yapi na mambo kama hayo, lakini kwa muda mrefu hakukuwa na watu wa kulisemea tatizo hili, wachache ikiwamo AAPH wanafanya, tukiweka miongozo thabiti bila shaka tutapunguza tatizo," amesema.

Naye Dk Innocent Yusufu, ambaye ni Mtafiti Mwandamizi wa Program ya AAPH na Mratibu wa Mradi wa Being - Tanzania na Ghana, amesema lengo ni kupunguza unyanyapaa na kuendeleza ushirikiano wa wadau mbalimbali.

Amesema, AAPH inayoshirikiana na Chuo Kikuu cha Harvard na washirika wengi nchini Tanzania kama Wizara ya Afya, taasisi za elimu ya juu na utafiti, pamoja na mashirika ya ndani na kimataifa yenye malengo kama hayo inatoa ari ya kuendeleza juhudi za pamoja ili kuimairisha afya ya akili kwa vijana na kutatua changamoto wanazozipitia.