Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuapa kwa kina Mdee kulivyowaamsha Mbowe, Mnyika

Jana, tuliwaletea utangulizi wa hukumu ya Jaji Cyprian Mkeha katika kesi iliyofunguliwa na Halima Mde na wenzake 18 ambayo ilibatilisha uamuzi wa Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), lililothibitisha kuvuliwa uanachama wabunge wao wa viti maalumu.

Jaji Mkeha wa Mahakama Kuu ya Tanzania alitoa hukumu hiyo yenye kurasa 79 Desemba 14, 2023.

Kamati Kuu ya Chadema, iliwavua uanachama kwa madai ya kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu wakati kamati hiyo ilikuwa haijafanya uteuzi wowote wa nafasi hizo kwa mujibu wa Ibara ya 7.7.16(a) ya Katiba ya chama hicho.

Mdee na wenzake, walivuliwa uanachama wa chama hicho na Kamati Kuu ya Chadema, Novemba 27,2020 na kukata rufaa baraza kuu la chama hicho ambalo liliketi Mei 11, 2022 kusikiliza rufaa na likabariki uamuzi wa kamati kuu.

Hukumu hiyo ya Jaji Mkeha imekuwa na maoni na tafsiri tofauti miongoni mwa baadhi ya viongozi wa Chadema, wanachama na wafuasi wa chama hicho na kwa msingi huo, tunawaletea kwa usahihi nini hasa kilichomo katika hukumu.

Leo, tunakuletea kwa undani nini hasa kilichopo ndani ya viapo vya akina Mdee na namna walivyomgusa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.


Kiapo kinavyosema

Jaji alisema kulingana na maelezo ya pamoja au joint statement ya waleta maombi, hoja zinazobeba maombi yao ni kwamba baada ya Mdee na wenzake kula kiapo, Novemba 25, 2020, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika alitoa taarifa kwa umma.

Katika taarifa hiyo, Mnyika alilaani kitendo hicho akisema kuapishwa kwao kulikiuka maelekezo ya chama ya kutotambua Uchaguzi Mkuu 2020 na alialika umma upendekeze wachukuliwe hatua gani.

Kwamba kupitia tangazo hilo la umma na kwa njia ya Whatsapp, katibu mkuu huyo aliwapa wito waleta maombi kufika mbele ya kamati kuu Novemba 27, 2020.

Jaji alisema kulingana na waombaji, taarifa kwa umma iliibua hasira kubwa kutoka kwa wafuasi wa Chadema ambapo baadhi waliapa kuwashambulia waleta maombi watakapofika mbele ya kikao cha nidhamu cha Kamati Kuu ya Chadema.

Kwa sababu ya kitisho cha usalama, kila mmoja aliomba kikao kiahirishwe kwanza hali itulie na pia kuhakikishiwa usalama wao kabla ya kuamua kuhudhuria kikao hicho kilichokuwa kimepangwa kufanyika Novemba 27, 2020.

Jaji alisema maelezo hayo ya pamoja ya waombaji, yanaonyesha zaidi kuwa waombaji hao hawakuwa wamepewa mashtaka kama inavyotakiwa na Katiba ya Chadema na kwa mujibu wa taratibu za ndani za kushughulikia nidhamu.

Hata hivyo, walieleza kamati kuu iliamua kufanya kikao bila waombaji kuwepo, wakati huo wakiwa bado wako Dodoma, licha ya kupewa udhuru na pia kamati kuu ilifanyia kazi uvumi na kuongeza madai mapya ambayo hatakuwepo.

Walieleza pia kuwa kikao hicho cha kamati kuu kilichanyika kwa ufupi kilikiuka kabisa kanuni za mjibu maombi wa kwanza yaani Chadema, katika kushughulikia masuala ya nidhamu na kufikia hitimisho la kuwafukuza uanachama.


Haki ya kusikilizwa

Jaji alisema waombaji waliendelea kueleza kuwa baada ya kutoridhishwa na uamuzi wwa kamati kuu, walikata rufaa katika baraza kuu, ambapo viongozi wa juu walioendesha kikao cha kamati kuu ndio walioendesha baraza kuu.

Viongozi hao walitoa kauli mbaya dhidi ya Mdee na wenzake wakati rufaa ikisubiri kusikilizwa na baadhi wakiapa kula sahani moja na waombaji hao.

Pia wajibu maombi walifanya kikao bila kuzingatia kanuni za kushughulikia masuala ya nidhamu kwa mujibu wa Katiba ya Chadema na hivyo kuwanyima waleta maombi haki ya kusikilizwa na kukosa uamuzi usio na upendeleo.

Ushahidi ambao waleta maombi waliuegemea unapatikana katika viapo vyao, kiapo cha pamoja cha kujibu kiapo cha mjibu maombi wa kwanza na majibu ya baadhi ya wadhamini waliofika kortini na kuulizwa maswali ya dodoso.


Walivyobatizwa Covid-19

Jaji alisema waleta maombi katika viapo vyao walieleza kuwa katika kikao na wanahabari cha Novemba 25, 2020, katibu mkuu wa Chadema alidai waleta maombi waligushi nyaraka na walikuwa ni wasaliti wa chama hicho.

Katika viapo hivyo, wanaeleza kuwa Novemba 27, 2020, wanachama wa Chadema waliandamana hadi makao makuu ya chama na kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kilikuwa kifanyike na hapo wakabatizwa jina la Covid-19.

Walieleza kuwa mmoja wa wanachama hao, Shaaban Othman alionekana kwenye televisheni akiwa amebeba bango lenye ujumbe “Kamati Kuu, fukuzeni hao Covid 19”, ambapo walikabidhi flash ikionyesha maandamano hayo ya wafuasi.

Wanasema katika viapo vyao hivyo kuwa uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema wya Novemba 27, 2020 wa kuwafukuza uanachama, uliathiri nafasi yao kama wabunge wa viti maalum na haki yao ya kikatiba ya kujumuika katika masuala ya kijamii.

Kwamba baada ya uamuzi huo, walikata rufaa baraza kuu kupinga utaratibu wote wa uliotumika hadi kamati kuu kufikia uamuzi wa kuwafukuza uanachama.


Walivyomgusa Mbowe

Wanaeleza katika viapo vyao kuwa katika rufaa yao kwenda baraza kuu, walilitaka kupitia mchakato mzima uliotumiwa na kamati kuu hadi kufikia uamuzi wa kuwafukuza uanachama na kwamba hawakusikilizwa.



Katika viapo hivyo, walisema Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe ambaye ni mjumbe wa kamati kuu na hapo hapo baraza kuu, alitoa matamshi mbalimbali kwa umma kuunga mkono uamuzi huo wa kamati kuu.

Wakimnukuu Mbowe walisema alitamka maneno “Spika anajua.Wanajua wabunge hawa wamekwishafukuzwa na chama hiki. Inasemekana ooh, baraza kuu limepangwa, baraza kuu letu lipo tarehe 25 mwezi wa nne.

“Kama kuna rufaa zao tutawaona kwenye baraza kuu. Ishu sio kukubali wabunge 19, tunapokataa wabunge 19, tunakataa ukiukwaji wa sheria za nchi, forgery (kugushi) iliyofanyika katika taifa,” walimnukuu Mbowe aliyeongeza kusema:-

“Nakwenda mimi kuidhinisha ubatili wa namna hiyo? Hakuna kitu kama hicho na hakitatokea kwenye Chadema ambayo sisi tunaiongoza na wenzangu hapa. Tunasimama upright (wima) Chadema haijawahi kuteua wabunge 19.”


Tulitakiwa kuomba radhi, sio rufaa kusikilizwa

Mdee na wenzake kwa mujibu wa viapo vyao, walisema walialikwa katika mkutano huo wa baraza kuu uliofanyika Mlimani City Jijini Dar es Salaam Mei 11, 2022 na walihudhuria, lakini nafasi pekee yaliyopewa ni kuomba radhi.

Akiendelea kunukuu kilichomo katika viapo hivyo, Jaji alisema waleta maombi wanasema Mei 11,2022 baraza kuu lilithibitisha uamuzi wa kamati kuu bila kuwasikiliza waombaji na kuendelea kuwafukuza uanachama wa Chadema.

Walisema wajumbe wa kamati kuu waliopitisha uamuzi wa kuwafukuza Novemba 27, 2020 akiwemo mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, John Mnyika ndio walikuwa pia sehemu ya wajumbe wa baraza kuu lililoketi Mei 11.

Mdee na wenzake katika viapo hivyo, wanasema baadaye Katibu Mkuu Chadema walimwandikia barua Spika wa Bunge akimjulisha uamuzi wa baraza kuu uliofikiwa Mei 11 ambao ulithibitisha kufukuzwa uanachama Mdee na wenzake.

Kwamba mjibu maombi wa pili ambaye ni NEC angetamka kuwa nafasi hizo 19 za viti maalumu ziko wazi baada ya NEC kupokea taarifa kutoka kwa Spika, akifanyia kazi uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema uliotolewa Mei 11, 2022.

Mwisho waombaji wakasema Kamati Kuu na Baraza Kuu la Chadema, wamekabidhiwa wajibu wa umma wakati wanashughulikia haki za waleta maombi na lazima utimizwe kwa busara na uzingatie haki ya asili au natural justice.

Kwa hiyo wanasema baada ya kupita hatua zote za kudai haki ndani ya chama, na hakuna mlango mwingine na wakiwa bado hawaridhiki na uamuzi wa baraza kuu uliothibitisha ule wa kamati kuu, wameamua kufungua maombi hayo.

Itaendelea katika gazeti letu na mitandao yetu ya kijamii kesho.