Kozi zenye fursa kwa wahitimu

Baadhi ya wahitimu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam wakiwa kwenye sherehe ya mahafali ya 46 ya chuo hicho. Picha na maktaba.
Muktasari:
- Nisome fani gani itakayoniwezesha kujiajiri au kuajiriwa mara nimalizapo masomo? hili ndilo swali kubwa lililopo kwenye jamii husasan kwa wanaotaka kuendelea na masomo ya juu.
Dar es Salaam. Nisome fani gani itakayoniwezesha kujiajiri au kuajiriwa mara nimalizapo masomo? hili ndilo swali kubwa lililopo kwenye jamii husasan kwa wanaotaka kuendelea na masomo ya juu.
Swali hili ndilo linalozunguka vichwani mwa baadhi ya wahitimu wa kidato cha sita na wengineo waliopo katika mchakato wa kujiunga na masomo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2022/23, wanazuoni wa kada mbalimbali wametoa mwelekeo wa taaluma zinazopaswa kuchangamkiwa kwa kuangalia vipaumbele vya nchi na changamoto zilizopo.
Fani zinazohusiana na sekta za viwanda, uwekezaji katika nishati ya gesi, kilimo, afya na lugha ya Kiswahili ni miongoni zinazotajwa kuwa na fursa zaidi.
Ushauri huo unatolewa kipindi ambacho Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua dirisha la udahili kuanzia juzi hadi Agosti 5 mwaka huu kwa mwaka wa masomo ujao.
TCU imefungua dirisha hilo ikiwa siku chache tangu Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) kutangaza matokeo ya kidato cha sita uliofanyika Mei mwaka huu.
Katika matokeo hayo, watahiniwa 93,136 sawa na asilimia 98.97 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo wamefaulu.
Wasichana waliofaulu ni 40,907 sawa na asilimia 99.51 wakati wavulana waliofaulu ni 52,229 sawa na asilimia 98.55. Mwaka 2021 watahiniwa waliofaulu walikuwa 87,043 sawa na asilimia 99.06.
Wakati TCU ikifungua dirisha hilo la udahili, Mwananchi limezungumza na wanazuoni mbalimbali na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) wametoa ushauri wao kwa wazazi, walezi na wanafunzi wenyewe kipi wakiangazie.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Suzanne Ndomba –Doran alisema kwa sasa Tanzania ipo kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda ambapo teknolojia inabadilika kwa kasi.
Alisema viwanda na sehemu nyingi za kazi zitahitaji vijana wenye ujuzi utakaoenda na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.
“Vilevile, ‘data’ ndiyo bidhaa muhimu kwa sasa. Wazungu wanasema ‘Data is the new oil’. Kwa hiyo vijana wenye ujuzi wa kukusanya na kuchakata data wana fursa nyingi sio tu katika soko la ajira la ndani lakini pia nchi jirani tulizo nazo kwenye ushirikiano ikiwemo Kenya, Rwanda, Uganda na kwingineko,” alisema.
Alizitaja kozi muhimu za kosoma kuwa ni zile zenye kuandaa vijana kupata ujuzi kwenye masuala ya sayansi na teknolojia ikiwemo masuala ya takwimu, biashara mtandao na maeneo mengine.
“Tanzania tumeanza kuwekeza kwenye nishati kama mafuta na gesi. Hivyo kuna haja ya kujenga rasilimali watu wenye ujuzi katika haya maeneo ya uhandisi.
Wanachokieleza ATE kinaungwa mkono na Dk Zena Mabeyo wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, aliyesema uchaguzi wa fani uendane na vipaumbele vya taifa husika na changamoto zilizopo.
Alisema kwa Tanzania kipaumbele ni uchumi wa viwanda na uwekezaji katika gesi, hivyo mwanafunzi atakayeingia chuoni sasa anapaswa kuchagua taaluma inayoendana na vipaumbele hivyo.
Uhaba wa wataalamu wabobezi katika sekta ya afya, alisema ni jambo jingine linaloonyesha uwepo wa fursa katika taaluma hiyo, hivyo wanafunzi wenye uwezo huo wanapaswa kuichangamkia.
“Utakumbuka hivi karibuni Serikali ilitangaza nafasi za ajira katika kada ya afya, zipo nafasi hazikujazwa kwa sababu ya walioomba hawakukidhi vigezo, wanafunzi wakasome fursa zipo,” alisema.
Kinyume na mtazamo huo, Profesa Anna Sikira alisema kulingana na uhalisia wa ulimwengu kwa sasa, taaluma ya kilimo ni fursa muhimu inayopaswa kukimbiliwa na wanafunzi.
Pamoja na fursa ya kuajiriwa katika sekta hiyo, pia inajitegemea na kumwezesha msomi kujiajiri.
“Tanzania tuna ardhi nzuri, tuna mito na maziwa, tuna hali nzuri ya hewa haya yote yanaonyesha fursa ilivyo pana katika kilimo,” alisema Profesa Sikira wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA).
Alisema iwapo mtu atasoma kilimo, hatalazimika kufikiri kuajiriwa pekee kwa kuwa zipo fursa lukuki zitakazomwezesha kujiajiri.
Mtazamo wa Profesa Sikira unatofautiana na Profesa Zacharia Mganilwa wa Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) aliyetaka wasomi kuchagua fani zitakazowapa ujuzi na maarifa.
Alisema ujuzi na maarifa utawasaidia wakati ambao fursa za ajira zitakosekana, watakuwa na uwezo wa kufanya kitu mbadala.
Kilimo na Afya ni fani zilizotajwa na Profesa Deus Ngaruko wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kuwa na fursa kubwa kwa wasomi kutokana na mahitaji yake.
Kuhusu kilimo, alisema kila siku ulimwengu unahitaji kula, kadhalika Serikali imekuwa ikiweka mikakati ya kuzalisha kwa wingi ili kukidhi mahitaji ya viwanda hivyo hiyo ni fursa.
Alisema uzuri wa fursa ya kilimo hazipo kwenye kuajiriwa pekee, Bali hata kuajiajiri.
Fani nyingine aliyoitaja ni Afya, akisema Tanzania ina Zahanati na Vituo vya Afya kila eneo ambavyo kimsingi vinahitaji wahudumu.
“Pia Afya ni hitaji la msingi ambalo kila siku watatokea watu watakaotaka kupata tiba, kwa vyovyote Serikali itaendelea kuajiri watumishi wa kada hii. Ni muhimu wanafunzi wakaisome,” alisema.
Wanafunzi waaze kufanya kazi za mikono kisha wakasomee kuziboresha kazi hizo, alisema Profesa Deus Ngaruko.
Badala ya mtu kuchagua fani itakayomjenga kuwa muajiriwa, alisema ni vyema waanze kujijenga katika kazi binafsi kisha wakasome kupata maarifa zaidi ya kuzikuza kazi hizo.
“Elimu yetu inamuandaa mwanafunzi akafanye kazi akimaliza akaikosa lawama zinakuja kwa aliyemfundisha, vema watoto waandaliwe kufanya kazi kisha waende vyuoni kusomea kazi hizo,” alisema.
Alisema hiyo itaongeza uhakika wa kile ambacho mwanafunzi anakwenda kusoma, badala ya kusomea kitu ambacho hana uhakika kama kitakuwepo.
Alieleza kuwa kutokuwepo kwa utaratibu huo, kunamfanya mwanafunzi asome kitu ambacho hatakutana nacho katika uhalisia wa maisha yake.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Dk Jimson Sanga alisema katika taifa kwa sasa vipaumbele vyake kwa sasa ni kuimarisha utalii na katika kukuza sekta ya utalii ni pamoja na uwekezaji hivyo ni wakati muafaka kwa taifa kufikiria uwekezaji katika elimu.
“Taifa letu sasa linategemea utalii lakini hatujafanya uwekezaji huko. Ninashauri wasome mahusiano ya kimataifa, lakini taifa pia liimarishe kozi hizo na zipewe kipaumbele ni kitu kizuri sana. Tanzania tunacho chuo chetu kule Kigamboni ambapo zinatolewa pia kozi za diplomasia lakini wakati umefika tulenge kimataifa,” alisema.
Sanga alisema Tanzania iwekeze kwa nguvu kuimarisha sekta ya utalii, “Huwa inaniuma sana utakuta raia wa nje akiwekeza Tanzania mtenda kazi wake ni Mkenya, kwanini tusiwe sisi? Hii ni fursa kwa vijana kuchangamkia kuna nafasi nyingi huko.
Alitaja maeneo mengine kuwa ni kukosekana kwa walimu katika kozi za hesabu na sayansi kuwa ni eneo pia lenye uhitaji.
Fursa za Kiswahili
Lugha ya Kiswahili nayo imeendelea kushika kasi na tayari imekwisha kutangazwa kila Julai 7 kuwa siku ya Kiswahili duniani hivyo kukiongezea fursa ndani na nje ya nchi.
Baadhi ya mataifa kama Afrika Kusini, Uganda zimekwisha kukitambua na kutangaza kuanza kufundisha Kiswahili nchini mwao hivyo kuchochea fursa za ajira kwa wanaosoma Kiswahili.
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango akizungumza katika maadhimino ya siku ya Kiswahili alitoa maagizo mbalimbali ikiwemo nyaraka zote za Serikali, dhifa na shughuli serikali, miradi na mikataba iandikwe kwa Kiswahili.
Dk. Mpango aliagiza balozi zote za Tanzania ughaibuni zianze kufundisha Kiswahili na wakufunzi watoke Tanzania ambao wameidhinishwa na Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) na Baraza la Kiswahili Zanzibar(Bakiza).
Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana yeye alitaka kutopuuzia kujifunza lugha za kigeni wakati wakiendelea na jitihada ya kukikuza na kukieneza Kiswahili ili kuweza kufaidika na fursa zinazozalishwa.
Alisema soko la Kiswahili duniani linalokadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 1.3 na kuongeza licha ya kuwepo kwa fursa nyingi za Kiswahili duniani, Tanzania bado hatujanufaika ipasavyo na fursa hizo.
Aliongeza ili Watanzania wawe na ushindani katika kufundisha, tafsiri na ukalimani na fursa zingine za Kiswahili kimataifa ni lazima wajue lugha zinazotumika katika nchi hizo.
Hivyo alitahadharisha juhudi za kukuza Kiswahili ndani na nje ya nchi, zisiwe na maana ya kupuuza lugha nyingine muhimu.
Akiunga mkono kauli hiyo, Mhadhiri wa masomo ya Afrika nchini Marekani na aliewahi kuwa Mwenyekiti chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (Chaukidu) Profesa Beatrice Mkenda, alisema kuwa Tanzania imekuwa ikisifika kote ulimwenguni kwa kuwa na wazungumzaji wa Kiswahili sanifu lakini bado fursa hizo zimekuwa zikichukuliwa na watu kutoka mataifa mengine akitolea mfano nchi jirani ya Kenya.
Profesa Mkenda mwenye uzoefu wa miaka 10 katika ufundishaji wa lugha hiyo nchini Marekani alieleza kuwa hiyo inasababishwa na wakenya wanaoomba fursa hizo mbali na kujua lugha ya Kiswahili, vilevile wanakuwa ni wajuzi wa lugha zingine za Kimataifa ikiwemo Kingereza haswa katika upande wa kuzungumza.
Akitolea mfano kupitia uzoefu wake wa kufundisha masomo ya Afrika, ikiwemo na lugha ya Kiswahili nchini Marekani alisema ameona fursa hizo mara nyingi wanaofanikiwa kuzipata ni kutoka nchini Kenya kutokana na wengi wao wana ujuzi wa lugha mbili yani Kingereza na Kiswahili.
“Wao wanapoandika maombi yao na kujieleza kwa nini wanataka hizo fursa wazungumzaji wa lugha ya Kingereza wanawaelewa zaidi kuliko baadhi ya Watanzania ambao wanakuwa mahiri zaidi katika lugha ya Kiswahili pekee,”alisema.
“Tunapozungumzia fursa za lugha ya Kiswahili hatuzungumzii Tanzania pekee kwani kuna mataifa mengine yanazungumza pia Kiswahili na kutokana na wao kuzungumza vizuri lugha ya Kingereza pamoja na lugha za mataifa mengine wafundishwaji wa lugha ya Kiswahili waliopo katika nchi hizo wanawaelewa zaidi,”alisema.
Naye Mhadhiri kutoka Idara ya Lugha za Kigeni na Fasihi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Eliakimu Sane alisema ni muda sasa wadau mbalimbali wakiwemo wataalam wa lugha pamoja na wadau wa elimu kuangalia ni namna gani wahitimu wa hapa nchini wanaandaliwa kupigania na kuweza kuzipata fursa mbalimbali zinazozalishwa na lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi.
“Pia uhimizaji wa kujifunza lugha za kigeni ni vyema ukaanzia katika ngazi ya msingi hadi vyuo vikuu ili mwanafunzi anapohitimu masomo yake pamoja na kile alichojifunza lakini aweze pia awe na uwezo wa kuzungumza Kiswahili pamoja na lugha nyingine za kigeni kama Kiingereza, Kifaransa au Kichina kwa ufasaha,”alisema.
Habari hii imeandikwa na Juma Issihaka, Herieth Makweta na Mariam Mbwana, Mwananchi