Trump achafua hali ya hewa tena, atangaza ushuru mpya kwa nchi zote duniani

Muktasari:
- Rais Donald Trump wa Marekani ametangaza vikwazo kwa mataifa yote duniani akidai kuziwekea ushuru mpya mkubwa kwa kile anachoeleza kuwa ni kukuza uzalishaji wa ndani wa taifa hilo. Uamuzi huo unatajwa kusababisha mfumuko wa bei na vita ya kibiashara.
Washington DC. Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza kuzilima vikwazo nchi zote duniani ikiwemo kutangaza ushuru mpya mkubwa kwa mataifa washirika wa kibiashara wa taifa hilo ikiwamo Tanzania.
Shirika la Habari la Associated Press limeripoti leo Alhamisi Aprili 3, 2025, kuwa Trump ametangaza uamuzi huo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika bustani ya Rose Garden nchini humo.
Miongoni mwa washirika wa biashara wa Marekani watakaoathirika zaidi na ushuru huo ni pamoja na China ambayo Trump ametangaza kuweka kodi ya asilimia 34 kwenye kila bidhaa inayoingizwa Marekani, huku kwa upande wa Tanzania ushuru utatozwa asilimia 10 kwa bidhaa inayoingizwa na kutoka nchini humo.
Uamuzi huo unatajwa kuwa ni hatua inayotishia kuvuruga mfumo wa uchumi wa dunia na kusababisha vita vya kibiashara kati ya mataifa hayo.
Katika hotuba yake, Trump amesema anapandisha viwango vya ushuru kwa mataifa yanayofanya biashara na Marekani, huku akiweka kodi ya msingi ya asilimia 10 kwenye kila bidhaa inayoagizwa kutoka mataifa mengine duniani.
Rais huyo asiyeishiwa vitimbwi amesema ushuru huo unalenga kuinua sekta ya uzalishaji wa ndani ya nchi na akieleza kwamba tangu kumalizika Vita Kuu ya Pili ya Dunia (WWII), Marekani imekuwa ikiporwa, kuharibiwa na kuumizwa na mataifa mengine duniani.

Trump amesema anachukua hatua hizo kuingiza mabilioni ya dola kwenye mzunguko katika Serikali ya Marekani na kurejesha usawa katika biashara ya kimataifa.
“Walipa kodi wa Marekani wameporwa kwa zaidi ya miaka 50, lakini hilo halitatokea tena kuanzia sasa,” amesema Trump.
Dharura ya kitaifa
Katika hatua nyingine, Trump ametangaza dharura ya kitaifa ya kiuchumi ili kuhalalisha ushuru huo. Ameahidi kwamba hatua hiyo itarejesha ajira za viwandani Marekani na akidokeza kuwa anatambua kuwa sera zake zinaweza kudhoofisha uchumi, huku wafanyabiashara wakikabiliana na ongezeko kubwa la bei.
Trump alitekeleza ahadi muhimu ya kampeni kwa kuweka ushuru aliosema ni wa “kisawasawa” kwa washirika wa biashara, akitumia mamlaka yake chini ya Sheria ya Nguvu za Dharura za Kimataifa ya 1977 bila kuhitaji idhini ya Bunge.
Hata hivyo, hatua yake kumuweka pabaya kisiasa, kwani baadhi ya maseneta wa Chama cha Republican, hasa kutoka majimbo yanayojishughulisha na kilimo na mipakani, wameeleza hofu yao kuhusu kuwekwa ushuru huo.
Hisa za Soko la Marekani zimeporomoka kwa kasi usiku wa leo baada ya kutangazwa ushuru huo, huku hofu ya kudhoofika kwa uchumi ikiongezeka.
“Kutokana na tangazo hilo, ushuru wa Marekani utakaribia viwango ambavyo havirekodiwa tangu Sheria ya Ushuru ya Smoot-Hawley ya 1930, ambayo ilisababisha vita vya kibiashara duniani na kuzidisha kuyumba uchumi (Great Depression) ,” amesema Scott Lincicome kutoka Taasisi ya Kiuchumi ya Cato.
Viwango vipya vya ushuru vinatarajiwa kuleta maumivu na kilio katika mataifa mengi yanayotegemea kuuza bidhaa kwa wingi nchini Marekani hususani China.
Serikali ya Trump imekokotoa viwango vya ushuru kulingana na nakisi ya biashara na mataifa hayo, kisha ikapunguza kiwango hicho kwa nusu, hatua ambayo Trump ameiita ya ‘huruma sana’.
Ikulu ya White House imesema nakisi ya biashara iliyotokana na ushuru na usawa wa biashara imefikia Dola za Marekani 1.2 trilioni mwaka 2024.
Mkuu wa Utafiti wa Uchumi kutoka Taasisi ya Fitch Ratings nchini Marekani, Olu Sonola, amesema wastani wa ushuru unaotozwa na Marekani utapanda kutoka asilimia 2.5 mwaka 2024 hadi 22 mwaka huu.
“Mataifa mengi huenda yakaingia katika mtikisiko wa uchumi,” anasema Sonora.
Ushuru kuongezeka zaidi
Ushuru huo mpya unaotokana na tangazo utagusa asilimia 25 kwenye magari yanayoagizwa kutoka nje ya Marekani; ushuru kwa China, Canada na Mexico; na vikwazo vilivyopanuliwa vya biashara kwa chuma na aluminiamu.
Trump pia ameweka ushuru kwa mataifa yanayoagiza mafuta kutoka Venezuela na anapanga kuongeza ushuru wa bidhaa kama dawa, mbao, shaba na chipu za kompyuta.
Mexico ni miongoni mwa nchi ambazo hazitakabiliwa na viwango vya juu vya ushuru ikilinganishwa na vile ambavyo tayari zinatozwa, kwani Trump amedai kuwa ni juhudi za kuzuia uhamiaji haramu na biashara ya dawa za kulevya kutoka katika mataifa hayo kwenda Marekani.
Hata hivyo, ushuru wa asilimia 20 kwenye bidhaa kutoka China kutokana na nafasi yake katika utengenezaji wa Fentanyl utaongezwa juu ya kiwango cha asilimia 34 kilichotangazwa na Trump.
Hofu kwa Democratic, Republican
Maofisa waandamizi wa Serikali, ambao walisisitiza kutotajwa majina, walisema ushuru huo utakusanya mabilioni ya dola kila mwaka. Ushuru wa asilimia 10 utaanza kutozwa kuanzia Jumamosi wiki hii, huku viwango vya juu vikianza kutumika Aprili 9, mwaka huu kwenye kila bidhaa inayoingia Marekani.
Trump aliondoa msamaha wa ushuru kwa bidhaa za China zenye chini ya Dola za Marekani 800 na anapanga kuondoa misamaha kwa mataifa mengine.
Wachambuzi wa nje wanatabiri kuwa uchumi wa Marekani utapata changamoto kutokana na ongezeko hilo na kudhoofisha ukuaji wa uchumi.
Mwanachama wa Chama Democratic, Suzan DelBene kutoka Washington, amesema suala la ushuru ni mojawapo ya dosari ndani ya utawala wa Trump.
“Rais hapaswi kuwa na mamlaka ya peke yake kuongeza ushuru wa kiwango hiki bila idhini ya Bunge,” amesema DelBene.
Wafuasi wa Republican wanaomuunga mkono Trump wamekiri kuwa ushuru huo unaweza kuvuruga uchumi na kusababisha ukosefu wa ajira cha asilimia 4.1.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Mike Johnson, kwa tiketi ya Republican kutoka Louisiana, amesema: “Tutaona jinsi hali inavyoendelea. Inaweza kuwa na changamoto mwanzoni, lakini naamini mwishowe italeta manufaa kwa Wamarekani.”
Mataifa yajibu
Tayari mataifa washirika wa Marekani yanayoathiriwa moja kwa moja na ushuru huo yameanza kuweka mikakati ya kujibu mapigo dhidi ya uamuzi huo wa Trump.
Canada tayari imeweka ushuru kwa bidhaa zake, huku Umoja wa Ulaya ukipandisha ushuru kwa bidhaa za Marekani zenye thamani ya kuanzia Yuro bilioni 26 (Dola za Marekani bilioni 28).
Kwa upande wake, China imetoa taarifa ikisema: “Ulinzi wa biashara hauwezi kusaidia na vita vya ushuru havina mshindi.”
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.