Kivuko cha MV Kigamboni chapata hitilafu

Kivuko cha MV Kigamboni
Muktasari:
- Mbunge wa Jimbo Kigamboni Dk Faustine Ndungulile, amewatahadharisha wananchi wanaofanya safari za kwenda na kutoka jimboni humo kuwa moja ya vivuko MV Kigamboni kimepata hitilafu na kiko kwenye matengenezo.
Dar es Salaam. Mbunge wa Jimbo Kigamboni Dk Faustine Ndungulile, amewatahadharisha wananchi wanaofanya safari za kwenda na kutoka jimboni humo, MV Kigamboni ambacho ni moja ya vivuko vinavyofaya safari zake kati ya Feri na Kikamboni, kuwa kimepata hitilafu na kiko kwenye matengenezo.
Hata hivyo amewatoa hofu wananchi hao kwa kuwaambia kuwa matengenezo hayo yanatarajia kukamilika saa saba mchana, leo Jumamosi Julai 23, 2023.
Dk Ndungulile ameyasema hayo leo katika akaunti zake, kwenye mitandao ya kijamii ya twitter na instgram, ambapo pia wananchi mbalimbali wametoa maoni yako wakimshukuru kwa kuwa mwepesi kutoa taarifa, lakini wakihoji ni lini tatizo la vivuko kuharibika litakuwa historia.
“Kivuko cha MV Kigamboni kimepata hitilafu. Matengenezo yanaendelea. Wenye magari mnashauriwa kutumia daraja la Nyerere. Matengenezo yanatarajia kukamilika saa 7 mchana. Aidha, nimejulishwa kuwa mfumo wa malipo umetengemaa,” ameandika Dk Ndungulile.
Hata hivyo mmoja wa watu wanaomfuatilia mbunge huyo katika akaunti yake ya Twitter, Gody Idabu, licha ya kushukuru kwa taarifa hiyo, amehoji ni mikakati ipi imewekwa ili kuondoka na taarifa hasi juu ya vivuko hivyo.
“Mheshimiwa, upo vizuri kwenye kutoa taarifa mapema ila ‘for how long’ (ni kwa muda gani) tutakuwa tunaendelea kupata taarifa ‘negative’ (hasi) tu, itakuwa vyema kama utaweza kutuambia miakakati gani inafanyika kuimarisha suala la vivuko, ili siku moja tukute hapa taarifa ‘positive’ (chanya) kuhusu vivuko na iwe kikomo cha hizi taarifa mabaya,” ameandika Idabu.
Kwa upande wa Instagram, Leody Mboya amehoji: “…hivi huu mradi utatutesa hivi mpaka lini mheshimiwa? Yaani mtu unaweza kufika feri ukasubiria kivuko ata kwa dakika 40 mpaka saa, na hii haijalishi kama ni vizima au vibovu. Kwanini hawajali mda wa watu? Mheshimiwa kuna jambo la ziada linahitajika kutatua hizi kero kabisa sio kila siku kivuko kimesumbua mara malipo, inachosha sana.”
Katika majibu yake, Dk Ndungulile ameandika: “…Fuatilia mtazamo wangu na msimamo wangu kuhusu jambo hili. Ni muumini wa huduma za vivuko kubinafsishwa."
Hata hivyo Mboya ametaka ufuatiliaji zaidi kwa kuandika: “…zidi kulipigania mheshimiwa. Binafsi huwa nakwazika sana na utaratibu wa utoaji huduma pale feri. Tunapoteza muda mwingi sana na hata kuathiri uchumi wetu.”