Kigamboni walia adha kivuko kuharibika

Muktasari:
- Wananchi wanaokaa Kigamboni jijini Dar es Salaam na vitongoji vyake, jana walipata adha ya usafiri baada ya kivuko cha Mv Magogoni kuharibika na kushindwa kufanya safari zake kama ilivyo kawaida.
Dar es Salaam. Wananchi wanaokaa Kigamboni jijini Dar es Salaam na vitongoji vyake, jana walipata adha ya usafiri baada ya kivuko cha Mv Magogoni kuharibika na kushindwa kufanya safari zake kama ilivyo kawaida.
Hali hiyo ilisababisha kivuko cha Mv Kigamboni kuelemewa na abiria walikuwa wakivuka kutoka upande mmoja kwenda upande wa pili, huku wakijazana, magari yakizuiliwa kuvuka kutokana na kivuko hicho kuwa kidogo.
Akizungumza na Mwananchi, Meneja vivuko kanda ya mashariki na kusini kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme (Tamesa), mhandisi Lukombe King’ombe alisema kivuko cha MV Magogoni kiliharibika jana alfajiri, baada ya mtambo wake mmoja kugoma kuwaka wakati kikijiandaa kuanza kutoa huduma.
“Kivuko hiki cha MV Magogoni kimeharibika leo alfajiri (jana) wakati walipotaka kuwasha kwa ajili ya kuanza oparesheni, mtambo mmoja uligoma kuwaka, hali hiyo ilisababisha tushindwe kufanya huduma,” alisema King’ombe na kuongeza:
“Tumeanza kufanya matengenezo kwa kuweka vipuri na hadi sasa tunavyoongea na wewe tunaendelea na matengenezo na tunatarajia kukamilisha matengenezo yetu jioni (jana)”.
Alisema athari walizozipata ni kwamba hawakuweza kuvusha magari kutoka upande mmoja kwenda mwingine, kutokana na kivuko kinachofanya kazi kuwa ni kimoja na hakikuwa na uwezo wa kubeba magari mengi tofauti na kivuko cha MV Magogoni, ambacho ni kikubwa na kina uwezo wa kubeba magari mengi kwa wakati mmoja.
King’ombe alisema Kivuko cha MV Kigamboni kina uwezo wa kupakiza abiria 800, magari 22 na tani 170 za mizigo kwa wakati mmoja, wakati kivuko cha MV Magogoni kina uwezo wa kupakiza abiria 2,000, magari 60 na tani 500 kwa wakati mmoja.
“Kutokana na kuharibika kivuko hiki kikubwa, tuliweka utaratibu wa kuwaingiza kidogo kidogo abiria tu kwenye kivuko cha MV Kivukoni kwa sababu kama unavyojua kivuko hiki ni kidogo...hivyo tukaweka utaratibu kikijaa, abiria inabidi wasubiri,” alisema.
Eneo hilo lina vivuko vitatu, ambavyo ni MV Magogoni, MV Kivukoni na MV Kazi.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mhandisi huyo, kivuko cha MV Kazi kipo kwa mkandarasi kinafanyiwa matengenezo makubwa.
Wananchi walia adha
Wakiongea na Mwananchi, baadhi ya wakazi wa Kigamboni wanaofanya biashara zao nje ya mji, walisema kuharibika kwa kivuko kimoja kulisababisha kuchelewa kwao kazini.
“Mimi nauza duka, natakiwa nifungue saa moja kasoro lakini leo nimefungua saa nne, haya yote ni mateso kwa sababu tulikaa kusubiri kuvuka pantoni yenyewe ilikuwa moja, yaani acha tu dada,” alisema Veronika Mbise, mkazi wa Kibada.
Kwa upande wake, Haruna Maulidi, mkazi wa Mji Mwema, alisema yeye alitakiwa kusafiri na boti kwenda Zanzibar, lakini changamoto ya kivuko ilisababisha ashindwe kusafiri na hivyo kuahirisha safari.
“Hizo gari zilizopaki pembeni wamegoma tu kuondoka kwa sababu walitangaziwa tangu asubuhi baada ya kivuko kikubwa kuharibika, walitangaziwa kupitia spika zilizopo hapa kwenye sehemu ya kupumzika abiria. Waliambiwa watafute njia nyingine mbadala ya kupita kwa sababu kivuko kinatoa kipaumbele kwa watembea kwa miguu,’’ alisema.