Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kituo cha kukuza, kuhifadhi tamaduni za Wasukuma mbioni

Muktasari:

  • Ujenzi wa kituo hicho cha kumbukumbu za Wasukuma kitasaidia kuendeleza mila na desturi na kuwawezesha vijana na kizazi kijacho kuzifahamu hivyo kuwaepusha kuiga tamaduni za nje.

Shinyanga. Katika kuhakikisha mila na desturi zinalindwa na kuwaepusha vijana kuiga tamaduni za kigeni, Mtemi Makwaiya wa tatu wa Busiya, Austini Makani ameweka wazi mpango wa kujenga kituo cha kukuza na kuhifadhi utamaduni wa Wasukuma.

Hayo yameelezwa leo Julai 9, 2025 na Mtemi Makani ambaye anakuwa chifu wa 24 wa Sanjo ya Busiya Ukenyenge wilayani Kishapu, ambapo amesema kuwa hatua hiyo  itasaidia kizazi kijacho kujifunza na kuthamini asili yao kutokana na vijana kuanza kusahau tamaduni zao.

Amesema lengo la kuanzisha kituo hicho ni kuiwezesha jamii hasa vijana kujua tamaduni za kabila la Wasukuma ikiwemo namna wanavyoshiriki katika shughuli za kilimo, vyakula wanavyokula na wanavyocheza ngoma zao.

Amesema kituo hicho kitatumika kuonyesha utamaduni wa kisukuma na kuwawezesha Watanzania kujifunza, pia itakuwa ni sehemu ya kupata tiba mbadala bila kutumia dawa za viwandani, hatua itakayochochea mabadiliko kwa jamii na mtazamo wa watu wengi.

“Mategemeo yangu hapa Busiya tuwe na kituo kikubwa cha kumbukumbu za kabila la Wasukuma huu ndiyo mpango uliopo,maana sasa hivi vijana wameanza kusahau tamaduni za kitanzania na kuiga mambo ya nje ambayo mengine yanakiuka maadili yetu,” amesema Mtemi Austin Makani.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Boniface Butondo amesema teknolojia imechangia kuleta mabadiliko makubwa yanayokuja na changamoto ya vijana na vizazi vijavyo kusahau mila na desturi za makabila yao na kuanza kuiga tamaduni za kigeni.

Baadhi ya wakazi wa Kishapu wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti akiwemo Maria Jimwaga wamesema ujenzi wa kituo cha kumbukumbu za Wasukuma kitasaidia kuendeleza mila na desturi na kuwawezesha vijana na kizazi kijacho kufahamu tamaduni za kabila lao.